Oct 7, 2012

SHERIA YA UKIMWI YA MWAKA 2008 YADAIWA KUWA BUTU INAJIKANGANYA

Washiriki wa mafunzo ya sheria namba 8 ya mwaka 2008 ya kuzuia na kupambana na UKIMWI ambayo ni sehemu ya Kampeni ya asasi isiyo ya kiserikali wilayani Mbozi ya MSCHCD ambapo imebainika kuwa sheria hiyo imekuwa butu baada ya kutekelezwa kwa miaka minne sasa bila kunasa hata mtuhumiwa mmoja licha ya kuwepo kwa kasi ya watu wanaoambukiza kwa makusudi katika jamii

washiriki wakiandika jambo wakati wa majadiliano
Na Danny Tweve
Mbozi

Imebainishwa kuwa tangu rais asaini sheria  namba 8 ya kuzuia na kudhibiti maambukizi ya UKIMWI ya mwaka 2008, wilaya ya Mbozi haijaweza kumshitaki ama kumfikisha mtu mahakamani kwa makosa yanayotokana na sheria hiyo licha ya kuripotiwa mara kwa mara kwa vitendo vinavyoambatana na makosa ya sheria hiyo.

Kaimu Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI katika halmashauri ya wilaya ya Mbozi SADNESS NGETWA amekiri kutofikishwa mahakamani kwa shtaka lolote linalohusiana na sheria hiyo , licha ya kuwepo malalamiko kwenye jamii ya vitendo vinavyoonyesha uvunjifu wa sheria hiyo

Wakizungumza kwenye mafunzo ya Utekelezaji wa sheria hiyo wilayani Mbozi baadhi ya wadau kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali na viongozi wa dini na makundi ya watu wanaoishi na VVU wamesema hali hiyo inachangiwa na mkanganyiko wa sheria yenyewe juu ya wakati upi mtu atahesabika anaambukiza kwa makusudi ikiwa sheria yenyewe inazuia taarifa za mtu mwenye VVU kutangazwa.

Mratibu wa asasi ya Maendeleo ya jamii katika Mapambano dhidi ya UKIMWI wilayani Mbozi MSCHCD BI ZAINABU MAJUBWA amesema pamoja na udhaifu wa sheria hiyo, bado kuna umuhimu mkubwa kwa TACAIDS na wadau wa mapambano dhidi ya UKIMWI kuendelea kuisambaza sheria  hiyo ili ijulikane kwa wananchi ambao ndiyo walengwa wa sheria hiyo.
Wadau hao wamesema licha ya kuwepo kwa vitendo vya uambukizaji wa makusudi vinavyofanywa na baadhi ya watu wanaojitambua kuwa na maambukizi, bado kumekuwa na ugumu wa kuwashtaki wahusika kwakuwa taarifa zao bado ni siri na kwamba sheria hiyo imekuwa mwiba kwa wanandoa hasa wakati mjamzito anapoenda kliniki na kubainika kuwa  na maambukizi ambapo imekuwa vigumu kumshirikisha mwanandoa mwenzake kwa kuhofia kuvunja ndoa.

Bwana Loyd Nzowa mmoja wa washiriki katika mafunzo hayo amesema, bado licha ya kuonyesha kupinga unyanyapaa, sheria hiyo haijaweka misingi itakayowezesha utekelezaji wake kuwa usiyo na vikwazo kwakuwa hata upatikanaji wa huduma za tiba bado unachangamoto nyingi hii inatokana na shughuli za UKIMWI kwa ujumla kutegemea misaada kutoka nje  kwa asilimia 90 kitu ambacho hakitoi uhakika wa huduma kwa  WAVIU.

Mafunzo hayo yanaendeshwa na asasi ya Mbozi Society  katika kata tano  ikilenga kueneza sheria  ya Kuzuia na kupambana na UKIMIWI ya mwaka 2008, kwa kujielekeza kwenye vifungu vya 7 na 8 vinavyohusiana na haki  na wajibu kwa  watu wanaoishi na VVU  na nisehemu ya ufadhiri wa Foundation for Civil Society.