Adverts

Oct 9, 2013

KIMONDO YAOSHA NYOTA, YAIBABATUA 4-0 MKAMBA RANGERS YA MORO

Na Danny Tweve wa Indaba Blog

Ligi daraja la kwanza imeendelea kuchanua katika viwanja mbalimbali nchini ambapo katika uwanja wa CCM Mbozi wenyeji Kimondo wamesherehesha mashabiki wake baada ya kuitafuna Mkamba Rangers ya Morogoro mabao 4-0

Katika mchezo huo uliojaa ufundi na mashambulizi ya kasi, ulimalizika kwa wenyeji kuweka kibindoni pointi tatu, huku wageni wakiondoka vichwa chini,

Katika michezo mingine majimaji iliutumia vyema uwanja wake wa nyumbani  wakati ambapo Burkina Faso ya Morogoro ilisafiria nyota ya Kurugenzi  Mufindi  kwa kuifungana  bao 1-1

Kimondo ambayo katika mchezo uliopita ilitoka suluhu ya kutofungana na Burkina Faso ilionyesha dalili za ushindi tangu mchezo kuanza baada ya mashambulizi kadhaa ya kosa kosa kuliandama lango la Mkamba

Bao la kwanza la Kimondo lilipatikana mnamo dakika ya 32 kupitia kwa Christopher Kasekwa baada ya kuunganisha mpira wavuni ulopigwa kwenye adhabu ndogo

Bao la Pili la Kimondo liliwekwa wavuni kupitia kwa  Charles Hiza mnamo dakika ya 39  ambaye aliunganisha wavuni mpira uliotokea wingi ya kushoto kwa Christopher Kasekwa.

Hadi mapumziko  kimondo ilikuwa mbele ya bao 2, na kipindi cha pili mchezo uliendelea kwa timu ya Mkamba rangers kujaribu bahati yao lakini hali iliendelea kuwa tete kwa upande wao kwani mnamo dakika ya 87 Geofrey Mlawa aliipatia timu ya Kimondo bao la tatu .

Bao hilo lilitokana na piga nikupige iliyojitokeza langoni mwa Mkamba baada ya shambulizi lililofanywa na safu ya ushambuliaji ya Kimondo kufuatia gonga baina ya Charles Hiza, Geofrey Mlawa na Godfrey Magetha  na kupiga hodi kwenye lango la Mkamba huku kipa wake Noel Steven Mkachage akionekana kushindwa kumudu kutokana na ufupi

Bao  la nne liliwekwa wavuni na Bryson Mponzi dakika moja baada ya bao la tatu baada ya kuanzisha shambulio lililombambatiza mlinzi wa Mkamba Thabit Kameta na hivyo mpira huo kumfikia mfungaji ambaye alimchambua kipa wa Mkamba na kuhesabu bao hilo

Ingawa bao la tano liliwekwa wavuni dakika ya 90 mwamuzi alipiga filimbi kuwa kipa wa mkamba alikuwa amesukumwa na hivyo mchezo kumalizika kwa Kimondo ikitoka na ushindi wa bao 4 –0 dhidi ya  Mkamba ya Morogoro.

Baada ya mchezo viongozi wa Mkamba walionekana kulaumiana na wachezaji na Mwalimu  wake Amri  Ibrahimu alipohojiwa kama ana maoni yoyote juu ya mchezo huo alisema nafasi ya kuzungumza amemwachia msaidizi wake Mohamed Mgalike na meneja wa Timu Gaudence Mnyangao ambao walikataa kuzungumzia mchezo huo licha ya kukiri kuwa wamelizidiwa.



Gooooooooo, ndivyo Charles Hiza akizama  na wavu mara baada ya kuitupia bao timu yake  huku katen wa Kimondo Geofrey Mlawa akishangilia nyuma wakati kipa wa Mkamba Noel Steven Mkachage akiwa amelala chini anachungulia mpira ukiingia wavuni

Heka heka langoni mwa timu ya Mkamba Rangers ambapo   ilikuwa ni mnamo dakika ya 39 ambapo bao la pili lilifunhgwa na Charles Hiza

Hapa wachezaji wa Kimondo wakicheza ndombolo baada ya ushindi wa bao la Pili

Wachezaji wa Mkamba Rajab Kasimu akichuana na Abu Mwamengo katika mchezo mkali uliomalizika kwa kimondo kutoka na ushindi wa mabao 4 kwa 0 katika mchezo uliofanyika uwanja wa CCM Vwawa