Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi imeagizwa kusimamia ukusanyaji wa mapato yake ya ndani kwa asilimia 100, ili iweze kutekeleza miradi yake iliyopangwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi akiwa na wajumbe wenzake wa kamati ya Fedha ya Halmashauri hiyo ametoa msimamo wa madiwani wakati akizungumza na wananchi kata ya Isansa baada ya kamati hiyo kujiridhisha na ujenzi wa kituo cha afya unaofanywa kwa njia ya Force account.
Amesema wakati zimesalia siku chache kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2017/2018 ni vyema wataalamu wakatambua kuwa Halmashauri ya wilaya haijafanikiwa kutekeleza baadhi ya miradi ya Maendeleo kutokana na mapato kidogo ya ndani ambapo hadi kufikia Juni Mosi Halmashauri imefikia asilimia 78 ya makusanyo yake ya ndani hata hivyo kuna vyanzo vingi zikiwemo leseni za biashara ambazo bado hazijaweza kukusanywa vyema, hivyo mkakati wake kwa sasa ni kujielekeza kukusanya kwenye vyanzo hivyo sambamba na mazao baada ya msimu wa mavuno kuanza.
Kutokana na hatua hizo tayari timu ya mapato ya Halmashauri ya wilaya ya Mbozi imeundwa ikihusisha wataalamu wa idara mbalimbali, huku kamati ya fedha ya Halmashauri hiyo ikikasimiwa majukumu ya kusimamia utendaji wa menejimenti katika kipindi chote ili kuhakikisha kuwa malengo yanafikiwa.
Kwa upande wao wataalamu wameahidi kutekeleza wajibu wao hasa katika suala la makusanyo na kwamba matarajio yao ni kuona kuwa Halmashauri yao inafanya vyema katika utekelezaji wa malengo yake ikiwemo miradi iliyopangwa.