Adverts

Jan 26, 2011

Hatukuhitaji wikileaks kutueleza tunayoyajua...

Hatukuhitaji wikileaks kutueleza tunayoyajua...: "Imeandikwa na Charles Kayoka NADHANI mtakubaliana na mimi kuwa hatukuhitaji tovuti ya Wikileaks kutuambia kuwa uongozi nchini Tanzania unawalinda mafisadi waliopo sasa hivi madarakani na waliokuwepo madarakani. Historia ya kulindani inaanza tangu wakati wa Mwalimu Nyerere aliekuwa akiwahamisha mafisadi kutoka idara moja kwenda idara ingine, na alipoulizwa alijitetea kuwa wataalamu ni wachache mkianza kufukuzana utajikuta kuwa huna watu. Lakini ile haikuwa sababu: Katika mfumo wa utawala wa ki-Machiavelli ni rahisi sana kutawala ukisaidiwa na watu uliowagundua kuwa ni mafisadi na ukawaacha bila kuwashitaki kwani watu hao wanajua wana makosa na kuwa wanaendelea kuwa madarakani kwa huruma yako. Na hivyo kama mtawala unakuwa huru kuiendesha nchi utakavyo! Hawa uliowahurumia kwa dhambi wanakosa msingi wa maadili wa kukukemea! Mfumo wa kifisadi hupenda sana walafi, wageni wahamiaji, na marafiki, kutaka kuitawala nchi milele. Hivi tunataka kuambiwa ni wikileaks kuwa wengi wa maafisa wa chama na serikali wanashirikiana na wawekezaji na hivyo kuifanya nchi ishindwe kukusanya kodi? Nani hakumbuki kuwa wakati wa uchaguzi wale waliokuwa na kesi mahakamani kuhusu ufisadi waliinuliwa mikono na kutajwa kuwa ni mashujaa, wapigiwe kura, na wakapigiwa kura wakitetewa na serikali; nani hajui jinsi watu wakubwa walivyojichukulia viwanja mijini na mashambani ingawa hawaviendelezi na hakuna anayewapinga; nani asiyejua kuwa mashirika yanaugua na mengine yanakufa kwa ubadhirifu kukiwa na raraka za kutoka kwa wakubwa; tunahitaji kukumbushwa kuwa watoto wa wakubwa waliajiriwa BoT kwa vyeti feki na wakuu walikuwa wakiju; kuwa watu wanaingia kwenye vikao vya NEC na CC, na kwenye Baraza la Mawaziri, wakijadili maadili, uongozi bora na tija, wakitoka tu wanakwenda kuwaambia wawakezaji wa ndani na nje namna ya kutoroka kodi; wikileaks imetusaidia kubitisha udhaifu uliopoa na kumsafisha Dk Hosea, kuwa ana nia njema, ila waliomteua hawana nia kutokomeza ufisadi. Sioni sababu ya kumsakama Hosea, kwa sababu ametuthibitishia kile wote tunachokijua, ambacho hatukukijua ni msimamo wake binafsi kuhusu ufisadi, tulidhani anawalinda mafisadi, tena kwa makusudi, kumbe sio kweli. Nadhani tumhurumie yeye na watendaji wenzake kuwa pingamizi kubwa dhidi ya juhudi zao sio mafiasadi, bali walewale waliounda Takukuru. Viongozi wa nchi walichukulie hili kama fursa ya kuthibitisha udhati wa nia kuondoa ufisadi; wakumbuke masikini, tuliowapigia kura rais na chama chake, wanadunishwa na kuteswa na mafisadi. Dk Hosea alindwe, tena zaidi sasa, sio kwa kumpatia ulinzi wa askari kanzu, bali kwa kuwa na uongozi thabiti unaotambulika kwa mafisadi kuwa una nia ya kweli ya kuwatokomeza. Watakapoona kuwa polisi, idara za usalama, viongozi, na Takukuru, wanazungumza na kutenda kwa lugha moja- hawataki ufisadi. Lakini ni kuwajengea dharau Dk Hosea na Takukuru kama mafisadi wanajua kuwa ni visu butu, mbwa wasiong’ata, wanoko wasio na tija ndipo tunawafanya wawe ni kituko! Na ni matumizi mabaya ya fedha za umma na wafadhili (tunazozilipa kama deni), kuunda Takukuruhalafu ndani ya walewale waliowatuma wanahakikisha haifanyi kazi.
"