Adverts

Feb 28, 2011

Sitta Azidi Kuwakuna Wasomi, *Wasema aliongoza bunge kwa maslahi ya taifa

WASOMI wa vyuo vikuu Kanda ya Kaskazini, wameeleza kuridhishwa na utendaji wa aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Bw. Samueli Sitta kutokana na kuendesha mijadala mbalimbali kwa maslahi ya taifa. Wasomi hao kutoka vyuo vikuu vya Mwenge, Tengeru, Mount Meru, KCMC College, Chuo Kikuu cha Stephano Moshi (SMMUCo) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara (MUCCoBS), wameyasema hayo katika mdahalo wa kujadili katiba mpya. Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Bw. Clemence Mbogo kutoka MUCCoBS, alisema katiba ya sasa haioneshi kuwalinda viongozi wanaoweka maslahi ya taifa mbele kama alivyokuwa Bw. Sitta. Alisema Bw. Sitta ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki alipokuwa spika wa bunge aliweka utaifa mbele na siyo maslahi bianfsi au vyama vya siasa kama wanavyofanya baadhi ya viongozi kwa sasa. Katiba yetu ya sasa imekaa kimya, haioneshi namna gani itawatetea viongozi wanaoweka maslahi ya taifa mbele na hii inasababisha wenye mamlaka kuwaondoa nani asiyejua Sitta alifanya kazi kwa maslahi ya taifa� alihoji. Kuhusu madaraka ya rais wasomi hao walisema katiba ya sasa inampa rais madaraka makubwa ya kuteua mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya bila ukomo. Wakizungumzia suala hilo, Bw. Godfrey Banza, Bw. Antony Lyimo na Paul Momba walisema katiba haioneshi idadi kamili ya mawaziri wanaopaswa kuteuliwa jambo ambalo husababisha rais kuteua idadi itakayompendeza yeye bila kujali gharama kwa taifa. Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Moshi, Bw. Japhary Michael aliwabeza baadhi ya watu wanaopinga wanasiasa kuzungumzia katiba kwani siasa ndiyo mhimili pekee ambao kila jambo nchini hupitia kwao. Aidha meya huyo alibeza kauli za baadhi ya viongozi wa CCM wanaotaka Watanzania wasizungumzie katiba kwa madai hawaifahamu kwani mahitaji ya katiba mpya kwa sasa yanatokana na katiba iliyopo kutofahamika na asilimia kubwa ya Watanzania. Akifungua mdahalo huo, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Dkt. Norman Sigalla aliwataka wasomi kuwa makini katika kufafanua katiba inayohitajika kwani mtazamo wa ubovu wa katiba iliyopo sasa huenda ukaonekana hivyo kutokana na uongozi uliopo madarakani. Katiba inaweza kuwa nzuri au mbaya kutokana na uongozi uliopo madarakani lakini pia viongozi wasipokuwa na uhusiano mzuri na wananchi wao huweza kuleta hali ya kutaka mabadiliko,� alisema. Awali waandaaji wa mdahalo huo, Waziri wa Elimu wa Serikali ya Wanafunzi MUCCoBS, Bw. Zawadi Kalist na Naibu wake, Bw. Amani Laizer walisema mdahalo huo umelenga kutoa muongozo sahihi kwa jamii kuhusu mabadiliko ya katiba badala ya kuvutwa na ushabiki wa kisiasa. (Chanzo: Gazeti Majira)
"