Adverts

Feb 23, 2011

Wabunge Wafungua Kesi Kupinga Dowans

Mbunge wa Kibakwe CCM, George Simbachawene(kulia) ni mmoja kati ya Wabunge waliofungua kesi kupinga malipo ya Dowans KATIKA hali inayodhihirisha Watanzania kukerwa na malipo ya Kampuni ya Dowans, Mahakama Kuu ya Tanzania imepokea na kusajili kesi ya kikatiba kupinga malipo hayo. Kesi hiyo ya kikatiba ilifunguliwa mahakamani hapo jana na Watanzania saba wakiwemo wabunge watatu na kupewa namba tano ya mwaka 2011 chini ya Kampuni ya Mawakili ya Mpoki na Lukwaro. Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, msingi wa kesi hiyo ni kwamba malipo ya Dowans ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 sehemu ya tatu kifungu cha 27 Ibara ya kwanza na ya pili. Katika kesi hiyo Watanzania hao wanaiomba Mahakama Kuu kutengua uamuzi wa malipo hayo kwa kuwa yanakwenda kinyume na katiba ya nchi. 'Sisi kama Watanzania wenye uchungu na nchi yetu, tunahurumia taifa letu na watu wake masikini wanaokosa hata huduma muhimu kutokana na hali ngumu, tumeamua kwenda kuomba haki Mahakama Kuu,' alisema Bw. Senkoro Nzoka mmoja wa Watanzania hao. Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 27 Ibara ya kwanza na ya pili malipo ya Dowans ni uvunjaji mkubwa wa katiba ya nchi kwa kuwa ni matumizi mabaya ya rasilimali za nchi. 'Kifungu cha 27 Ibara ya kwanza na ya pili inataka kila mwananchi kulinda rasilimali za nchi, sisi kama Watanzania tuna wajibu kuhakikisha rasilimali za nchi hazichezewi,' alisema Bw. Senkoro. Kifungu hicho cha Katiba kinasomeka- '27.-(1) Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, Kulinda mali ya umma, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine. (2) Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao,' inasema sehemu hiyo ya Katiba ya nchi ya mwaka 1977. Alisema kifungu hicho ndio msingi wao wa kufikia maamuzi ya kufungua kesi hiyo wakiwawakilisha Watanzania. Hata hivyo Bw. Nzoka alisema hawezi kutoa ufafanuzi wa kina juu ya kesi hiyo kwa kuwa ni suala la kisheria na kuweka wazi kuwa anachoweza kukiri ni kwamba wamejitolea kuwawakilisha wanannchi wasio na uwezo watakaoathirika kukosa huduma muhimu. 'Kama unavyojua hili ni suala la kisheria kwa sasa, siwezi kusema zaidi lakini tambua kuwa wabunge wa CCM walikataa na kuitaka serikali kutafuta njia ya kuepusha malipo hayo, huo ndio mwongozo wetu,' alisema Bw. Nzoka bila kutoa ufafanuzi wa kina. Uchunguzi wa Majira ulibaini wabunge watatu wanaowakilisha wenzao katika kesi hiyo kuwa ni Mbunge wa Kibakwe, Bw. George Simbachawene, Bi. Anjela Kairuki pamoja na Bw. Gosbert Blandes. Naye Bw. Hassan Nassoro ambaye ni kijana msomi Mtanzania aliyekuwa nchini Uingereza alisema atazungumzia kesi hiyo baadaye kwa kuwa ni suala la kisheria huku akithibitisha kuwa yeye ni mmoja kati ya walioifungua. Sakata la malipo kwa Kampuni ya Dowans limekuwa kero kubwa kwa Watanzania tangu ilipoibuka kupitia vyombo vya habari na bungeni. Awali ilidaiwa kuwa malipo hayo yalikuwa ni bilioni 195 lakini baadaye ilibainika kuwa taarifa hizo zilipikwa na watu wenye manufaa na kampuni hiyo kwa lengo la kuwaibia Watanzania. Kwa mujibu wa kile kilichoelezwa kuwa ni uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara ICC) malipo hayo ni sh. bilioni 94. Katika hatua inayoonyesha suala hilo kukumbwa na giza nene juzi mtu aliyedai kuwa mmiliki wa kampuni hiyo alitingwa nchini na kuzungumza na wahariri wa vyombo vya habari kwa masharti ya kutopigwa picha. Sharti hilo limezua utata mzito huku Watanzania wengi wakidai kuwa mtu huyo si mmiliki wa kampuni hiyo na kuwa uenda amenunuliwa na wahusika ili wafikie lengo lao la kuvuna jasho la Watanzania la sh. bilioni 94. Hii ni kesi ya pili kupinga malipo ya Dowans, kesi ya kwanza ilishafunguliwa na asasi za kiraia zipato 50 zikiwakilishwa na Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC). Chanzo:Gazeti Majira)
"