Mbunge wa jimbo la Makadara nchini Kenya Gidion Mbuvi akiwa amevaa miwani ya jua pamoja na hereni na kuingia navyo Bunge.
Mbunge wa jimbo la Makadara nchini Kenya Gidion Mbuvi maarufu kama Sonko jana alitakiwa kutoka nje ya kikao cha bunge kutokana na kile kilichodaiwa kuvaa kwa namna isiyoendana na hadhi ya bunge.
Mbunge huyo aliingia bungeni akiwa amevaa miwani ya jua na hereni ndogo za masikioni zenye vito (studs) wakati Naibu Waziri wa Habari na Mawasiliano George Khaniri alipomtaarifu naibu Spika wa bunge Farah Maalim ndipo Sonko alipotakiwa kutoka nje ya bunge.
Naibu Spika Maalim amesema katika historia ya bunge la Agosti hakuna mbunge mwanaume aliyewahi kuingia bungeni amevaa hereni au kitu chochote masikioni, huku akisisitiza kuwa namna Sonko alivyokuwa amevaa haiendani na hadhi ya bunge.
Kabla ya Maalim hajachukua uamuzi wa kumumtaka Sonko atoke nje, alitoa nafasi ya kupata maoni mbali mbali kutoka kwa wabunge wengine kuhusiana na uvaaji huo, ambapo Mbunge wa Bumula Wakoli Bifwoli alisema sio sahihi kwa mbunge kuvaa kama mwanamke.
Wakati wakoli akisema hivyo Mbunge wa Kangundo Johnston Muthama alisema aina ya uvaaji huo unaashiria tabia nyingine kabisa ambayo haihusiani na wanaume waliokamilika na kuwa siku moja vijana watakuja kuvaa sidiria iwapo uvaaji huo utaachiwa uendelee.
Katika utetezi wake Mbuvi amesema kwa kuvaa hivyo alikuwa akiwakilisha vijana bungeni, lakini wabunge Fred Outa wa jimbo la Nyando na David Koech wa jimbo la Mosop hawakukubaliana nae, wakisema huo ni mfano mbaya kwa vijana na kuwa sio vijana wote huvaa kama alivyovaa mbunge huyo.
MO BLOG TEAM: Wadau mnalionaje suala la mbunge kutinga mavazi ya kisasa yanayokwenda na wakati?Ni kweli kwamba muonekano wa mbunge kimavazi una nafasi yake katika jamii au anaweza kuvaa vyovyote ilimradi atetee haki za wananchi anaowawakilisha?? Tupeni maoni yenu…!!!
"