Adverts

Jan 17, 2011

HATIMAYE WALIMU WA CHINDI WAREJEA KAZINI LEO ASUBUHI

Na Danny Tweve
Timu ya walimu 8 walioendeleza mgomo wa kurejea kituo chao cha kazi kutokana na mambo ya ushirikina sasa wamerejea.
Akithibitisha kurejea kwao mwalimu mkuu wa shule hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Luvanda amesema, kimsingi wamekubaliana na jitihada za serikali na wazee wa mila hivyo wanaamini sasa mazingira ni salama.
Amesema timu hiyo kwa pamoja imeondoka asubuhi hii kwenda Chindi kuendelea na kazi kama kawaida na kwamba wanatarajia ushirikiano mkubwa kutoka kwa wanakijiji.
Wakati hilo likifanyika upande wa serikali tayari ulianza kujipanga kuwafukuza kazi kwa kushindwa kwao kurejea vituoni na tayari mipango ya kuwaandaa walimu wengine kwenda kuchukua nafasi ilikuwa mbioni.
Chanzo changu kutoka kwenye mfumo kianaeleza kuwa ilikuwa inasubuliwa wiki hii wangedeka tu, mambo yangewaharibikia kwakuwa tayari uhamisho wa walimu wengine ulikuwa unaandaliwa kwenda kuchukua nafasi zao na wao kukabidhiwa barua za kufukuzwa kazi.
Chindi itaendelea kukumbukwa kwa matukio ya ushirikina yaliyotikisa kiasi cha Mkuu wa wilaya pia kuelekea kuamini kama upo kutokana na mambo yaliyokuwa yakitokea kwenye mazingira hayo yakiwemo walimu kuvibrate(mtetemo) kama simu!.
Teknolojia hiyo ni ya asili wilayani Mbozi kwani pamoja na Chindi yapo maeneo mengine yaliyoripotiwa kutokea kwa matukio kama hayo yakiwemo Msia, Machindo, Isanga, Chikanamlilo, Ikonya na Ikana.
Kwa upande wa idara ya elimu pia imeainisha eneo la ushirikina kama changamoto zinazoikabili sekta hiyo wilayani Mbozi kutokana na mazingira ya kusomea na kufundishia kutishiwa na imani hizo za karne ya 15 hadi 18 kwa mujibu wa maandishi.
Katika jitihada zingine zinazofanyika kuvutia walimu wilayani Mbozi, idara ya elimu imeviomba vyuo vinavyotoa mafunzo ya ualimu kuwaleta wanafunzi wao wakati wa mafunzo ya vitendo kuja kufundisha mbozi ambapo tayari chuo cha Ualimu cha St Agrey cha Mbeya kimekubali kuleta walimu 500 wa mazoezi kuja kupiga kambi wilayani Mbozi.
Hongera bwana Mboka kwa kukubali ombi la wanambozi, kwani mchango wako kwenye ufaulu wa mwaka ujao tutautambua na unastahili kuigwa.