May 26, 2013

ZAMBI AFAGILIA JK KUVUNJA BODI YA KAHAWA


 

Na Danny Tweve Mbozi,

 Mbunge wa Mbozi Godfrey Zambi amesifu hatua ya Mheshimiwa rais Jakaya Kikwete  kusikiliza hoja aliyoiibua bungeni na hatimaye kuivunja bodi ya Kahawa aliyowahi kuilalamikia bungeni kuwa  imeundwa kwa upendeleo wa ukanda.

Akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara ulioambatana na ugawaji  wa madawati kwa shule ya msingi ya Ichenjezya katika mamlaka ya mji wa Vwawa, Mbunge huyo amesema ingawa hoja hiyo ilionekana kubezwa hatimaye imezaaa mabadiliko aliyoyafanya mheshimiwa rais kwa kuteua bodi mpya ambayo sasa itaongozwa na Dr Juma  Ngasongwa

Alisema mwaka jana alimwandikia waziri wa Kilimo Christopher Chiza  kupinga uteuzi uliofanywa na waziri wa Kilimo wakati huo Profesa Jumanne Maghembe ambapo Dr Eve Hawa Sinare iliteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi hiyo huku wajumbe watano wa kamati hiyo wakitokea  mkoa mmoja.

Katika barua yake ya Juni 4, 2012, Mh  Zambi pamoja na kumwandikia waziri wa kilimo pia alinakili barua hiyo kwa Mh Rais Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro  akielezea kukiukwa kwa sheria na utungwaji wa kanuni za zao la kahawa bila kuzingatia taratibu.

Anasema bodi hiyo ya awali ilikuwa na wajumbe ambao wengine walikuwa na migongano ya kimaslahi na wengine kutojulikana makundi wanayowakilisha tofauti na bodi ya sasa ambapo imehusisha wajumbe kutoka maeneo yote ambayo Kahawa inalimwa.

Anaeleza kuwa anafurahi kusimama mbele ya wananchi kuwa rais amesikiliza kilio hicho na kuivunja bodi hiyo pamoja na kuiteua bodi nyingine ambayo sasa inahusisha maeneo yanayozalisha zao hilo.

“ ninafuraha kuwaelezeni leo hii kuwa tarehe 30 na 31 mwezi huu wadau wa kahawa watakutana mkoani Morogoro kuzungumzia maendeleo ya zao la Kahawa mkiwa na bodi mpya ambayo ina uwakilishi niliokuwa naupigania na kuusimamia” alieleza Mh Zambi.

Amesema katika suala la kutetea maslahi ya wananchi wake yupo tayari kuitwa vyovyote ilimradi anasimamia ukweli, na kwamba katika hilo kuna wakati alilaumiwa na kuonekana akitofautiana na waziri aliyeteuliwa na chama chake, na kwamba alifanya hivyo kwakuwa anatambua kuwa alikuwa akiwakilisha maslahi ya wapiga kura wake na wazalishaji wa kahawa nchini kote.

Amesema ni vyema pia wananchi wake wakatafakari kwa makini kauli iliyokuwa ikisisitizwa na Mbunge wa awali wa jimbo hilo marehemu Halinga kuwa wananchi wa wilaya hiyo wanapaswa kuwasomesha watoto wao ili kuepuka kuwa chakula cha wasomi.

Alisema neno hilo si zuri sana kulizungumzia mbele ya jamii lakini ni ukweli kwamba pasipo kusomesha watoto wao, wataendelea kuwa watumwa wa jamii iliyosoma ambayo ndiyo yenye fulsa za kufanya maamuzi huku wao wakiwa watekelezaji tu

Akiwa kwenye mkutano huo uliofanyika nje ya uwanja wa shule  ya msingi ya Ichenjezya Mh Zambi alitoa msaada wa madawati 100 yenye thamani ya shilingi Milion sita kwa shule ya Ichenjezya na kufikisha idadi ya madawati 180 ambayo amekwisha yatoa kwa shule hiyo kwa ushirikiano na mamlaka ya bomba la mafuta TAZAMA.
MWISHO