Rais wa Jamhuri wa Muunganowa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali yake itaendelea kulinda ardhi ya wakulima wadogo wadogo wakati wa utekelezaji wa mradi mkubwa, pengine kuliko yote ya kilimo iliyopata kubuniwa nchini katika eneo la Kusini mwa Tanzania wa South Agricultural Corridor Growth of Tanzania (SACGOT).
“Kamwe hatutachukua ardhi kutoka kwa wakulima wadogo wadogo ili kuwapa wakulima wakubwa. Wakati wote tutatetea haki ya wakulima hao kuendelea kumiliki ardhi yao wakati tukiwasaidia kuwa sehemu ya mradi huo wa SACGOT,” Rais Kikwete amemwambia Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, Mama Ngozi Okonjo-Iweala.
Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Mama Okonjo-Iweala, jana, Alhamisi, Januari 27, 2011, kwenye Hoteli ya Sheraton, mjini Davos, ambako Rais Kikwete amefikia. Rais Kikwete amewasili mjini Davos mchana wa jana akitokea mjini Geneva, tayari kuhudhuria Mkutano wa Uchumi Duniani wa World Economic Forum (WEF) unaoendelea mjini humo.
Rais Kikwete alikuwa mjini Geneva kuongoza mkutano wa kwanza cha Tume ya Kimataifa Kuhusu Afya ya Akinamama na Watoto ambayo ni mwenyekiti mwenza wake. Mkutano huo ulifanyika juzi kwenye makao makuu ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ambako Rais Kikwete aliuongoza kwa kushirikiana na mwenyekiti mwenza wake, Waziri Mkuu wa Canada, Mheshimiwa Stephen Harper. Tume hiyo ya Umoja wa Mataifa (UN) imeteuliwa na WHO.
Rais Kikwete amesema kuwa katika utekelezaji wa mradi huo Serikali itahakikisha kuna uwiano kati wa ushiriki katika wakulima wadogo na wakulima wakubwa, wote wakishirikishwa katika kilimo cha biashara. “Wakulima wakubwa hawatawekeza katika mradi huu kama mbadala wa wakulima wadogo bali kwa ushirikiano wa makundi yote mawili.”
Rais Kikwete amekutana na Mama Ikonjo-Iweala ili kumwelezea kuhusu mradi huo na kuiomba Benki ya Dunia kuunga mkono mradi wa SACGOT ambao uzinduzi wake kimataifa unatarajiwa kufanyika leo kwenye mkutano wa WEF na ambako Rais Kikwete atakuwa mshiriki muhimu. Uzinduzi wa mradi huo kwa nyumbani ulifanyika hivi karibuni.
Mpango wa SACGOT ambao umebuniwa na Tanzania yenyewe, utashirikisha wadau wote wa kilimo ikiwa ni pamoja na wakulima, sekta binafsi, Serikali, taasisi muhimu na kubwa za fedha duniani na sekta ya umma. Mradi huo ulibuniwa wakati wa Mkutano wa WEF-Africa uliofanyika Dar es Salaam Mei mwaka jana.
Mapema Mheshimiwa Rais Kikwete amemweleza Mama Okonjo-Iweala sababu za Tanzania kuamua kutekeleza mradi mkubwa zaidi kuliko wowote ulipata kutekelezwa katika historia ya Tanzania. “Nimeamua nikueleze kuhusu mpango huu mkubwa sana wa kilimo. Kama unavyojua, wetu ni umasikini ambao msingi wake ni kilimo duni. Ukifungua nafasi na fursa katika kilimo, maisha ya wananchi wetu yatabadilika sana na haraka,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kwetu sisi kilimo ni karibu kila kitu. Ni sekta ambayo inabeba maisha ya asilimia 80 ya wananchi wetu, ni sekta inayotoa ajira kwa watu wengi kuliko sekta nyingine yoyote, ni sekta inayochangia asilimia 26.5 ya pato la taifa, ni sekta inayochangia asilimia 30 ya mapato yetu ya fedha za kigeni lakini bado sekta hiyo inakua kwa kasi ndogo ya asilimia 4.8, ambayo ni ndogo sana kulinganisha na sekta nyingine.”
Mama Okonjo-Iweala amemhakikishia Rais Kikwete kuwa Benki ya Dunia imefurahishwa na ubunifu wa mradi huo na kuwa iko tayari kuunga mkono na kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza mradi huo ambao utatekelezwa katika sehemu za mikoa ya Morogoro, Iringa, Mbeya, Rukwa na Ruvuma.
“Huu ni mradi bora sana kwa sababu ya asilimia 80 ya Watanzania wanaishi mashambani na maisha yao yanategemea kilimo. Hili ni jambo muhimu sana hasa kwa kutilia maanani kuwa mradi huu utaangalia masuala yote kuhusu kilimo na hasa suala la kuunganisha wakulima wadogo na wakubwa,” amesema Mama Okonjo-Iweala.
Mwisho.
Imetolewa na:
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini, Davos.
28 Januari, 2010
"