Jan 5, 2016

REA WAPOKELEWA VIJIJINI KWA SAHANGWE LAKINI....

Wakazi wa kata ya Kigala wamepongeza hatua ya wakala wa Umeme vijijini REA kutekeleza mpango wa usambazaji wa umeme katika kijiji kimoja cha kata hiyo, hata hivyo wameonyesha hofu yao kutokana na mradi huo kuonyesha dalili za kuishia kijiji kimoja!Ingawa hakuna maelezo ya kitaalamu juu ya sababu za mradi huo kusimama licha ya kazi ya survey kufanywa hadi kijiji cha Kigala,ni kijiji cha Mlengu pekee ambacho mradi huo umeshatekelezwa na mkandarasi anaonekana kumalizia usambazaji kwenye kijiji hicho pekee.Hali hiyo imemsukuma mheshimiwa Diwani wa kata hiyo Nguvila kuanza kufuatilia ngazi za juu kutokana na kuelezwa kuwa mkandarasi wa mradi wa kupeleka umeme kijiji cha Kigala ni mwingine.Kwa ujumla jitihada za kuunganisha umeme vijiji vya kata ya Ikuwo na Kigala katika wilaya ya Makete zimepokelewa kwa mikono miwili na wananchi wa maeneo hayo na kupongeza jitihada za mbunge wao aliyemaliza muda wake Dr Binirith Mahenge ambaye aliasisi mchakato huo na kuusimamia. Wanaeleza kuwa matarajio yao ni kuona kuwa Mbunge wa sasa Mh Dr Norman Sigala anatoa msukumo zaidi katika kuhakikisha vijiji vilivyopangwa kutekelezewa mradi huo vinanufaika.Kwa mazingira ya vijiji hivyo kupata umeme wanaona ni sawa ya ndoto ya mchana kwakuwa tangu uhuru wamekuwa wakihangaika na miundombinu hasa barabara na hawakutegemea suala la umeme hivyo hatua ya sasa ni dalili ya ukombozi kiuchumi kwa wananchi hao na kwamba kutachangia uanzishaji wa viwanda vingi vijijini.