May 28, 2011

MAMA SALMA AWATAKA VIONGOZI WA UWT KUSHIRIKIANA NA WASOMI





Na Anna Nkinda – Maelezo, Dodoma
Wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) nchini wametakiwa kushirikiana na vijana wasomi katika kufanya kazi zao ili kuboresha utendaji wao wa kazi kwani nguvu kazi zaidi itatokana na vijana hao na siyo vinginevyo.
Wito huo umetolewa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanachama wa umoja huo katika ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa hivi sasa vijana wasomi wanafanya kazi zao na kushindana kwa hoja zenye nguvu kutokana na elimu waliyo nayo hivyo basi kama wataamua kuwatumia umoja huo utanufaika na kuwa na mabadiliko ya kiutendaji.
“Shirikianeni na wasomi wa vyuo vikuu, wafundisheni kazi, wapeni nafasi na siyo kuwapinga kwa kuwaona kuwa wao wanajua zaidi kuliko ninyi kwani hivi sasa Dunia imebadilika inaenda sambamba na teknolojia hivyo basi ni rahisi kwa vijana kufahamu mambo mengi tofauti na wazee na mkumbuke kuwa ili muweze kushindana ni lazima mfanye mageuzi,” alisema mama Kikwete.
Aidha Mama Kikwete aliwasisitiza kina mama hao kuwa na tabia ya kutunza siri na kuhifadhi yale yote ambayo yanajadiliwa ndani ya vikao vya Chama na siyo kuyaongea nje kwa watu wasiohusika.
Mwenyekiti huyo wa WAMA pia aliwataka wanawake hao kuongeza juhudi ya kuwahamasisha akinamama wengi zaidi kujitokeza kuwania uongozi katika nafasi za majimbo na kata , kwani ni dhahiri kwamba wanawake wengi wamejitokeza kwenye nafasi za viti maalum kuliko za kata na majimbo.
Alimalizia kwa kuwasisitiza kina mama hao kuongeza ushirikiano kupitia vikundi vya maendeleo ya kiuchumi kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia wanawake wengi zaidi kufaidika na fursa zilizopo chini ya mipango ya Serikali ya kumkomboa mwanamke.
Akisoma taarifa ya UWT ya mkoa wa Dodoma Katibu wa umoja huo Amina Kanyogoto alisema kuwa wamekuwa wakihamasisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi kwa kufanya semina kwa kila kata, kutoa semina kwenye mabaraza ya wilaya na mkoa, kutoa ushauri nasaha kupitia kwa viongozi wao kujitokeza kwenda kupima kwa hiari na kutoa semia kwa waelimisha rika.
Aliyataja mafanikio waliyoyapa hadi sasa ni wanawake wengi kuwa na mwamko wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi zote baada ya kuhamasishwa na pia kina mama wengi wamekuwa na ari ya kufanya biashara ndogondogo za kujitafutia kipato cha familia zao.
Kanyogoto alisema, “matatizo yanayotukabili ni ukosefu wa fedha kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za uzalishaji mali kwa wajasiriamali wanawake, mikopo inayotolewa haitoshelezi mahitaji na bidhaa zinazotengenezwa na kina mama bado ni tatizo kwa ajili ya ukosefu wa masoko na uuzaji wa bidhaa hizo.”
Mama Kikwete yupo mjini Dodoma kwa ajili ya kuhudhuria matembezi ya uchangishaji wa chakula kwa shule za msingi yatakayofanika kesho tarehe 29/5/2011 yaliyoandaliwa na Shirika la Chakula Duniani (WFP) kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali ya hapa nchini.
Mwisho.