Adverts

Feb 20, 2011

Ukata mkali waitafuna serikali- mgawo wa idara, taasisi wapunguzwa

SERIKALI imesema hivi sasa haina fedha za kukidhi mahitaji ya idara na taasisi zake na kuwataka wananchi kuwa makini katika matumizi ili kukabiliana hali ngumu iliyopo. Akizungumza katika mahojiano maalum na MTANZANIA Jumapili ofisini kwake mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki,Ofisa Habari na Mahusiano wa Wizara ya Fedha na Uchumi,Ingiahedi Mduma, alisema pato la serikali hivi linategemea zaidi kodi za wananchi tofauti na miaka ya nyuma. Alisema zamani kiasi kikubwa cha fedha za kujiendesha, kilikuwa kikitoka kwa wafadhili. Licha ya kutokuwa tayari kufafanua kiundani, ofisa huyo alisema matumizi ya fedha katika baadhi ya halmashauri nchini hayafuati taratibu zinazotakiwa. Alisema katika siku za nyuma, halmashauri zimekuwa zikitumia vibaya fedha zinazotengwa kila mwaka,bila kufikia malengo yaliyokusudiwa na serikali. “Hivi sasa serikali ina upungufu mkubwa wa fedha na hata halmashauri zetu zinachangia kuwepo hali hii, kutokana na kutumia fedha kinyume cha malengo yaliyopangwa,”alisema Mduma. “…ni kweli hivi sasa serikali haina fedha kabisa… tunaendelea kujipanga kuona namna gani ya kupambana na hali hii”. Alisema sababu moja ya kukosekana kwa fedha kumechangiwa na matumizi mabaya ya wakuu wa vitengo, ambao wameshindwa kutimiza wajibu wao. “Unajua kila mhusika hasa halmashauri zetu, zinatakiwa kuainisha bajeti yake ya kila awamu… hivyo wanapotumia fedha hizo kinyume cha maombi yake, awamu inayofuata watakatwa ili kufidia awamu iliyopita,”alisema Mduma. Alisema kutokana na hali hiyo, serikali imeanzisha kitengo cha ufuatiliaji wa matumizi ya fedha kwa kila halmashauri zote nchini ili kukabiliana na wimbi hilo. “Serikali imeanzisha kitengo cha ukaguzi kwa halmashauri ili kukabiliana na wimbi hili, kwani tumebaini fedha zinazoombwa kwa miradi mingi hugeuzwa kwenda kufanya miradi ambayo haikutarajiwa,”alisema Mduma. Alisema kutokana na hali hiyo, kila halmashauri imetakiwa kuongeza kasi ya ukusanyaji wa kodi hizo ili kuokoa jahazi. “Ni kweli hakuna fedha si unaona hata hapa ofisini kwangu hakuna hata faili moja… sisi wenyewe hapa kukavu kwa kuwa tunafahamu hali halisi hatuwezi kulalamika wakazane tu kuzikusanya kodi ili tuwagawie haraka kile kinachopatikana,”alisema Mduma.
"