Adverts

Feb 4, 2011

MSD YAISAIDIA SEKONDARI YA TOSAMAGANGA VIFAA VYA MAMILIONI YA SHILINGI

MSD YAISAIDIA SEKONDARI YA TOSAMAGANGA VIFAA VYA MAMILIONI YA SHILINGI: "
BOHARI kuu ya dawa nchini (MSD) imetoa msaada wa vifaa vya kemikali kwa ajili ya maabara na vyenye thamani ya sh mil 6.3 kwa shule ya sekondari Tosamaganga ili kuwawezesha wanafunzi wa kidato cha sita kufanya mtihani kwa vitendo. Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache baada ya wanafunzi wa shule hiyo ya Sekondari ya Tosamaganga, Mkoani Iringa kuwa na hofu ya kutofanya kwa vitendo mitihani yao ya kidato cha sita kutokana na kukosekana kwa vifaa hivyo. Akikabidhi vifaa hivyo kwa uongozi wa shule hiyo, Afisa mauzo wa MSD, Yona Msengi alisema kuwa msaada huo umetolewa ili kuwasaidia wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi, kufanya kwa vitendo mitihani yao ya kidato cha sita, itakayoanza February saba mwaka huu. Alisema kutokana na MSD kuwa mdau wa sekta ya afya ambayo wataalamu wake wanatokana na wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi, haikuwa na budi kushughulia tatizo hilo kwa kutoa vifaa vya maabara na kemikali zenye thamani ya shilingi 6,340,100, kabla ya mtihani huo. “Baada ya kusoma habari ya mwananchi, iliyotoka siku ya jumamosi wiki jana, ikieleza jinsi mlivyo na uhitaji mkubwa wa vifaa vya maabara na kemikali, tuliamua kuitikia wito wenu na kuja kuwasaidia vifaa hivi kabla ya mtihani kwa sababu bila nyie, hatuwezi kuwa na wataalamu hapo Baadae,” alisema Msengi. Akipokea msaada huo, Mkuu wa shule hiyo Julius Shulla alishukuru kwa msaada huo, kwa madai kuwa utaweza kuwasaidia wanafunzi wake kufanya vyema katika mtihani wao wa kidato cha sita. “Nashukuru sana, kwa kweli mmetusaidia kwa kiwango kikubwa kwa sababu tunahitaji msaada wa vifaa hivi ili wanafunzi wetu wafanye kwa vitendo mitihani yao, sio rahisi kwetu kuwezesha darasa lenye wanafunzi zaidi ya 400 kuwa na vifaa hivi muhimu kwa sekta ya sayansi, tumefarijika sana,” alisema. Awali wakati wa mahafali ya kidato cha sita shuleni hapo, Shulla alisema ili wanafunzi hao zaidi ya 400, waweze kufanya vyema mtihani wao, lazima kuwepo na vifaa vya maabara na kemikali ambavyo vitagharimu kiasi hicho cha sh milioni 13, ambapo nusu yake tayari vimetolewa. Alisema kuwa wakati, shule hiyo ikiwa chini ya Serikali kuu, fedha za kifaa vya maabara zilikuwa zikifika mapema na kwamba tangu, iwe chini ya halmshauri ya Wilaya ya Iringa, hali imekuwa mbaya, kutokana na halmashauri hiyo kudai kuwa haina fedha za kununulia vifaa hivyo. Kwa upande wao wanafunzi wa Tosamaganga, walisema kuwa walishukuru kwa kupatiwa vifaa hivyo kwa madai kuwa endapo visingekuwepo, ingekuwa ndoto kwao kufanya kwa vitendo mtihani wao wa wiki ijayo. Hata hivyo wameiomba Serikali na mashirika mengine, kuwasaidia vifaa vilivyobaki, ili wanafunzi wote wanaosoma sayansi waweze kufanya mtihani wao kwa vitendo. Mwisho
"