Adverts

Jan 25, 2011

Fasta fasta...!

Fasta fasta...!: "
Utoto una mambo yake, nakumbuka siku moja tukiwa shuleni, shule hizi za kulala bweni, tulimkuta kuku porini, rafiki yangu anayetokea huko kusini mwa Tanzania, akaniambia tumkamate yule kuku tumchinje, tupate kitoweo. Akilini mwangu nikawaza , na kukumbuka hadithi za babu kuwa ukila kuku wa watu mwenyewe akikuloga kuku atakuwa akilia tumboni, siku zote…nikaogopa. ‘Wewe kaa upande ule, tumkamate tupate kitoweo haraka, usizubae(siku hizi inaitwa fasta fasta)! Nilikawa najifanya kumkamata huku nategea akimbie, na kweli alikimbia, na hatukufanikiwa kumkamata. Ikawa heri yetu, inagwaje rafiki yangu alinilaumu sana. Ndio kawaida yetu, ukipata wewe ni mshindi ukikosa …lawama! Leo wakati nahangaika na usafiri gari la daladala likatukosakosa pale kituoni tuliposimama, limetoka barabarani linapitia eneo wanaposubiri abiria, kukwepa foleni, na ili wafike huko mjini haraka iwezekanavyo…(fasta fasta)! Tuliokuwepo pale tukamzomoa yule dereva, wakati waliopo ndani ya basi wanamshanglilia anavyokatisha barabara, kwasababu wanawahishwa huko wanapokwenda fasta-fasta. Nikawaza hii haraharaka ina mawili kupata au kukosa, heri ukipata utajipongeza na kuuona huo utaratibu ndio unaofaa, na utaupigia mstari mkubwa, hata kuutafutia mahala pa kujilinda kwenye katiba, lakini ukikosa kuna mawili, kuishia pabaya au kupata ajali. Heri uishie pabaya tutajua kuwa sheria imafuata mkondo wake, lakini ukipata ajali kuna mawili, watu kupoteza maisha yao, au kuharibikiwa na gari na itakuwa mwisho wa ajira… Wakati nawaza haya nikakumbuka mdahalo wa katiba kule chuo kikuu, wakati tunautizama, mama nanihii akaniuliza mbona yule mtu anaongea kwa kujiamini kiasi kile, haogopi kukamatwa, mpaka anasema …kamuajiri shemeji yake… Sikuweza kumpa jibu la haraharaka kwasababu nilikuwa bado nasikiliza maelezo yaliyokuwa yakitolewa. Lakini akilini kwangu nikawaza kuwa wengi bado wana ile kasumba `yakuogopa kukamatwa’ hata pale tunapotaka kusema `ukweli’. Lakini ukweli halisi unaotokea barabarani, au mitaani, au enzi za shule za kukamata kuku wa watu wanafanya kivitendo, mbona hatuugopi! Ndio hayo maisha ya kutaka vya harakaharaka(fasta fasta)! Wakati mjadala unaendelea kwenye runinga, mzee mmoja aliyekuwepo nasi akasema, `hivi hawo wanaosikiliza ni wanafunzi au ni vijana wa mitaani’ nikageuka kumwangalia yule mzee kujua ana maana gani. Aklasema, mbona sioni tofauti yao na vijana wengine. Anasimama mtu wanazomea, anasimama mtu wanashangilia, hata kabla hatujasikia hoja ya huyo mtu, haya nayaona kwenye mikutano ya watu wa kawaida, sikutegemea kuyaona mahali kama pale. Je huyu wanayemzomea akizungumza mambo ya maana watasemaje, au akiamua kukaa kimya, na alikuwa na hoja nzuri sana, hawaoni kuwa wamekosa la muhimu…na huyo wanayemshangilia akitoa hoja inayokwenda kinyuma na hicho wanachomshangilia nacho watasemaje?...’ akaniangalia mimi niseme kitu, lakini nikageuka kusikiliza watoa hoja. Mjadala wa katiba umeanza, na nashukuru sana walioweza kuuanzisha vyema ni hawo waliouandaa hapo chuoni na hata ukaweza kurushwa hewani, na nashukuru kuwa waliwachagua watu wanaokubalika na jamoo kuwa wanazungumza ukweli, … ingawaje mijadala kama hii ilishaanza, ila kwa vile walioanzisha hiyo huenda walikuwa hawakidhi haja ya `warushaji ‘na kama tujuavyo, mpenda roho hula nyama mbichi, ..sio kila watakaozungumza wataonekana wema, hata kama wakizungumzacho kina wema ndani yake, lazima wapewe kipaumbele wale `wanaotoa hoja zenye kukubalika ama na jamii au na maslahi yetu’ Hilo tuliachie hapa kwanza. Lakini mimi, kilichonifanya niandika hapa hii leo ni ile hali aliyozungumza mzee wetu hapa, kuwa kama `wasomi’ tuonyeshe mfano, kwakweli mumeonyesha mfano wa mjadala wa wazi na uwazi. Lakinii kuna mambo ambayo tunatakiwa sote tukubali, kuwa kwenye mjadala, tushangilie hoja, au tubeze hoja, tusimzomee mzungumzaji hata kabla hajazungumza, au kumshangilia mzungumzaji kabla hajazungumza hoja yake. Tunajuaje kuwa atakachozungumza kina kidhi haja, tunajuaje kuwa atakachozungumza mtu Fulani tusiyemtaka hakitakuwa na mslahi kwetu. Kumbuka kinachojadiliwa ni katiba, ni katiba ya wote, unaowakubali na usiowakubali, je usiowakubali hutaki wazungumze? Katiba ni muhimu sana, na kipindi cha mjadala, ni mahala pa kuangalia kila jambo, hata lile unaloliona halina maana kwako, inabidi liachwe lizungumzwe kwanza, kwani kutokana na hilo jambo, huenda tukaweza kupata `umaana wake’ na uwekweje katika ubora , na ili ubora huo auone mzungumzaji na arizike, yeye mtoa hoja na wengine kama yeye’ . Sizani kama unaweza kushangilia kufaulu mtihani kabla hujaufanya, …kwani umeutunga wewe? Basi kama ilivyo darasani au kwenye vyumba vya maabadara ni vyema tukasubiri matokeo kwanza kabla ya kupitisha `hitimisho’ Tukifanya fasta fasta kwa kitu kama katiba, ….oh, baada ya miaka mitano, tutahitaji mdahali kama huu…kama hali itakuwa shwari! Najua wasomi wanajua hili, lakini kwa tahadhari ni vyema tukakumbushana kuwa sisi ni kiyoo cha jamii. Tabia ya kuzomea, au kushangilia kabla ya hoja, kwangu mimii naona tunatekwa na makundi ya watu. Sisi tunatakiwa tuwe na msimamo wa pamoja wa kisomo bila kujali, mtu, rangu, imani au chama, ili kitakachoandikwa baadaye kisiwe tu kitawasaidia hawo `kikundi’ cha jamii pekee, lakini kiwasaidie wao na wengine pia, si leo tu hata kesho, na hapa tutakuwa tumetimiza wajibu wetu wa kuitwa `wasomi’ Tusitekwe na msemo wa harakaharaka(fasta-fasta) tukapata ya leo tu, au kukosa kabisa, na baadaye jamii zijazo zikaja kutubeza. Ni mimi: emu-three
http://miram3.blogspot.com/feeds/posts/default?alt=rss

"