Adverts

Jan 22, 2011

UVCCM: Dowans Irudi Bungeni

Katbu mkuu waUVCCM Matini Shigella KAMATI ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana limeopendekeza kurudishwa bungeni suala la Kampuni ya kufua umeme wa Dowans/Richmond ili Watanzania wajue nani alisababisha serikali kubeba mzigo wa kutakiwa kulipa sh. bilioni 94 na awajibishwe. Kwa hatua hiyo, UVCCM wamesema endapo Kamati ya Dkt. Harrison Mwakyembe ililidanganya bunge, mbunge huyo ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Ujenzi awajibishwe na kama kuna mtu yeyote alijiuzulu bila hatia, asafishwe. Tamko hilo lilitolewa na Mjumbe wa Kamati hiyo na Mwenyekiti wa UV-CCM Mkoa wa Arusha, Bw. James ole Millya kwa niaba ya kamati hiyo, ilipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari jana kuhusu maamuzi ya kikao chake kilichofanyika juzi. Alisema endapo kosa hilo ni la serikali, basi itamke ni nani mmiliki wa Richmond, aliyehamishia mkataba wake kwa Dowans ambayo inatakiwa kulipwa mabilioni ya fedha za walipa kodi. 'UV-CCM inaitaka serikali kuwataja rasmi wamiliki wa Richmond. Haiingii akilini mmilikishwa (Dowans) ajulikane na alipwe fidia ya sh. bilioni 94, wakati mmilikishaji (Richmond) asijulikane. 'Hao Dowans waliotajwa na serikali ambao ndio walinunua mali za Richmond waisaidie serikali yetu kuwataja wamiliki halali wa Richmond ili wao ndio wawajibike kulipa pesa hizo badala ya serikali,' alisema Bw. Millya. Katika mkutano huo ambao wajumbe wa kamati hiyo walizungumza kwa zamu kila mmoja na mada yake, UV-CCM iliitaka serikali kuwa na msemaji mmoja ambaye atatoa ufafanuzi na maelezo juu ya masuala makubwa yanayogusa maslahi ya taifa, na kulaani hatua ya sasa ambapo mawaziri wamekuwa wakitoa maoni tofauti hadharani. Kwenye suala la hali ya CCM na UV-CCM lililotolewa tamko na Bw. Marwa Mathayo ambaye pia ni mwenyekiti wa jumuiya hiyo mkoani Mara, umoja huo uliwakemea baadhi ya viongozi wa chama chao na serikali kwa kutopendana na kujenga uhasama na chuki, jambo ambalo walisema ni aibu na urithi mbaya kwa vijana. 'Watambue kuwa wao walipokuwa vijana hawakurithishwa chuki na uhasama miongoni mwao. Vitendo hivi haviwezi kuvumiliwa. UV-CCM inawataka sasa wale wote wanaoendekeza uhasama na chuki iliyojengeka katika msingi wa ubinafsi, waache mara moja. Vinginevyo tutawataja kwa majina na kuwataka vijana kote nchini kuandamana na kuwalaani, maana uhasama na chuki zinaleta mipasuko katika jamii na chama kwa ujumla,' alisema. Bw. Mathayo. Akiwasilisha hoja ya mikopo ya elimu ya juu nchini, Bi. Zainab Kawawa alisema kuwa bodi ya mikopo haijafanya kazi yake vizuri na hivyo kupendekeza ipinduliwe ili kunusuru vijana wa Tanzania wanaoteseka kwa kukosa mikopo. 'UV-CCM imebaini kwamba kuna urasimu unaofanywa na watendaji, na haiingii akilini Mkwawa University wagome kwa kutolipwa posho zao na baada ya siku moja walipwe. Jambo hili si utamaduni wa vijana wa Kitanzania na halikubaliki popote duniani. Wale wote wanaohusika, CCM ichukue hatua ili serikali iwawajibishe mara moja ili tabia hii isijirudie. 'UV-CCM haiko tayari na katika historia yake haijawahi kuwa tayari kuwaona vijana wa vyuo wakigoma ndipo matatizo yao yanatatuliwa. Wale wote wanaotaka kuanzisha utamaduni mpya wa utawala wa kwamba mpaka vijana wagome au kundi fulani ligome ndipo ufumbuzi wake upatikane wapishe ofisi za umma, wawajibike mara moja na serikali iwafikishe mahakamani kwa kuisababishia hasara,' alisema Bw. Kawawa ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia vyama vya wafanyakazi. Katika hatua nyingine, mmoja wa wanasheria mahiri nchini, Profesa Abdallah Safari amemuunga mkono Waziri Samuel Sitta, akisema hoja zake ziko dhidi ya malipo ya Dowans ni sahihi kwa kuwa kulipa tozo hiyo ya sh. bilioni 94 ni kukiuka katiba ya nchi. Prof. Safari aliyasema hayo jana Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari, waliotaka kujua maoni yake kama mwanasheria juu ya mjadala huo unaoendelea nchini. 'Msimamo wangu juu ya Dowans mbona uko wazi, nakubaliana na Waziri Sitta moja kwa moja, naunga mkono hoja za mzee yule, yuko sahihi kabisa, nafikiri ninyi hoja zake mnazijua...lakini mbali ya hilo, kuilipa Dowans ni kukiuka katiba ya nchi, katika ibara yake ya tisa. 'Katika ibara hiyo imeelezwa kuwa serikali italinda rasrimali za nchi hii si kuzitapanya...kuwalipa Dowans inakiuka ibara hiyo...hili ni sawa na lile suala la nyumba za serikali ambalo nashangaa vyama vya siasa haviliongelei kabisa...pia mikataba yenyewe ya kimataifa inasema wazi kuhusu kuheshimu mikataba,' alisema Prof. Safari na kuongeza; 'Lakini inasisitiza mikataba inayopaswa kuheshimiwa ni ile iliyo halali tu, si mikataba inayoonekana kuwa na rushwa ya wazi wazi kabisa. Nakumbuka Mwalimu aliwahi kumwambia Kabila mkubwa (Rais Laurent) kuwa asilipe mikataba yote ya feki iliyoingiwa na Mobutu...Mwalimu Nyerere pia aliwahi kupinga mikataba ya kikoloni kama ule wa Nile Basin.' Mara kwa mara Bw. Sitta ambaye alikuwa spika wa bunge la tisa wakati mjadala wa kampuni tata ya Richmond ulipoibuka bungeni, amenukuliwa mara kadhaa akisema kuwa Dowans ni kampuni ya wajanja wachache wanaotaka kujichotea fedha za walipa kodi wananchi maskini wa nchi hii, kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.Chanzo:Gazeti Majira
"