Daniel Mjema, Moshi
Ni siku za mwisho? Hili ndilo swali lililoanza kuumiza vichwa vya watu baada ya kijana mmoja kuibuka wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro na kudai ameoteshwa dawa ya ajabu na Bikira Maria inayotibu magonjwa sugu ukiwamo Ukimwi.Kama ilivyo kwa mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambikile Mwasapile wa Loliondo ambaye amejizolea umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi, kijana huyo naye amekuwa akitoa tiba kwa sh500.
Kwa imani ya waumini wa Kanisa Katoliki Duniani, Bikira Maria ni mama wa Yesu ambaye anaaminiwa na waumini wa Kanisa hilo na hata katika sala jina lake ndilo linalotumika zaidi huku wakiamini kuwa Yesu ni mtoto wa Mungu.Habari za uhakika kutoka eneo la Customs katika mji mdogo wa Tarakea, mpakani mwa Kenya na Tanzania, zilimtaja kijana huyo ambaye sasa anajiita Nabii, kuwa ni Hilary James Kitwai (28), kutoka wilayani Babati.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu kutoka Tarakea, Kitwai alisisitiza kuwa dawa hiyo ameoteshwa na Bikira Maria na Yesu na kwamba inatibu Ukimwi, Saratani, Kisukari, Shinikizo la Damu, Figo, Pumu na maradhi ya maumivu.
"Walinitokea kwenye ndoto wakanionyesha huo mti na waliniambia kwa sasa tuko wawili tu Tanzania, lakini huyo mwenzangu simfahamu. Mimi natoza Sh500 lakini katika hiyo pesa yangu na familia yangu ni Sh300 tu,"alidai.
Kitwai ambaye amekuwa gumzo katika mji wa Tarakea, alisema anakabiliwa na changamoto kubwa katika kuwahudumia wenye mahitaji kwa kuwa hana msaada na kuomba serikali imsaidie kumpatia wahudumu.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka wilayani Rombo, tayari vyombo vya ulinzi na usalama vimemzuia kwa muda, kijana huyo kutoa tiba inayofanana na ya mchungaji Mwasapile na kuitisha sampuli za mizizi anayoitumia.
Kijana huyo ambaye ni fundi baiskeli kwa miaka mingi katika eneo hilo, aliibuka Jumatatu wiki hii na kuanza kutoa tiba kwa kutumia kikombe na tayari watu takribani 100 kutoka Kenya na Tanzania wamekunywa dawa yake.
"Anadai kuwa ameoteshwa na Bikira Maria na alielekezwa huo mti ambao una utomvu na kuanzia juzi (Jumatatu),watu kama 100 hivi walishakunywa dawa hiyo ambayo wenyeji wanadai mti wake ni sumu,"kilidai chanzo chetu.Ofisa Mtendaji wa Kata ya Tarakea, Motamburu, Kimario, alilithibitishia Mwananchi kuwapo kwa kijana huyo.
Kimario alisema yeye binafsi, Ofisa Afya na Ofisa Usalama wa Taifa, walifika nyumbani kwa kijana huyo juzi na kumfanyia mahojiano."Tulimhoji akasema alitokewa na Bikira Maria na Yesu ambao walimwonyesha mti huo ambao upo katika Mto Tarakea na walimwambia yupo mmoja tayari anayetibu maradhi sugu na kwamba yeye atakuwa wa pili,"alisema mtendaji.
Kwa mujibu wa mtendaji huyo, kijana huyo aliwaeleza kuwa baada ya Babu wa Loliondo na Yeye, bado atatokea mtu wa tatu ambaye naye ataoteshwa dawa za kutibu maradhi hayo na baada ya hapo Yesu mwenyewe atakuja duniani.
"Tulimuuliza kama ameshatoa dawa hiyo kwa watu mbalimbali akasema alianza kutoa Jumapili na watu kama 20 hivi walikunywa na alitupa vipande vya miti viwili vya dawa hiyo na tumevikabidhi kwa uongozi wa juu,"alisema Kimario.
Kwa mujibu wa Kimario aliyekuwa akimkariri kijana huyo, alisema 'nabii' huyo ameamua kutoendelea kutoa tiba hiyo hadi hapo serikali itakaporidhia na kwamba kwa sasa anamuomba Mungu ampe maono zaidi juu ya dawa hiyo.
Wananchi walioongea na Mwananchi baada ya kuzagaa kwa taarifa hizo, wameitahadharisha serikali kuwa makini na watu wanaojiita ni manabii vinginevyo wananchi wanaweza kukumbwa na maafa ya kunywa sumu bila kujua.
Wananchi hao wameitaka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kuwajibika kikamilifu kwa kuzuia matumizi ya dawa ambazo hazijathibitishwa kutokuwa na madhara.Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Anthony Tesha ambaye pamoja na kukiri kusikia habari hizo lakini alisema anaviachia vyombo husika kufuatilia jambo hilo.
source:Rombo kama Loliondo
"