Jan 16, 2011
ASKOFU WA RC ATISHIWA BASTOLA MADHABAHUNI NJOMBE
ASKOFU WA RC ATISHIWA BASTOLA MADHABAHUNI NJOMBE: "
Devotha John wa Mwananchi
MWANAMKE ambaye jina lake halikufahamika,
amevamia madhabahuni na kuchomoa bastola
kisha kutishia kumwua askofu wa Jimbo Kuu la
Njombe, Alfred Maluma aliyekuwa akiendesha ibada
katika Kanisa la Mtakatifu Joseph jimboni humo.
Jaribio hilo la mauaji lililozua tafrani kubwa kanisani
hapo na hata kuvuruga kwa muda mwenendo wa
ibada, lilidhibitiwa na padri mmoja aliyekuwapo
madhabahuni hapo ambaye alimrukia mama huyo
na kuikamata bastola hilo.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza kuwa tukio
hilo la kwanza kutokea katika Kanisa la Mtakatifu
Joseph lililoko Jimbo Kuu la Njombe, lilitokea Alhamisi
iliyopita wakati wa ibada ya kusimika mashemasi.
Kwa mujibu wa habari hizo, mwanamke huyo awali
alikuwa ameketi kwenye mabenchi kama mumini
wa kawaida aliyekuwa akifuatilia ibada hiyo, lakini
ghafla alisimama na kufuata askofu huyo na
kumnyoshea bastola hiyo.
'Wakati wa kipindi cha mageuzo, mwanamke huyo
alienda altareni na kumnyoshea bastola Askofu huyo
akitaka kumuua,' mmoja wa mashuhuda wa tukio
hilo, alilieleza gazeti hili na kuongeza. Baada ya
kutoa bastola hiyo huku askofu akiendelea na
mageuzo, padri aliyefamika kwa jina la Ngiri,
alimrukia kwa haraka na kumpokonya bastola hiyo."
Hata hivyo, habari zaidi zilieleza kuwa baada ya
kuikagua bastola hilo ilikuwa haina risasi, lakini
mwanamke huyo alikutwa na risasi kwenye begi lake
la mkononi.
Mashuhuda wengine walilieleza gazeti hili kuwa
bastola hiyo ilifahamika kuwa ya mmoja wa
mapadre wa parokia za Jimbo la Njombe (jina la
parokia na padre vimehifadhiwa), lakini
haikufahamika mwanamke huyo aliipataje. “Ni
Mungu tu aliyesaidia kwa kuwa huyo mtuhumiwa
alikuwa amedhamiria kuja kuua na akasahau
kuweka risasi hivyo inatakiwa polisi litupe ufafanuzi
zaidi,” alisema shuhuda mwingine wa tukio hilo.
Jumapili iliyopita, baadhi ya mapadre walielezea
tukio hilo kwenye ibada zao na kufafanua kuwa
uchunguzi wa awali umebaini kuwa mwanamke
huyo ana matatizo ya akili.
Katibu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe, Erasmo
Mligo alithibitisha tukio hilo, lakini akaeleza kuwa
hawawezi kuzungumza chochote kwa kuwa suala
hilo sasa liko mikononi mwa polisi. "Suala hilo sasa liko
kwa mkuu wa upelelezi Wilaya ya Njombe hivyo sisi
kama kanisa hatuwezi kuzungumza chochote zaidi ya
kuthibitisha kuwa tukio limekuwapo," alisema Mligo.
Kamanda wa Polisi wa Iringa, Everist Mangara
aliliambia Mwananchi jana kuwa ana taarifa ya tukio
hilo, lakini bado anafuatilia taarifa zake. "Tukio hilo
nimelisikia, lakini sijalipata vizuri ila ninaendelea
kulifuatia kwa karibu," alisema Mangara "
new post