MH RAHIM MUSHI -HAKIMU MFAWIDHI WILAYA YA MBOZI NA MOMBA AKIZUNGUMZA NA MTANDAO HUU JANA
Na Danny Tweve wa IndabaBlog
Hakimu mfawidhi wa mahakama za Mbozi na Momba Mh Rahim Mushi amesema ucheleweshaji wa nakala za hukumu kutoka mahakama za mwanzo wilayani humo unatokana na mazingira ya mahakama hizo kutokuwa na wachapaji (typists) na badala yake kumtegemea mpiga chapa mmoja aliyeko katika mahakama ya wilaya Mbozi
Akizungumza na mtandao huu kuhusiana na changamoto zinazokabili idara ya mahakama, Mh Mushi amesema pamoja na jitihada za kupunguza msongamano wa kesi katika mahakama hizo, suala la nakala za hukum limekuwa kero kwa wananchi hasa katika mahakama za mwanzo zilizombali na mahakama ya wilaya ya wilaya Mbozi
Akitolea mfano mahama ya mwanzo ya Kamsamba ambayo ipo umbali wa kilometa 146 kutoka makao makuu ya wilaya ya Mbozi inafanya zoezi la uchapaji kuwa gumu kutokana na eneo hilo kutokuwa na gari la idara ya mahakama wala piki piki na matokeo yake kutegemea siku hakimu anaenda mahakama za wilaya ama wakati wa ukaguzi wa mahakama ndipo mafaili hubebwa.
Alisema hali hiyo inaweza kuchelewesha haki kwa wananchi hasa pale wanapotaka kukata rufani, hivyo kukosa mahala pa kurejea, na kwamba hatua za sasa ni kuomba idara ya mahakama kuweka mazingira yatakayowezesha hatua za utoaji haki kuwa karibu na wananchi
Alisema katika mazingira kama hayo wakati mwingine suala hilo linaweza kuchukua zaidi ya miezi miwili kusubilia nakala za hukumu kitu ambacho alisema kinaweza kutafsiriwa kuwa si utawala wa sheria hasa kwa chombo cha mahakama kinachotegemea kutoa haki
hata hivyo amepongeza mazingira ya mahakama yanayoendelea kuboreshwa hasa katika eneo la upatikanaji wa shajala na posho za mahakimu kwa wakati kitu ambacho amekiri kuwa ni mapinduzi makubwa kwa idara hiyo ikilinganishwa na huko nyuma
Mh Rahim Mushi akisalimiana na DSO wa Mbozi bwana Msangi katika viwanja vya mahakama ya wilaya ya Mbozi huku mahakimu wengine wakibadilishana mawazo nje ya viwanja hivyo. |