Oct 12, 2011

NAPE: WANAOPIGA SARAKASI KUTAFUTA MAAMUZI YA KUJIVUA GAMBA YAFUTWE WATAULA WA CHUYA

Nape akizungumza na Waandishi wa habari leo Dar
KATIBU wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye leo amezungumza na waandishi wa habari, katika ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, Ifuatayo ni taarifa kamili kama alivyoisoma kwa waandishi hao:-
Kumekuwepo na juhudi za muda mrefu sasa kutaka kupotosha au hata kushawishi kubadili kabisa maamuzi ya Chama juu ya dhana nzima ya kufanya mageuzi ndani ya Chama (KUJIVUA GAMBA).
Juhudi hizi zimekuwa zikifanywa na kikundi kidogo sana cha watu wachache ambao kwa namna moja ama nyingine wameathiri wanamageuzi haya tunayoyafanya.
Tatizo kakikundi kenyewe kana nguvu kiasi ya pesa jambo linalofanya kelele zao ziwe kubwa lakini zisizo na mashiko.
Juhudi hizi za kujaribu kuhujumu mageuzi haya ndani ya chama zimekuwepo kwa muda mrefu sasa na tumejitahidi sana kuzipuuza, lakini nadhani umefika wakati wana CCM na Watanzania kujua ukweli walau kwa kiasi ya kinachoendelea.
Wanaofanya juhudi hizi wanadhani hatuzifahamu kwa sababu tu tumekaa kimya wakati wakicheza sarakasi zao za kujaribu kuupotosha umma.
Chama tunafahamu na kufuatilia kwa makini kila kinachoendelea hakuna tusichokijua juu ya juhudi hizi na zingine nyingi zikiwemo jitihada za kutaka kumhujumu hata Mwenyekiti mwenyewe. Nasisitiza tunazifahamu.
Juhudi za hivi karibu ni zilikuwa za kutaka Chama kishindwe Igunga ili kujaribu kuhalalisha hoja ya kwamba mageuzi tuyafanyayo hayana tija kwa Chama.
Juhudi hizi zilifanyika bila kificho, tunajua hazikuwa na nia njem akwa Chama ila zilisukumwa na uroho na ubinafsi zikiwa na ujasiri mkubwa wa kifisadi, bila kujali masilahi mapana ya Chama kama taasisi na nchi yetu kwa ujumla.
Baada ya kushindwa kwa juhudi hizo Igunga, sasa wanaanza kujaribu kutumia watu mbalimbali kuimba wimbo wao wa zamani kuwa tunapotosha dhana ya kujivua gamba bila kusema usahihi ni upi kama tunachokifanya ni kupotosha.
Ikumbukwe huu sio wimbo mpya uliimbwa sana mara tu baada ya kutangaza maamuzi ya NEC.
Bahati nzuri vimeshakaa vikao vya Kamati Kuu karibu mara mbili, ambavyo vyote vimepongeza utekelezaji wa haya mageuzi ndani ya chama.
Mapema mwaka huu Baraza Kuu la UVCCM Taifa chini ya Uenyekiti wa Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa katika taarifa yake kwa vyombo vya habari walipongeza utekelezaji wa maazimio ya NEC.
Sasa pengine tujiulize kama wana CCM na Watanzania kwa ujumla hawa wanaodai tunapotosha maamuzi ya NEC ni kina nani na kwa masilahi ya nani?
Naendelea kusisitiza hakuna kilichopotoshwa.
Ushindi wa Igunga kwenye uchaguzi mdogo, pamoja na ule wa chaguzi ndogo za Udiwani kwenye kata kumi na saba kati ya ishirini na mbili zilizofanya uchaguzi ni uthibitisho wa kukubalika kwa mageuzi tuyafanyao.
Nachukua nafasi hii kuwashukuru sana wa na CCM nawananchikwaujumlakuungamkonomageuzituyafanyayokwaniMwalimualishatuasa “BILA CCM MADHUBUTI NCHI YETU ITAYUMBA”
Walikwenda na kaulimbiu Igunga “TUSHINDWE ILI TUHESHIMIANE” wakasahau kuwa Chama ni taasisi si mtu, ushindi ule Igunga na kwenye kata mbalimbali ni Ushindi wa wana CCM na wapenda nchi hii wote! …Hivyo basi “TUMESHINDA ILI TUHESHIMIANE” Bahati mbaya kwao hawa kutegemea kutokea yaliyotokea.
Nawasihi wasiweweseke watulie na kutafakari upya wayafanyayo huku wakikumbuka…HAKUNA TUSICHOKUJUA.
Nichukue nafasi hii kuwaomba wana CCM nchi nzima kutulia na kuzipuuza juhudi hizi kwani tukifanyacho ni kwa masilahi mapana ya Chama chetu na nchi yetu, hakuna sababu ya kutiwa hofu, kila kitu kiko salama.
SABABU YA KUSHINDA TUNAYO, NIA YA KUSHINDA TUNAYO NA UWEZO WA KUSHINDA TUNAO.
Malengo mengine makubwa waliyo kuwa nayo kupitia kushindwa kwa CCM Igunga kama kungetokea ili kuwa kuipa nguvu kampeni yao kubwa na ya muda mrefu ya kujaribu kujenga hoja ya kutenganisha Uenyekiti waTaifa wa CCM na Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Bahati mbaya kwao na wapambe wao mambo yamekwenda kinyume na dua zao. Changa moto ni nayo itoa kwao, kwa nini wasitoke wenyewe kutoa madai wayatoayo hadharani badala yake wanatumia watu?
Hii hoja ya kutenganisha kofia kama ina masilahi kwa chama nasi kwa kikundi kidogo kwa nini wanatumia nguvu ya pesa kutaka kushawishi wajumbe? Anayeamini kwa nini asiilete kikaoni bila kushawishi watu kwa pesa?
Mwenendo wa siasa nchini unadhihirisha kuwa upinzani hauna nguvu kiasi hicho ila unapata nguvu ndogo waliyo nayo kutoka kwa kikundi hiki kidogo sana cha Wanaojiita wana CCM lakini kwa kweli ni waasi.
Wengi wao walianza kwa kuasi Imani ya CCM na sasa wana endesha kampeni ya watu kuasi maamuzi halali ya vikao halali vya Chama chetu.
Naomba niwakumbushe TULIAMUA, TUKAAHIDI NA TUTATEKELEZA HAKUNA KINACHOBADILIKA KWA SARAKASI ZA BARABARANI, WANAPOTEZA MUDA.
Yaliyobaki yanayofanywa na wapambe na wanaotaka kutumiwa ya kimaadili tutayashughulikia kwenye vikao. Chama cha siasa makini ni vikao.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Imetolewa na:-
Nape Nnauye
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
12/10/2011