*******
Yule nesi aliingia chumba maalumu wanapopumzika madakitari, hasa wanapokuwa wamemaliza kazi ya upasuaji, na hukaa hapo kwa muda wakibadili mavazi na kutafakari kazi waliyoifanya. Aliingia kwa wasiwasi, huku anatetemeka kwa woga, uso umetahayari, alikuwa hajui asemeje. Mkononi alikuwa bado na ile chupa ya maji ya kumwekea mgonjwa, ambayo alishindwa hata kuiacha kule kwenye chumba maalumu cha wagonjwa, na akawa kaishikilia mkononi. Nia ilikuwa kubadilisha na kuiondoa ile ambayo ilishaanza kumalizika, lakini…
Alipoingia chumba cha upasuaji, akakuta madakitari hawapo, akajua moja kwa moja wapo kwenye chumba cha mapumziko, ambacho kipo pembeni tu ya hicho chumba cha upasuaji. Akaushikilia ule mlango kuusukuma, akasita, …akajiulize nigonge kwanza, akasema, hapana, ngoja niingie moa kwa moja,…na wakati anawaza hili , akawa keshausukuma mlango na kupiga hatua moa ndani . Kilichomshitua zaidi ni kuwakuta madakitari wote wakimkodolea macho, pale alipoingia ghafla hata kupiga hodi, na hii iliashiria kuwa kuna tatizo...
Madakitari wote wakawa kimya kusikiliza nini atasema, na yeye akawa kashikwa na butwaa, na anashindwa aanze vipi. Mwanzoni akilini alikuwa kawaza vinginevyo, na alijua akifika hapo atapata ahueni kwa kumbiwa jambo la matumaini kuhusina na mgonjwa wao…, lakini hali aliyoikuta mle ndani ilionyesha taswira tofauti ya kukatisha tamaa, akajikuta mwili unanyong’onyea, karibu aidondoshe tena ile chupa ya maji iliyokuwepo mkononi mwake, lakini kwa bahati nzuri alikuwepo dakitari kijana, karibu kidogo na aliposimama, na dakitari huyu alishaanza kusogea, akiataka kusikia taarifa na hapohapo kukimbilia kwenye hicho chumba maalumu cha wagonjwa. Aliona yale mabadiliko ya yule nesi , akamsogelea haraka na akaidaka ile chupa ya maji, ambayo ilionyesha dhahiri, itamponyoka yule nesi mkononi….
Yule nesi alikumbuka kabisa hakuchukua muda mrefu, alivyotoka mle na kumuacha mgonjwa akiwa bado hajazindukana, …hakumbuki ilikuwa saa ngapi, lakini kwa makadirio ya haraka hakuchukua muda mrefu, hadi chumba cha madawa. Alikumbuka ilivyokuwa, kuwa alipofika chumba cha madawa bahati mbaya alimkuta mwenzake, ambaye ni rafiki yake mkubwa, akiwa na wagonjwa wengi waliohitaji huduma ya kupewa dawa, wakiwa na vyeti vyao kutoka kwa madakitari. Kwa hali ilivyo, aliona kama ataamua kuwasubiri hawo wagonjwa wahudumiwe kwanza, atachelewa, kwahiyo alitumia kinga ya unesi na kuingia moja kwa moja hadi ndani wanapohifadhia madawa, lakini baada ya kuomba ruhusa kwa mwenzake, ili asije kuonekana kuwa anamwingilia mwenzake kazi yake.
‘Naomba chupa ya maji, ile ya mwanzo tuliyomuwekea mgonjwa yule aliyemaliza kupasuliwa, inakwisha muda si mrefu, na mgonjwa mwenyewe haonyeshi hata dalili ya kuzindukana, sijui hawa madakitari watachukua hatua gani…’ akamwongelesha mwenzake ambaye alikuwa kabanwa sana na wagonjwa wanaohitaji dawa.
‘Wewe nawe kwani mgeni hapa pita chukua pale usisahau kuandika kwenye daftari, tafadhali…maana unajua utaratibu…mmmh, umesema nini, kuhusu huyo mgonjwa, aah, hayo wanajua hawo wataalamu, waachie wao,… lakini yule mgonjwa anatisha, ule uso ulifanya nini?’ akauliza huku anachukua dawa kabatini.
‘We acha tu, dunia hii ina vituko, hasa eneo hili, kwakweli limevunja rekodi, asilimia ya wagonjwa hapa ni wa vidonda, hasa vya kupigana na kukatana na mapanga au visu…lakini nashangaa, kwanini maugomvi haya yawahusishe na akina mama pia, kwani naona kesi nyingi zimekuwa zikiwahusu akina mama, waliopigwa na waume zao, mbona wanawake wanapata shida sana maeneo haya, kila siku tunatibu watu waliojeruhiwa na wengi ni wanawake, na….bwana wee, ngoja niondoke, maana wasije wakarudi wakanikuta sipo na mgonjwa. Siunamjua tena yule dakitari kijana, kamkomalia yule mgonjwa utafikiri ndugu yake. Anasema lazima atapona…’ akasema huku anaandika kwenye daftari kuonyesha kuwa kachukua dawa gani.
‘Kweli hiyoo ndiyo azima yetu, kama madakitari,…kuwa mgonjwa atapona, kwa vyovyote iwavyo, vinginevyo, sio tegemeo letu, au vipi,… azima ya dakitari yoyote ni mgonjwa kupona. Nampenda sana yule dakitari kijana, vipi uliwahi kuongea naye kuhusu lile swala langu…’ akasema na kuacha kugawa dawa, kuonyesha kuwa hlo swala alilomuelekeza au kumtuma mwenzake lilikuwa la muhimu sana!
Nesi huyu aliyekuwa akihudumia wagonjwa wa dawa, alikuwa kajaribu sana kuwa karibu na dakitari kijana, lakini ilikuwa vigumu, kwani kukutana kwenyewe ni hospitalini, na kazi zao haziwapi nafasi ya kuongea, na kila anapokutana naye, anajikuta akibabaika, asijue la kumwambia zaidi ya kumsalimia tu. Dakitari kijana alijua hili, akawa na hamu ya kusikia nini msichana yule anakihitaji kwake.
Kwa upande wake, alikuwa hana mawazo ya mapenzi na huyo nesi…ila alisema moyoni mwake kama ni lazima kuwa na mpenzi pale hospitalini, angelimchagua rafiki yake, ambaye mara nyingi wanakuwa wote katika shughuli za upasuaji. Lakini hakuwa na mawazo hayo kwa sasa, kwani kazi yake ilikuwa muhimu kuliko kitu chochote kwa muda ule.
‘Kila jambo lina muda wake, kwasasa sitaki kujihusisha na mambo hayo mpaka lengo langu litimie..’ akajisema moyoni.
‘Wewe ukoje, utamuanzaje mwanaume hivihivi…nilishakuambia, mimi mwenyewe namezea mate, na kiukweli nampenda, pengine zaidi yako, sasa nikutafutie dawa wewe kwanza wakati na mimi ni mgonjwa…hahaha…we zubaa tu, utashangaa chombo kinaeleea baharini. …’ Akasema huku anatoka kwenye chumba cha madawa.
Alipofika chumba cha upasuaji ambapo wapo madaktari wanafanya kazi yao, akajaribu kuchungulia kwenye dirisha dogo, nia ilikuwa amwangalie dakiari kijana sura yake.
Tangu dakitari kijana afike hapo amekuwa akimsumbua moyo wake, sura yake, tabia na …yamekuwa yakimsumbua na kuwaza atafanyaje ampate yeye. Rafiki yake anaonekana kumtaka yeye zaidi, na inaonyesha ili afanikiwe inabidi ashindane na rafiki yake, kitu ambacho alikuwa hakitaki, lakini afanyeje, kwani Umri wake unahitaji mchumba, unahitaji mume, lakini hajatokea anayemfaa. Kwa mtizamo wake alikuwa akimtaka mtu kama dakitari kijana, lakini watu kama hawo wamekuwa adimu, kila amuonaye anamchumba wake tayari, sasa yeye lini atampata mchumba kama dakitari kijana.
Alimkumbuka jamaa aliyemuhadaa kuwa atamuoa, sasa miaka mitatu, anamsubiria, hana dalili ya kuoa, au kuchumbiwa, na hata hivyo hana hadhi kama ya dakitari kijana. Alishagundua kuwa huenda jamaa huyo anamuhadaa tu, kwahiyo lazima achangamkie mtu kama dakiatari kijana. Alichungulia kwenye kidirisha kidogo, lakini ilikuwa sio rahisi kuona ndani vyema, na wakati anakodoa macho kuangalia ndani, akasikia mtu akimkaribia, na mkono ukawa umemshika kiunoni, alishituka karibu adondoshe ile chupa ya maji aliyoshika.
‘Wewe unafanya nini hapa saizi, wewe siumepewa jukumu la kumwangalia yule mama mgonjwa, unachungulia nini tena huko…’ alikuwa `matroni’ ambaye ni mkali kama pilipili, hamkopeshi mtu kwenye kazi yake. Na akianza kuongea utafikiri ni mkanda wa video umewashwa.
‘Ndio nimetoka kuchukua chupa ya maji, ile ya mwanzo inakwishia…’ akasema huku akiwa na wasiwasi, . Cha ajabu yule `matroni, akawa anamchezea nywele zake kichwani, na mara akawa anashusha mkono mabegani, akawa anambinyabinya mabegani, akaendelea kushusha mkono mgongoni, hili likamshangaza yule nesi, akakumbuka alichoambiwa kuwa huyu matroni anatabia ambayo wengi wanamtilia mashaka, ile tabia ya kushikashika wasichana na kuwatomasa
`Ni mama mtu mzima, lakini anatabia ya ajabu kweli…’alisikia siku moja nesi mmoja akiongea na nesi mwenzake. Lakini kwa bahati mbaya hakuwahi kusikia hiyo tabia mbaya ni kitu gani! ` au ndiyo hii anayonifanyia mimi leo…’ maana hii mikono yake inanichezea mwili wangu , kama wanavyopenda kufanya wanaume, …hata ngoja nisimpe nafasi hiyo..’ akajisogeza mbali na yule mama, huku akijifanya kumuuliza swali!
‘ Vipi matroni, umependa nywele zangu nini, ehe, watu wania kuwa ni nzuri na ndefu… wanazisifia kuwa zinakuwa haraka…’ akasema huku anajishebedua.
‘Kweli una nwele nzuri, na hata maumbile yako mazuri…mmh, hivi mchumba wako ni nani…maana we acha tu…hebu nenda kamwekee huyo mgonjwa hayo maji…’ akasema yule mama, huku akimwangalia yule nesi kwa mtizamo wa aina yake, akamtizama, hadi alipoingia ndani ya wodi ya wagonjwa maalumu. Wakati anamtizama yule msichana akiondoka, moyoni alikuwa akiisema,..` huyu msichana ni miongoni mwa wasichana warembo humu hospitalini, lakini sijapata muda wa kuwa karibu naye, ipo siku…hapa kuna dili nzuri sana, …laki tano za chapuchapu siwezi kuzikosa kwa wanaume wakware…, hasa bosi wangu, ngoja ipo siku!
Yule nesi akakimbilia kule kwenye chumba cha wagonjwa maalumu, huku akiwaza kuhusu huyu mwanamama(matroni) akasema moyoni, `lakini mimi sioni ubaya wake, labda watu wanamuhisi vibaya tu kwa vile anapenda kuwakagua, na kuwashikashika, lakini hiyo si ndiyo kazi yake…atajuaje usafi wako, umevaa nini…na…lakini mmmh, inatia shaka kidogo, mbona anapapasa kiaina-aina..mmh..’ Alikuwa keshaanza kuiweka vizuri ile chupa ya maji mkononi kabla hajaingia ndani kabisa kwenye kile chumba cha wagonjwa maalumu, huku akiendelea kuwaza…`Aaah, ngoja nikaiondoe ile chupa ya majii hata kama haijaisha kabisa, maana naweza kujisahau ikakutwa imekwisha. Na yule dakitari bingwa namuogopa kama nini, anaweza kukumeza mzimamzima, hana utani kwenye kazi yake…na..na anaweza akasababisha ukafukuzwa kazi hivihivi, hivi nikifukuzwa kazi nitakuwa mgeni wa nani…oh..vipi tena..’
Alijikuta anashikwa na kigugumizi pale alipofungua mlango na mcho yake yakiwa yametua kitanda alichokuwa amelala yule mgonjwa. Macho yalimtoka pima, na kushindwa kusema, hata ile chupa aliyoshika mkononi ikamponyoka na kudondoka chini, lakini kwa bahati nzuri ilitua kwenye sehemu laini na haikupasuka. Alijikuta akitetemeka kwa woga, na kutamani akimbie, lakini angekimbilia wapi,…akatamani apige yowe, lakini ingesaidia nini…akashikwa na bumbuazi kwa dakika moja, huku akishindwa afanyeje…
Je ni nini kimetokea humo wodini
Ni mimi: emu-three
http://miram3.blogspot.com/feeds/posts/default?alt=rss
"