Adverts

Jun 4, 2018

BENKI YA NMB YAJIELEKEZA KUJENGA UWEZO KWA VIKUNDI

Benki ya NMB Tawi la Mbozi na Mlowo kwa pamoja wameelezea nia yao ya kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Mbozi katika kushughulikia changamoto za ukuaji na uaminifu kwa vikundi vya wakulima ili mikopo inayopatikana iwe na tija kiuchumi 
Wakizungumza na menejimenti na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi, Timu ya wataalamu wa benki hiyo wamesema bado jamii ya wananchi wa Mbozi hawajafikiwa vyema na elimu ya Mikopo kiwango ambacho wengi wa wanaojitokeza kukopa  kutokujipanga vyema kulingana na mipango yao.
Wamesema ikiwa halmashauri inaona vyema kutoa huduma zake kupitia vikundi ni vyema wakaishirikisha benki hiyo ili kujenga uwezo na kuandaa wajasiliamali wenye nia ya dhati  ya kujikwamua na umaskini kwanza badala ya kuanzisha programu za hamasa juu ya mikopo mbalimbali bila kuwaandaa kwanza 

VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA VINGI VYAVUKA KIKWAZO KWENYE VIGEZO 2017/2018

Vituo vya kutolea huduma za afya 19 tu kati ya 80 ndivyo vilivyopata nyota sifuri katika tathmini ya mwaka 2017/2018 imefahamishwa.
Wakitoa taarifa ya ukaguzi wa  hali ya vituo hivyo kwa kuzingatia mwongozo wa BRN, Wakaguzi wa wizara ya Afya wamesema kuna ongezeko kubwa la vituo vilivyovuka kutoka nyota sifuri hadi kuingia kwenye nyota moja ikilinganishwa na mwaka 2016.
Kwa mwaka 2016 vituo 45 vilipata nyota 0 kati yake vikiwemo zahanati 45 lakini kwa mwaka huu hali imekuwa tofauti ambapo Zahanati 19 kati yake 16 za serikali zimepata nyota sifuri, zahanati  48 zimepata nyota moja, 8 Nyota Mbili ambapo vimo vituo vya afya na Hospitali ya Misheini ya Mbozi na  Hospitali ya wilaya ya Mbozi imepata Nyota tatu.
Katika mchanganuo huo Zahanati ya Mbaya ambayo ni Binafsi imeshika nafasi ya mwisho kwa kupata wastani wa alama 0.
Katika uchambuzi huo miongoni mwa mapungufu yaliyobainishwa nipamoja na  vituo 63 kati ya 80 kutokuwa na vyoo seti tatu kama mwongozo unavyotaka ambapo inashauriwa kuwa na vyoo vya wanawake, wanaume na watoa huduma (wataalamu) kwenye majengo ya zahanati, aidha kukosekana kwa vyoo rafiki kwaajili ya walemavu na wenye mahitaji maalumu.
Katika ukaguzi huo kulikuwa na jumla ya Maeneo 12 yaliyowekwa kwenye makundi katika ukaguzi yakiangalia uwezo na uendeshaji wa vituo vyenyewe ikiwa ni pamoja na miundombinu yake, utendaji wa wataalamu, Matumizi ya zana, vitendanishi na takwimu za afya zilizopo kituoni katika kupanga mipango ya mbele, ushughulikiaji wa  huduma za dharura, mtazamo wa kumlenga mteja na uwajibikaji.

HALMASHAURI YA WILAYA YA MBOZI YAJIELEKEZA KUFIKIA 100% YA MAKUSANYO

Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi imeagizwa kusimamia ukusanyaji wa mapato yake ya ndani kwa asilimia 100, ili iweze kutekeleza miradi yake iliyopangwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi akiwa na wajumbe wenzake wa kamati ya Fedha ya Halmashauri hiyo ametoa msimamo wa madiwani wakati akizungumza na wananchi kata ya Isansa baada ya kamati hiyo kujiridhisha na ujenzi wa kituo cha afya unaofanywa kwa njia ya Force account.
Amesema wakati zimesalia siku chache kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2017/2018 ni vyema wataalamu wakatambua kuwa Halmashauri ya wilaya haijafanikiwa kutekeleza baadhi ya miradi ya Maendeleo kutokana na mapato kidogo ya ndani ambapo hadi kufikia Juni Mosi Halmashauri imefikia asilimia 78 ya makusanyo yake ya ndani hata hivyo kuna vyanzo vingi zikiwemo leseni za biashara ambazo bado hazijaweza kukusanywa vyema, hivyo mkakati wake kwa sasa ni kujielekeza kukusanya kwenye vyanzo hivyo sambamba na mazao baada ya msimu wa mavuno kuanza.
Kutokana na hatua hizo tayari timu ya mapato ya Halmashauri ya wilaya ya Mbozi imeundwa ikihusisha wataalamu wa idara mbalimbali, huku kamati ya fedha ya Halmashauri hiyo ikikasimiwa majukumu ya kusimamia utendaji wa menejimenti katika kipindi chote ili kuhakikisha kuwa malengo yanafikiwa.
Kwa upande wao wataalamu wameahidi kutekeleza wajibu wao hasa katika suala la makusanyo na kwamba matarajio yao ni kuona kuwa Halmashauri yao inafanya vyema katika utekelezaji wa malengo yake ikiwemo miradi iliyopangwa.

May 29, 2018

DAWA YA KINGA YA VVU KULENGA MAKUNDI MAALUM

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo Mfuko wa Henry Jackson kutoka serikali ya Marekani wamo kwenye hatua za maandalizi kwaajili ya kutekeleza mpango wa utoaji dawa kinga kwa watu walio katika makundi maalumu ya jamii ambayo yapo kwenye hatari ya kuambukizwa.
Kulingana na taarifa za utekelezaji wa Mpango huo, wanawake wanaouza ngono pamoja na wanaume walio kwenye biashara hiyo watashiriki kwenye mpango huo baada ya hatua za awali ambapo watahamasishwa kujipima wenyewe na ikithibitika wana maambukizi wataunganishwa na huduma za CTC ikiwa ni pamoja na kuingizwa kwenye mpango wa matumizi ya dawa za kupunguza makali ARV's
Ama kwa upande mwingine wale ambao hawatakutwa na maambukizi, wataanza kutumia dawa kinga ambapo kila siku watawajibika kumeza kidonge kimoja kwa kipindi kinachofikia siku 21 mfululizo huku pia wakitumia njia za kinga zingine zinazoelekezwa kitaalamu. Hatua hiyo inalenga kupunguza uwezekano wa mtumiaji wa dawa kinga kuambukizwa na virusi ikiwa ataacha kutumia njia zingine ikiwemo matumizi ya Kondomu katika kipindi cha matazamio ya dawa.
Kutokana na takwimu kuonyesha nchini Tanzania asilimia 25 ya wanawake wanaouza ngono wamo kwenye hatari ya maambukizi na katika utafiti uliofanyika hivi karibuni walibainika kuwa na maambukizi ya VVU, wakati ambapo 26% wanaume wanaofanya ngono ya wanaume kwa wanaume pia walibainika kuwa na maambukizi wakati 36% ya wanaotumia dawa za kulevya pia walikutwa na maambukizi hayo.
Mpango huo utatekelezwa kwenye vituo vya afya vyenye huduma za CTC,kwa kuzingatia idadi ya wateja wanaotumia ARV's, Uwepo wa wataalamu waliopata mafunzo ya utoaji huduma kwa watu wanaoishi na VVU.
Kutokana na utaratibu huo si kila Mtanzania atafikiwa na Dawa Kinga hiyo hivyo imesisitizwa umuhimu wa watanzania kuendelea kutumia njia za kinga zilizoelekezwa na wataalamu ili hatua ya majaribio ya dawa Kinga ya sasa yaweze kupimwa kwenye kundi lengwa la wanaouza ngono kwa baadhi ya maeneo yaliyoingizwa kwenye mpango huo katika Mkoa wa Mbeya na Songwe.

UMISETA MOTO- SONGWE YAKOLEZA JIKO KUTETEA UBINGWA TAIFA

Timu ya Umoja wa wanafunzi wa Sekondari  -Mkoa wa Songwe, imo kwenye hatua za mwisho kwenda kushiriki mashindano ya Taifa yanayokusudiwa kufanyika Mkoani Mwanza. Timu hiyo imeundwa rasmi na orodha ya wachezaji kusomwa mbele ya afisa elimu Mkoa wa Songwe JUMA MHINA juzi katika uwanja waa shule ya sekondari ya Vwawa.
Timu hiyo yenye wachezaji 120 itawakilisha mkoa wa Songwe katika michezo ya Mpira wa Miguu kwa wanaume, Mpira wa Pete, Riadha, Mpira wa mikono, Mpira wa Kikapu na michezo ya ndani.Mkoa wa Songwe ndiyo bingwa wa taifa ka mwaka uliopita ambapo iliweza kuwadungua Unguja kwenye mpira wa Miguu katika fainali.

Jul 22, 2016

MKUU WA WILAYA YA MBOZI AWATAKA MADIWANI KUWAFUATILIA WALENGWA WA TASAFMkuu wa wilaya ya Mbozi Bw. John Palingo amewataka madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi kufanya ufuatiliaji kwa walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa chini ya TASAF awamu ya tatu.

Akitoa salamu za serikali, Mkuu wa wilaya ya Mbozi amesema kuwa hatua hiyo itawarudisha kwenye mstari walengwa kutokana na kuwepo taarifa za matumizi mabaya ya fedha wanazonufaika kupitia mpango huo

Katika hatua hiyo amesisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kutekeleza azma ya mpango huo kufikiwa .

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya ametangaza nia ya kurejesha na kuzifungua barabara za katikati ya mji wa Vwawa  na kwamba kitaitishwa kikao cha wadau wa maendeleo mji wa Vwawa ili kujadili jambo hilo mchana wa leo ama kesho asubuhi ili hatimaye kufikia maamuzi ya pamoja ya namna bora ya uendelezaji wa huduma ya usafiri na uchukuzi mjini.

Polisi Songwe yaja na Ligi ya vijana msimu wa mavuno


Jeshi la Polisi kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo wilayani Mbozi katika mkoa wa Songwe  wanakusudia kuanzisha ligi ya vijana itakayoanza kulindima mwezi August, 2016

Akizungumza na mtandao huu, Mkuu wa polisi wilaya ya Mbozi Henry Kyssima amesema hatua hiyo inalenga kubaini vipaji vya vijana na hatimaye kutumia ligi hizo kuwaunganisha na timu mbalimbali zinazoanza ligi hivi karibuni

Ligi zinazokusudiwa kuwavizia wachezaji hao ni pamoja na zile za ligi kuu, daraja la kwanza na daraja la pili ambazo tayari kufuatia mwaliko huo kuna ugeni mkubwa ambao umeanza kuvinjali katika wilaya ya Mbozi na vitongoji vyake kwaajili ya kusaka vipaji hivyo

Kyssima amesema anatambua kuwa kipindi cha August kuna shughuli nyingi za kiuchumi zinazoendelea wilayani hivyo katika kuendesha ligi hiyo, itasaidia pia kutumia muda wa mapumziko katika michezo badala ya kuelekeza fedha na mapato yao kwenye matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu

Amesema ligi hiyo itaendeshwa kwenye kanda tano na baadaye washindi wa kanda watakutanishwa hadi kupatikana kwa mshindi wa wilaya.

Jan 21, 2016

UTOAJI WA CHAKULA MASHULENI BADO CHANGAMOTO

Baraza la Madiwani wilaya ya Mbozi leo limeelezwa kuwa suala la utoaji wa chakula shuleni, bado limeendelea kukwaza mafanikio ya utendaji na ufaulu wa watoto kwenye shule za msingi.

Hayo yamejitokeza wakati wa kikao cha baraza la madiwani kupitia taarifa za kata ambapo imebainika kuwa shule nyingi ambazo hazikufanya vizuri kwenye matokeo ya darasa la saba ni zile ambazo hazina mpango wa chakula.

Shule ya Izyaniche ambayo mwaka juzi iliongoza kiwilaya katika miaka miwili mfululizo imekuwa ya mwisho kiwilaya na ni miongoni mwa shule 10 kimkoa za mwisho


Jan 8, 2016

SAMMATA AIPAISHA TANZANIA ,ANYAKUA TUZO

Hatimaye Mbwana Ally Sammatta ameiwakilisha vyema Tanzania baada ya kushinda miongoni mwa wachezaji wazawa wa Afrika kama mchezaji bora wa Mwaka anayechezea ligi za ndani ya Afrika
 Samatta anaungana na Mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang kutoka Gabon kuwa vinara wa CAF kama wachezaji bora wa mwaka 2015 kwa mara ya kwanza.

Samatta anakuwa mchezaji wa kwanza ukanda wa Afrika Mashariki kutwaa tuzo hiyo akiwa mchezaji bora anayeshiriki ligi za ndani barani Afrika

Mbwana Samatta amewafunika wenzake akiwemo mchezaji mwenzie wa Tp Mazembe  na kipa wa DRC CONGO Robert Muteba Kidiaba ambaye aliinuka na pointi 88, na kufuatiliwa na mchezaji kutoka Lgeria Baghdad Bouneydjah aliyepata pointi 63
 Wakati utamu huo ukimjia Samatta na taifa lake Tanzania, Majonzi yamehamia kwa wachezaji wakongwe akiwemo Yaya Toure kutoka Ivorycost na Ayew Andre wa Ghana ambao wamenyanyasika mbele ya mchezaji kinda wa miaka 26 Aubameyang aliyezoa pointi 143 zikiwa saba zaidi ya alizopata Toure huku Ayew akipata 112
 chanzo vanguard
Jan 6, 2016

MADIWANI MBOZI WAPIGWA DARASA MBOZI

Madiwani wapya wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi kwa mfululizo wa siku mbili wamehudhulia mafunzo ya kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao.
 Miongoni wa taasisi zilizoshiriki kuwajengea uwezo ni pamoja na Ofisi ya kanda ya maadili ya utumishi wa Umma, Ofisi ya katibu tawala mkoa na wakuu wa idara za halmashauri ya wilaya.Eneo pekee lililozua maswali mengi ni suala la maadili ya utumishi wa umma, mahusiano baina ya serikali kuu na serikali za mitaa ambapo masuala ya mwingiliano wa kiutendaji na masuala ya ufuatiliaji maadili ya watumishi yalijadiliwa kwa upana.