Nov 2, 2013

MATOKEO DARASA LA SABA KITAIFA, SHULE YA ASIYESOMA YAONGOZA MKOA WA MBEYA



NA INDABA AFRICA

Shule ya mfanyabiashara  maarufu wilayani Mbozi Bwana Lington Chaula ambaye hakufanikiwa kupata elimu miaka yake ya ujana, imeshika nafasi ya kwanza katika mkoa wa Mbeya na nafasi ya tisini kitaifa katika matokeo ya darasa la saba yaliyowekwa hewani jioni hii

Ilasi imekuwa shule ya  kwanza kimkoa na pia ya kwanza katika wilaya ya Mbozi kwa kuwa na wanafunzi 29 ambapo kati yao waliopata wastani wa daraja la  A (kwanza) ni  11 na waliobakia wamepata daraja B.

Matokeo hayo yanaonyesha pia shule mojawapo isiyotarajiwa ya IZYANICHE iliyopo kwenye moja ya pori la wilaya Mbozi imefanya vizuri kwiwilaya na kuchukua nafasi ya tano

Kwa matokeo hayo, inathibitisha nia ya Mzee Chaula kuonyesha kusikitishwa kwake kwa kushindwa kupata elimu bora na kudhamilia kuwapa fulsa watanzania wengine kupitia uwekezaji alioufanya kwenye elimu kuanzia chekechea hadi kidato cha sita.

Mzee Chaula katika moja ya vipindi vilivyorushwa na TBC mwanzoni mwa mwaka huu alikaririwa akifafanua mbele ya mwandishi aliyekuwa akimhoji kuwa anajisikia uchungu anapoona watoto hawapati elimu na kuendelea kuzurura mitaani

Katika hali ya kuonyesha kujali suala la elimu alifika mahala akatoa machozi wakati akizungumzia adha ya kutokuwa na elimu huku akikumbuka namna ambavyo kwa upande wake alikosa elimu.

Alisema wakati akiwa tayari amejiimarisha kibiashara alilazimika kuajiri mwalimu wa kumfundisha kiwango ambacho kilimwezesha kumudu majukumu ya biashara zake na kwenda na teknolojia za sasa ikiwemo matumizi ya kompyuta kwaajili ya kutunza kumbukumbu mbalimbali za biashara zake.

Anasema ni mazingira hayo yalimsukuma kuanzisha shule kama moja ya maeneo ya uwekezaji ambapo alianzisha Ilasi English Medium School ambayo iliwezesha pia kuanzishwa kwa shule za sekondari kidato cha kwanza hadi cha nne, na tano hadi sita.

Kwa sasa kampuni ya Ilasi pia inamiliki kituo cha Redio cha Ilasi FM ambacho kimeendelea kuwa zana muhimu ya kutoa elimu katika jamii na kuongeza kasi ya mabadiliko ya fikra miongoni mwa wananchi katika maeneo kinakosikika mkoani mbeya pamoja na mikoa jirani.

Shule maarufu mkoani mbeya za Umoja, St. Mary's, Mkapa na zingine nyingi zimefungashwa tela na Ilasi iliyopo wilayani Mbozi kwa matokeo hayo ya darasa la saba.

Kwa matokeo haya, sekeseke la walimu wakuu kujichuja kutokana na shule zao kufanya vibaya ndiyo msimu wake ambapo inatarajiwa kuwa katika vikao vya madiwani, yataibuka ya kwanini shule fulani imetuwakilisha vibaya?