Aug 4, 2012

Gazeti la NIPASHE: Magufuli amtega Meya wa Arusha hoja ya Lema

Gazet
Hoja ya kukiondoa kituo kikuu cha mabasi katikati ya jiji ambayo ilitumiwa na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) kujinadi katika kampeni zake za uchaguzi mkuu ulipita, sasa ametwishwa Meya wa Jiji Gaudence Lyimo (CCM).

Aliyemtwisha zigo hilo ni Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli na alifanya hivyo wakati akifungua mkutano wa wadau wakuu wa Mfuko wa Bodi ya Barabara uliofanyika jijini hapa juzi.

Magufuli alikuwa akizungumzia mikakati ya kuondoa foleni inayoanza kulinyemelea jiji la Arusha ambapo alisema moja ya ufumbuzi ni kuihamisha stendi hiyo ya mabasi.

“Ni vizuri Meya upo hapa, wekeni mikakati ya kuhamisha ile stendi, hakuna haja ya mabasi yote yanayokuja Arusha lazima yaingie katikati ya jiji,” alisema na kuongeza, “tena katika jiji hili mnaweza kuwa na stendi tatu za mabasi makubwa katika maeneo tofauti kulingana na mahitaji.”

Alitaja maeneo hayo ambayo ni nje ya jiji kuwa ni kwa mabasi yanayotokea barabara ya Moshi, yanayotokea Dodoma na Babati na stendi nyingine ni kwa mabasi yanayotokea barabara ya Namanga.


Hoja ya kuhamisha stendi ilikuwa ni moja ya ajenda katika mikutano ya kujinadi kuwania ubunge wa Arusha Mjini iliyokuwa ikihubiriwa na Lema ambaye pamoja na stendi pia alizungumzia azma yake ya kuhamisha soko kuu lililopo katikati ya jiji.

Hata hivyo, Lema hakufanikiwa kutimiza azma yake baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kumvua ubunge mapema Aprili, mwaka huu, baada ya mahakama kuridhika kwamba alitumia lugha ya kashfa dhidi ya aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya CCM, Dk. Batilda Burian.

Lema amekata rufaa kupinga hukumu hiyo na kesi bado haijapangiwa tarehe ya kusikilizwa.

Katika hatua nyingine Magufuli alisema wizara yake itahakikisha ujenzi wa barabara itakayounganisha kati ya barabara ya Arusha – Babati na Arusha – Namanga inajengwa na kukamilika ili magari yatokayo maeneo ya Babati kwenda Namanga na kinyume chake yasilazimike kupita katikati ya mji.

Alisema hayo wakati akijibu maelezo ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, ‘aliyemchomekea’ ombi hilo katika maelezo yake ya awali kabla waziri huyo hajafungua mkutano huo.

“Najua Mkuu wa Mkoa Mulongo ‘amenichomekea’ ujenzi wa barabara hii ili kuhakikisha magari yatokayo Babati kwenda Namanga na kurudi yasilazimike kupita mjini ili kupunguza foleni…nasema wizara itasaidia ujenzi huo ili ikamilike,” alisema.

Chanzo Nipashe