Adverts

May 29, 2018

DAWA YA KINGA YA VVU KULENGA MAKUNDI MAALUM

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo Mfuko wa Henry Jackson kutoka serikali ya Marekani wamo kwenye hatua za maandalizi kwaajili ya kutekeleza mpango wa utoaji dawa kinga kwa watu walio katika makundi maalumu ya jamii ambayo yapo kwenye hatari ya kuambukizwa.
Kulingana na taarifa za utekelezaji wa Mpango huo, wanawake wanaouza ngono pamoja na wanaume walio kwenye biashara hiyo watashiriki kwenye mpango huo baada ya hatua za awali ambapo watahamasishwa kujipima wenyewe na ikithibitika wana maambukizi wataunganishwa na huduma za CTC ikiwa ni pamoja na kuingizwa kwenye mpango wa matumizi ya dawa za kupunguza makali ARV's
Ama kwa upande mwingine wale ambao hawatakutwa na maambukizi, wataanza kutumia dawa kinga ambapo kila siku watawajibika kumeza kidonge kimoja kwa kipindi kinachofikia siku 21 mfululizo huku pia wakitumia njia za kinga zingine zinazoelekezwa kitaalamu. Hatua hiyo inalenga kupunguza uwezekano wa mtumiaji wa dawa kinga kuambukizwa na virusi ikiwa ataacha kutumia njia zingine ikiwemo matumizi ya Kondomu katika kipindi cha matazamio ya dawa.
Kutokana na takwimu kuonyesha nchini Tanzania asilimia 25 ya wanawake wanaouza ngono wamo kwenye hatari ya maambukizi na katika utafiti uliofanyika hivi karibuni walibainika kuwa na maambukizi ya VVU, wakati ambapo 26% wanaume wanaofanya ngono ya wanaume kwa wanaume pia walibainika kuwa na maambukizi wakati 36% ya wanaotumia dawa za kulevya pia walikutwa na maambukizi hayo.
Mpango huo utatekelezwa kwenye vituo vya afya vyenye huduma za CTC,kwa kuzingatia idadi ya wateja wanaotumia ARV's, Uwepo wa wataalamu waliopata mafunzo ya utoaji huduma kwa watu wanaoishi na VVU.
Kutokana na utaratibu huo si kila Mtanzania atafikiwa na Dawa Kinga hiyo hivyo imesisitizwa umuhimu wa watanzania kuendelea kutumia njia za kinga zilizoelekezwa na wataalamu ili hatua ya majaribio ya dawa Kinga ya sasa yaweze kupimwa kwenye kundi lengwa la wanaouza ngono kwa baadhi ya maeneo yaliyoingizwa kwenye mpango huo katika Mkoa wa Mbeya na Songwe.