Nov 4, 2013

MSIMU UMEANZA WA KILIMO, JE NA MWAKA HUU WANANCHI WATAUZIWA MBOLEA MBOVU?

 MWAKA ULIOPITA WILAYA YA MBOZI ILIKUMBANA NA MATUKIO YA UDANGANYIFU KWA MAKAMPUNI KUUZA MBOLEA ISIYOFAA KWA SHUGHULI ZA KILIMO
 HAPA IKIWA INAPAKIZWA KUREJESHWA DAR ES SALAAM KWAAJILI YA KWENDA KUHARIBIWA
GARI LINALOSAFIRISHA LIKIWA LIMEPIGWA KUFULI NA FUNGUO KUKABIDHIWA KWA ASKARI POLISI WALIOPEWA JUKUMU LA KUSINDIKIZA MBOLEA HIYO HADI DAR E SSALAAM

Na Mwandishi wa Indaba blog.
Msimu umeanza huku wananchi wakikumbuka vidonda vya msimu uliopita baada ya wafanyabisahara na makampuni kuwaingiza kingi kwa kuwauzia pembejeo zilizo na viwango vya chini ama zilizopitwa na wakati.

Itakumbukwa na wananchi wa wilaya ya Mbozi kuwa Mamlaka inayosimamia ubora wa Mbolea iliingia wilayani humo na kufungia moja ya maghala yanayouza mbolea hiyo baada ya kubaini kuwepo kwa mbolea iliyoganda, lakini kwa mshangao wa wananchi baada ya miezi miwili kibali cha yule yule aliyefunga ghala hilo kilitolewa kikiagiza uongozi wa wilaya uruhusu ghala hilo liendelee na biashara.

Ni mazingira hayo hayo yanayowafanya wananchi kuwa na mashaka na msimu huu huku wakijiuliza je mambo yatakuwa yale yale kama ya mwaka jana?

Ni msimu huo wa mwaka jana ambapo wakulima waliuziwa mbegu za Mahindi zilizowekwa rangi ya mikeka kwenye viwanda vidogo vidogo vilivyopo mafichoni katika mji wa Mlowo ambapo licha ya makampuni yanayouza mbegu za mahindi kuitwa na kutoa ushahidi wakati wa ukamataji, ushirikiano ulikuwa mdogo hii ikidhaniwa kuwepo mikono ya wafanyakazi wa makampuni ya mbegu kwenye biashara hiyo haramu.

Ni msimu huo huo ambapo pia dawa za kupulizia mashambani zilipobainika kuuzwa zikiwa zimekwisha muda wake na hivyo kuendeleza wimbi na malalamiko kuwa shughuli ya Kilimo ni eneo la kutengeneza fedha za haraka haraka kupitia wakulima na hasa wakati wa msimu wa kilimo unapoanza ambapo kila kitu kuanzia zana za kulimia zinakuwa feki, mbolea feki, mbegu feki, madawa mengine feki na hadi vibarua feki!

Wakati hayo yakitokea, wataalamu wa Kilimo wilayani wanapasha kuwa kwa msimu huu mbolea inayotarajiwa kupatikana kwa wingi wilayani Mbozi ni Minjingu. majanga mengine haya!

Kwa muda mrefu kumekuwepo malalamiko kutoka kwa wakulima wakizungumzia kutofanya vizuri kwa mbolea hiyo wilayani Mbozi, lakini serikali kutokana na uzalendo kwenye makampuni ya ndani inasisitiza kuwa mbolea hiyo inafaa baada ya kufanya kitu kinaitwa "soil testing"

Licha ya hoja za wawakilishi wa wakulima kwenye vikao mbalimbali kutaka kujua mstakabali wa matumizi ya mbolea  hiyo ni wazi Minjingu imepewa heshima rasmi kutamba katika kilimo cha mahindi wilayani mbozi kwa lengo la kurejesha hali ya udongo ambao umeendelea kupoteza rutuba ya asili  kutokana na matumizi ya mbolea za kisasa za chumvi.

Nia ni njema lakini wakulima wanajiuliza majaribio haya yanafanyikia kwenye mikono yao wakati hali ya uhakika wa chakula haiashirii mbolea hiyo kuleta mafanikio? 

Nami najiandaa kwenda shambani nikitarajia kuwa serikali itakuwa sikivu pale nitakapouza debe moja la mahindi kwa bei ya kuruka kutokana na hatua zote za uzalishaji kuandamwa na ufeki hadi kunisukuma niuze kwa bei feki!!! kwaherini!!!