Adverts

Oct 1, 2010

MAJAMBAZI YAJERUHI MWEKEZAJI KAPUNGA RICE FARM

Na Danny Tweve Mbeya.

Watu wasiojulikana wamevamia na kuwajeruhi  kwa risasi Msimamizi wa shughuli za Kilimo katika shamba la Mpunga Kapunga Rajendra Kumar pamoja na dereva wake.

Habari kutoka hospitali ya Misheni ya Chimala zilizopatikana mchana wa leo zinaeleza kuwa Kumar amehamishiwa Muhimbili kwa ndege ya kukodi baada ya hali yake kuwa mbaya kutokana na jeraha la risasi iliyopigwa eneo la Jicho la kulia.

Dereva wake ambaye amejeruhiwa upande wa sikio Frank Tweve amesema wakiwa na gari aina ya Toyota Hilux lenye namba za usajiri T 331 AZN kwenye geti la Site One majira ya saa 12.58 jioni akisaini kitabu kutoka kwa walinzi wa kampuni hiyo kwenye geti hilo,ghafla walivamiwa na watu wanne.

Anasema kuwa kabla ya kuamrishwa ulisikika mlio wa bunduki ambapo ghafla akihisi kutoona mbele na kabla ya kuhamaki alisikia milio mfululizo ya risasi huku bosi wake pamoja na mke wa Dereva ambaye alikuwa kwenye gari walipiga kelele baada ya kujeruhiwa, huku walinzi wakionekana kushangaa tu.

Kutokana na hali hiyo anasema ujasiri ulimjia ghafla na kuamua kurukia kwenye gari na kuliondosha kwa kasi hivyo kuwakosesha nguvu watu hao ambao pia wanaonekana kuhofia hali hiyo na kuamua kutimkia kwenye pori lililo karibu na geti hilo.
Tayari walinzi hao wawili wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi juu ya tukio hilo.