Nov 4, 2013

PAMOJA NA KUELEZWA SUALA LA MKOA MPYA LIMEKWISHA, WANANCHI WAHOJI NANI AMESIKILIZWA?

Wananchi wa eneo jipya linalopendekezwa kuwa Mkoa wa  Songwe wameendelea kuhoji mwelekeo wa suala hilo kutokana na awali kuleta mvutano kwenye vikao vya maamuzi na uongozi wa mkoa  kusukuma ajenda ya makao makuu isipewe uwanja wa kujadiliwa na baadaye kamati ya ulinzi na usalama ilibariki maamuzi hayo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesema mapendekezo yanayoelezwa kusogezwa kwa mheshimiwa raisi ndiyo yale yanayopingana na mapendekezo ya wilaya zinazounda mkoa huo mpya ambapo suala la Makao makuu ya Mkoa huo mpya linalezwa kufanywa kwa kuridhishana 

Unajua kilichotokea ilifika mahala mwenyekiti akatamka " ninyi si mmepata jina la Mkoa, basi na wenzenu wapate makao makuu " alieleza mmoja wa wajumbe wakati akirejea yaliyojitokeza kwenye mchakato waugawanji mkoa kwenye vikao vya RCC

suala hilo lilichokonolewa kwenye kikao cha RCC hivi karibuni lakini, lilizimwa na Mwenyekiti kwa kueleza kuwa walishapeleka kwa Mh Rais mapendekezo na muhtasari wa maamuzi ya mkoa huo  na kinachosubiriwa sasa ni maamuzi ya Mh Rais kutangaza anavyoona yeye.

Licha ya wilaya za Mbozi,Ileje na Momba kufikia hatua ya kuhoji nani mwenye haki ya kufanya maamuzi ya maeneo yanayolengwa , Suala la kurejewa maamuzi ya makao makuu ya mkoa huo yameonekana kuwa na kigingi kizito kana kwamba hakuna utaratibu wa kujisahihisha kwenye utendaji wa serikali" anaeleza Mwananchi mwingine katika kujadili suala hilo

Suala hilo kwa sasa limeachwa mikononi mwa chama cha Mapinduzi katika kuliwasilisha kwa Mheshimiwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa ili kuliangalia kwa mtazamo tofauti na ule wa watendaji wa serikali ambao wamewasilisha mapendekezo yanayolalamikiwa na wajumbe wa kikao cha RCC kutoka wilaya za Mbozi, Ileje na Momba kuwa msimamo wa mwenyekiti ulikuwa umejielekeza kupeleka makao makuu Mkwajuni.

Kwa taratibu za ziara za Mh Rais mikoani, pamoja na kupokea taarifa ya serikali kupitia mkuu wa mkoa, pia chama tawala huandaa tarifa yake na kuiwasilisha kwake ambapo huelezea kwa undani matatizo, changamoto na mafanikio ya ukuaji wa chama na utoaji huduma ambapo pia humulika kasoro za kiutendaji kwenye mkoa husika.
Inadhamiliwa kuwa suala la ugawaji mkoa wa Mbeya litajitokeza kwenye taarifa za chama sasa na hata
 katika ziara za mheshimiwa raisi atakazozifanya katika wilaya zinazounda mkoa mpya, na kuna wakati ambapo viongozi wa makundi ya jamii kama madiwani  kwenye vikao vyao wamewahi tamka kutaka kuendelea na mkoa wa zamani ili kuepuka mgawanyo wa mkoa usio na tija na hasa inapokuwa kwenye makao makuu yake.

Wengi wanatafsiri hali hiyo kuwa ina msukumo wa aliye na kisu kikali ndiye hula nyama, kwa maana ya kuwa Naibu waziri wa elimu Mh Mlugo amekuwa na "influence" katika kufikia maamuzi ya kupeleka makao makuu ya mkoa wa Songwe kwenye eneo lake la utawala (jimboni mwake) kwa kufanya ushawishi kwenye meza ya mwenyekiti wa RCC.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mh Abas Kandoro alishatoa ufafanuzi mara kadhaa juu ya kuhusishwa na kupindisha maamuzi ya ugawaji wa mkoa na hususani suala la makao makuu yaliyopendekezwa kuwa Mkwajuni, kuwa suala hilo limezingatia vigezo na nimaamuzi yaliyobarikiwa na kamati ya ulinzi na usalama.

Alishafafanua kuwa hana maslahi yoyote na maamuzi hayo kwakuwa yeye si mkazi wa mkoa wa mbeya na kwamba akishastaafu atarejea mkoani kwake Iringa, hivyo msukumo wa kupeleka makao makuu wilayani Chunya ni katika kuhakikisha dhana ya maendeleo kwa uwiano inazongatiwa.

Suala hili sasa  limebakia likijadiliwa kwenye makundi ya Kisiasa na hasa kwenye chama cha Mapinduzi ambapo mijadala ya kusimamia misimamo na maslahi inaonekana kuchukua nafasi zaidi, huku vigezo vya maamuzi vikionekana kutowekwa mezani mapema kabla mchakato huo haujaagizwa kuanza kwenye ngazi za chini.