Adverts

Nov 18, 2010

UNGA WA BILION 1 MILION 322 WADAKWA BODA YA TUNDUMA

Na Danny Tweve
Mbozi

Watu wawili raia wa Afrika Kusini walikamatwa jana wakiwa na shehena ya madawa ya kulevya yenye thamani ya dola za Kimerekani 822,000 sawa na pesa za madafu za kibongo Bilion 1 Milion 322  wakiwa kwenye mchakato wa kuzivusha kutoka bongo kuelekea Bondeni kwa Mandela.


Akielezea tukio hilo Meneja wa Mamlaka ya Mapato mkoa wa Mbeya Rogasian Shirima alisema kuwa walipata dokezo toka kwa raia wema kuhusu kuvushwa kwa madawa hayo na ndipo walipoongeza umakini katika ukaguzi mpakani na kufanikiwa kukamata madawa hayo.

Shirima alimtaja dreva wa gari aina ya Nissan Hardy Board pick up lenye namba za usajili CA 508-650 kuwa ni Vuyo Jack (29) akiwa na mwanamke mwenye asili ya Asia Anastacia Cloete (25) kuwa walibeba jumla ya kilo 42.5 za madawa ya kulevya wakitokea Dar es Salaam na kuelekea Cape town nchini Afrika ya Kusini.

Katika zoezi la upimaji mzigo huo ilibainika kuwepo kwa Cocaine paketi 26 zenye uzito wa kilo 28.5, Heroin paketi 3 za uzito wa kilo 3.5 na Morphine paketi 8 za uzito wa kilo 10.75.

Makasha ya dawa  hizo  zilipofunguliwa  zilikuwa na mihuri ya Pakistan na nembo au chata za Ng’e na nyoka aina ya Cobra ambapo polisi wa kitengo maalum hapo mpakani walipima na kuthibitisha dawa hizo . (chemical identification)

 Aidha alama za nyoka na ng’e zimefahamika kuwa ni moja ya vitambulisho vinavyotumiwa na maharamia wa dawa za kulevya kutambulisha dawa aina ya Cocaine na Heroine.

Dereva wa gari hilo Vuyo Jack alipohojiwa juu ya yeye kupakia mzigo huo alidai kuwa yeye aliingia hapa nchini na kwenda Mazimbu Morogoro kwenye kambi ya wakimbizi ambapo alikutana na kundi la watu saba akiwepo mtanzania mwenye asili ya kiasia ambao walimkodi awasafirishie almasi hadi Cape town kwa ahadi ya kumlipa dola za kimarekani 10,000.

“Walidai niwape gari ili wakapakie almasi hizo ambapo walichukua gari hilo wakiniacha Morogoro na kwenda nalo Dar es Salaam ambako walipakia mzigo huo, baada ya wiki moja walinipigia simu kwamba wananiletea gari nianze safari ambapo waliniambia kuwa almasi hizo zimewekwa ndani ya dash bodi” alielezea.

Akielezea zaidi alisema kuwa mhindi ndiye alimwonyesha almasi kipande kimoja na kumwambia kuwa wamepakia nyingi hivyo awe mwangalifu njiani.

Hata hivyo haikuwa rahisi kujua kwa mbinu iliyotumika kwani pakati hizo za madawa ya kulevya yalifichwa kwenye maeneo mbali mbali ya gari ikiwepo kwenye chesesi, mashavu ya gari na maeneo zilimoungiwa taaa za mbele na za nyuma.
Aidha maeneo mengine dawa hizo zilifichwa ndani ya milango, sehemu  inayotenganisha AC na rejeta pamoja na kwenye mabomba ya kupitisha hewa ndani ya gati  ambapo iliwalazimu wakaguzi kuwaita mafundi magari waliobomoa sehemu mbalimbali za gari hilo na kutoa madawa.

Uchunguzi umebaini kuwepo kwa usafirishaji mkubwa wa dawa za kulevya  kutokana na mbinu kubwa ya wafanyabiashara hao ambao maafisa wa TRA siyo rahisi kung’amua.

mwisho
indaba2010