CHAMA Cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimeandaa bonanza la vyombo vya habari, ambalo litadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
Leo TASWA na TBL zilifanya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
kuzungumzia bonanza hilo litakalochukua washiriki zaidi ya 1,000.
Meneja Uhusiano na Mawasiliano ya Umma wa TBL, Editha Mushi, alisema maandalizi yanaenda vizuri kuhusiana na bonanza hilo na kwamba litakuwa la aina yake kuanzia michezo vyakula na vinywaji.
“TBL itahakikisha bonanza la mwaka huu linafana na linakuwa la aina yake kuanzia katika michezo, vinywaji na vyakula ili kila mmoja aamini kwamba kweli limedhaminiwa na kampuni ya bia.
“Tunawaomba waandishi wajitokeze kwa wingi huku tukiamini kwamba kila mmoja atafurahi siku hiyo, maana lengo ni kuwakutanisha pamoja watu wa tasnia ya habari na kubadilishana mawazo na pia kupongezana kwa kazi ngumu mnayoifanya,” alisema Mushi.
Aliwawapongeza viongozi wa Taswa kwa kuendelea kushirikiana na TBL na kwamba kampuni yake itaendelea na ushirikiano huo hata katika masual mengine ambayo itayadhamini yakiandaliwa na Taswa.
Lakini Mushi hakutaja tarehe rasmi kwa maelezo kuwa bado wanafanya mawasiliano na kumbi mbalimbali, ingawa pendekezo la awali ni iwe ama Machi 12 au Machi 19 na kwamba kabla ya Ijumaa wiki hii suala hilo litakuwa limepatiwa ufumbuzi.
Alipoulizwa wamedhamini bonanza hilo kwa kiasi gani, Mushi alijibu: “Bajeti ya Taswa wakati wanatuomba udhamini mwaka jana ilikuwa sh. Milioni 37, lakini kadri siku zinavyoenda mambo yameongezeka, sasa hivi ni zaidi ya sh. Milioni 40 na makisio yetu huenda likafika sh. Milioni 50,” alisema.
Alieleza kuwa watakapotangaza tarehe rasmi, ataweka wazi na suala la gharama ingawa itakuwa zaidi y ash. Milioni 40.
Naye Mwenyekiti wa Taswa, Juma Pinto aliishukuru TBL na kusema wanataka bonanza la mwaka huu liwe bora zaidi na kutaja baadhi ya michezo itakayoshindaniwa kuwa ni soka, netiboli, wavu, kuvuta kamba, kufukuza kuku na riadha.
Pia alisema kutakuwa na mashindano ya kucheza muziki na kwamba katika michezo ya kawaida zawadi ni vikombe, lakini katika muziki ni fedha taslimu.
"