Jun 4, 2018

VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA VINGI VYAVUKA KIKWAZO KWENYE VIGEZO 2017/2018

Vituo vya kutolea huduma za afya 19 tu kati ya 80 ndivyo vilivyopata nyota sifuri katika tathmini ya mwaka 2017/2018 imefahamishwa.
Wakitoa taarifa ya ukaguzi wa  hali ya vituo hivyo kwa kuzingatia mwongozo wa BRN, Wakaguzi wa wizara ya Afya wamesema kuna ongezeko kubwa la vituo vilivyovuka kutoka nyota sifuri hadi kuingia kwenye nyota moja ikilinganishwa na mwaka 2016.
Kwa mwaka 2016 vituo 45 vilipata nyota 0 kati yake vikiwemo zahanati 45 lakini kwa mwaka huu hali imekuwa tofauti ambapo Zahanati 19 kati yake 16 za serikali zimepata nyota sifuri, zahanati  48 zimepata nyota moja, 8 Nyota Mbili ambapo vimo vituo vya afya na Hospitali ya Misheini ya Mbozi na  Hospitali ya wilaya ya Mbozi imepata Nyota tatu.
Katika mchanganuo huo Zahanati ya Mbaya ambayo ni Binafsi imeshika nafasi ya mwisho kwa kupata wastani wa alama 0.
Katika uchambuzi huo miongoni mwa mapungufu yaliyobainishwa nipamoja na  vituo 63 kati ya 80 kutokuwa na vyoo seti tatu kama mwongozo unavyotaka ambapo inashauriwa kuwa na vyoo vya wanawake, wanaume na watoa huduma (wataalamu) kwenye majengo ya zahanati, aidha kukosekana kwa vyoo rafiki kwaajili ya walemavu na wenye mahitaji maalumu.
Katika ukaguzi huo kulikuwa na jumla ya Maeneo 12 yaliyowekwa kwenye makundi katika ukaguzi yakiangalia uwezo na uendeshaji wa vituo vyenyewe ikiwa ni pamoja na miundombinu yake, utendaji wa wataalamu, Matumizi ya zana, vitendanishi na takwimu za afya zilizopo kituoni katika kupanga mipango ya mbele, ushughulikiaji wa  huduma za dharura, mtazamo wa kumlenga mteja na uwajibikaji.