May 27, 2013

KIMONDO YAANZA RAUNDI YA PILI YA MABINGWA WA MIKOA KWA KUTOA KICHAPO CHA BEBERU JIZI!




Timu ya Kimondo SC ya wilayani Mbozi katika mkoa wa Mbeya imeendelea kutakata katika raundi ya pili ya ligi ya Mabingwa wa Mikoa baadaya kuisukutua bila dawa timu ya Mji ya Njombe bao 1-0 juzi katika mchezo uliofanyika uwanja wa sabasaba  mjini Njombe

Katika mchezo huo ambao tangu kuanza kwake ulikuwa ukionyesha jitihada za wazi za kuhitajika mbeleko kwa timu ya wenyeji, hali iliendelea kuwa tete kadiri dakika zilivyokuwa zikienda mbele kutokana na mbinu za hapa na pale za mwamuzi kushindwa kupenya ili kuleta madhara kwa upande wa Kimondo.

Kimondo licha ya majaribio kadhaa vipyenga vya kuotea vilionekana kuharibu ladha ya mchezo kiasi cha mashabiki wa Njombe kushindwa uzalendo na kuamua kushabikia timu ya Kimondo ambayo ilionekana kutandaza soka lenye ladha mithiri ya asali ya Ilomba na Idiwili.

Katika dakika za mkiani, baada ya majaribio kadhaa ya kuingia eneo la hatari na kupigiwa vipyenga vya kuotea, ndipo staili ya “mpime huko huko mbali” ilipoanza na haikuchukua muda mrefu kwani gonga kama nne kutoka kwenye lango la Kimondo zikielekezwa kwenye lango la timu ya Mji Njombe ziliwezesha shuti la umbali wa mita 52.56  kuleta sherehe kwa upande wa Kimondo baada ya kumpima kipa wa Mji Njombe na katika maeneo hatarishi na kusababisha timu ipumulie mashine mbele ya mashabiki wake uwanja wa nyumbani.

Ushindi huo ulipakatwa kama mwali na timu ya Kimondo kwani jitihada zote za kujaribu kuondoa aibu uwanja wa nyumbani kwa Mji Njombe hali iliendelea kuwa ngumu na hadi dakika kumi zilizoongezwa na mwamzi kumalizika bado Njombe walionekana kuzidiwa pumzi.


Nyongeza ya dakika ilionekana dhahiri shairi kutaka kusababisha kilio cha bao la pili hivyo mwamzi akajikuta anapuliza filimbi huku akiangalia huku na kule kuhofia uongozi wa mkoa uliokuwa upo uwanjani na kushuhudia timu yao ikitoka imetota huku wageni kutoka Mpakani wakizungumza Kinyiha,Kiwemba,Kinyaki na  kinyamwanga huku maneno “Nyinza sana” tununu fijo”, natemwa, na tukuvifyondomola” yakisikika kwa furaha


Mchezo wa marudiano baina ya  Kimondo SC ya Mbeya  na Mji Njombe unatarajiwa kufanyika katika uwanja wa sokoine mjini Mbeya Jumapili Juni 2 mwaka huu.

Chachandu ya ligi hiyo inashamihilishwa na namna timu zilivyojipanga kuhakikisha ushindi kwa kufanya usajiri wa kusugulia meno kwa tupa!!

 Meneja wa timu ya Kimondo ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya Mbozi Erick  Minga anafafanua kuwa mchezo wa marudiano itakuwa ni kuanika unga wa mhogo kiangazi, kwani timu yake imejaindaa vilivyo.

 Timu zingine zinazoshiriki ligi hiyo na mikoa yake kwenye mabano ni pamoja na Friends Rangers ya Dar es Salaam, African Sports ya Tanga, Abajalo ya Dar es Salaam,Kariakoo ya Lindi, Machava FC ya Kilimanjaro ,Mpwapwa Stars ya Dodoma,Stand United FC ya Shinyanga na Magic Pressure ya Singida


Nyingine ni Polisi Jamii ya Bunda mkoani Mara, Biharamulo FC ya Kagera, Saigon FC ya Kigoma na Katavi Warriors ya Katavi.

Timu zitakazofuzu kucheza raundi ya tatu zitacheza mechi za kwanza kati ya Juni 8 na 9 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitakuwa kati ya Juni 15 na 16 mwaka huu.