Apr 3, 2011

TEC yaihadharisha Serikali

BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limeitahadharisha Serikali kuwa tofauti kubwa ya kipato miongoni mwa wananchi inaweza kusababisha kutoweka kwa amani nchini. Katibu Mkuu wa TEC, Padri Antony Makunde alitoa tahadhari hiyo katika hafla ya viongozi wa dini ya kuombea amani jijini Dar es Salaam ambapo alisema amani iliyopo sasa hapa nchini inaweza kutoweka kama serikali haitafanya juhudi za kuondoa tofauti hiyo. “ Tuilinde amani iliyopo kwa kumaliza kero za wananchi, umaskini unaweza kusababisha tunu ya amani tuliyonayo ikatoweka,” alisema Makunde. Katika hafla hiyo iliandaliwa na Jumuiya ya Waislam Waahamadiyya, Padri Makunde alisema ikiwa Serikali haitaheshimu misingi ya kidemokrasia inaweza kusambaratisha amani ambapo alitaja pia kashfa dhidi ya dini za wengine kuwa ni jambo linaloweza kusabababisha kutoweka kwa amani. Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira alisema matatizo ya kiuchumi yaliyopo nchini yasiwe sababu ya kutoweka kwa amani. “ Tuna matatizo ya kiuchumi, lakini hiyo isiwe sababu ya kutoweka kwa amani, amani ikitoweka uchumi hauwezi kuimarika,” alisema Wasira. Kiongozi wa Jumuiya ya Waislam Waahamadiyya nchini, Tahir Chaudhry alisema lengo la kuandaa hafla hiyo ni kuomba amani kwa pamoja kwa sababu kila dini inahubiri amani. “ Hakuna dini inayohubiri uvunjifu wa amani, hiyo haitakuwa dini, ndiyo maana tumeona tuwaalike wenzetu wakristo ili tuombee amani kwa pamoja,” alisema.
"