Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa amejibu mapigo ya Chama cha Mapinduzi(CCM) na kusema kuwa Chama chake hakitasitisha maandamano yanayoendelea katika mikoa mbalimbali nchini na kwamba yupo tayari kwa lolote.
Akizungumza kwa njia ya simu akiwa njiani kutoka Mkoa wa Kagera jana, Katibu huyo aliitaka CCM iache kutapatapa baada ya kuona umma wa Watanzania wameamka na kuona jinsi serikali isivyopatia ufumbuzi kero zinazolalamikiwa na wananchi.
Kwa msisitizo akasema kuwa yeye na Mwenyekiti wake Freeman Mbowe wako tayari kwa lolote hata kama ni kukamatwa kwa ajili ya kutetea maslahi ya Watanzania.
Dk. Slaa alikuwa akijibu kauli ya Kamati Kuu ya CCM iliyotolewa juzi ambapo mbali na mambo mengine, imekilaumu Chadema kufanya maandamano katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na kuchochea uasi na machafuko nchini.
Akitoa tamko hilo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Kapteni mstaafu John Chiligati, alisema kufanya maandamano ni haki kikatiba, lakini kitendo cha viongozi wa Chadema kuhamasisha uasi na kuchochea chuki dhidi ya serikali iliyowekwa madarakani na wananchi ni kitendo kinachoweza kuvunja amani nchini.
Hata hivyo, Dk. Slaa alisema CCM ndio inasababisha vitendo vya uvunjifu wa amani nchini kutokana na Serikali yake kutowajali wananchi maskini, hivyo lawama hizo hazipaswi kwenda kwa viongozi wa Chadema waliojitolea kufa kwa ajili kupiga kelele kwa kukataa ukandamizwaji huo.
"Mimi sina hofu na kauli wanazozitoa CCM, waache wapige kelele kwani inaonyesha ni jinsi gani serikali ilivyoshindwa kuongoza na sasa wanahitaji huruma za wananchi ambao kwa miaka mingi wamenyimwa haki zao," alisema Dk. Slaa.
Aliendelea kusema "Nchi ni sawa na tunda la amani, lilokuwa juu ya mti unaoitwa haki, nashangaa sana CCM inavyopaza sauti juu ya amani pekee ikiwa inakakataa kutoa haki, tunachohitaji ni haki ifanyike."
Hata hivyo, alisema kabla ya kwenda kushtaki kwa wananchi kwa njia ya maandamano katika mikoa mbalimbali, walitumia wabunge kuilalamikia Serikali ndani ya Bunge juu ya malipo ya Dowans, Kagoda na Meremeta, lakini serikali ilikataa kutoa majibu.
Alisema, kama Serikali inaona maandamano wanayoyafanya yanavunja sheria ya nchi hakuna haja ya kukiadhibu Chadema, bali yeye na Mwenyekiti wake Mbowe wakamatwe.
Alimtaka Kapteni Chiligati kujifunza sheria na kusoma Katiba ya nchi kwanza kabla ya kuanza kutoa vitisho ambavyo vinaweza kuipeleka nchi katika sehemu mbaya.
"Naomba waache kukiadhibu chama, naomba wanitafute mimi na Mbowe watukamate tupo tayari kukamatwa kwa ajili ya kutetea wananchi, kinyume cha hapo moto huu hautazimika hadi kieleweke," aliongeza kusema.
Alisema wao kama chama cha upinzani wapo kama kioo cha kueleza mabaya yanayofanywa na serikali na kamwe hakuna vyama vya upinzani vinavyofanya kazi kuipigia debe Serikali kama wanavyotaka CCM.
Mapigo haya ya Dk. Slaa yanakuja siku moja baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa(Nec) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Kapteni John Chiligati kukutana na waandishi wa habari na kusema kuwa nyendo za Chadema zina agenda ya siri ya kuing’oa kwa nguvu serikali iliyoko madarakani kinyume cha Katiba, hivyo akaitaka serikali pamoja na vyombo vyake vya dola kuchukua hatua za kisheria haraka.
Kapteni Chiligati alisema Kamati Kuu inaungana na hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa mwishoni mwa Mwezi wa Februari, mwaka huu kukemea kauli za uchochezi ili kuinusuru nchi katika machafuko na pia zinavunja sheria za kikatiba za nchi.
“CCM inaviomba vyombo vya dola viwe imara kuchukua hatua za kisheria…wanachofanya Chadema ni kutuchonganisha na wananchi, kutoa kauli hatari za kujaribu kugilibu akili za watu ili kuchochea machafuko, umwagaji wa damu na uasi”, alisema Chiligati.
Alisema, hatua za Dk. Slaa kuendeleza malumbano na uchochezi kupitia maandamano ya wafuasi wake kunaonyesha kuwa hajakubaliana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwishoni mwa mwaka jana na kumfananisha na Jonas Savimbi aliyekuwa kiongozi wa Chama cha Unita cha nchini Angola.
Hata hivyo, kumeibuka kauli mbalimbali kutoka kwa viongozi wa vyama na taasisi binafsi wakikemea kitendo cha Chadema kuhamasisha uasi na chuki dhidi ya serikali iliyopo madarakani.
Miongoni mwa waliopaza sauti zao kukemea ni pamoja na Waziri wa Nchi ofisi ya Rais mahusiano na Uratibu, Steven Wasira ambaye alikitaka chama hicho kisije kikajilaumu pale Serikali itakapokosa uvumilivu na kutumia dola kudhibiti hali hiyo.
Wasira alisema Chadema hakina haki ya kufikiria kuiondoa Serikali madarakani ikiwa imechaguliwa na wananchi walio wengi kwa kura halali.
Waziri huyo alisema, kama hali ngumu ambayo Chadema inasema ndio chanzo cha wao kuandamana, ni jambo ambalo linatokana na mlolongo mrefu kutokana na dunia kukabiliana na matatizo ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta.
Naye Anne Kilango,Mbunge wa Same Mashariki (CCM), alinukuliwa akisema maandamano ya Chadema hayalengi kupinga malipo ya Dowans na badala yake yanafanywa ili kuhamasisha wananchi kufanya vurugu.
Kilango alisema kama kweli Chadema kinataka Dowans isilipwe kingeongeza nguvu za wanasheria ili kuhakikisha kesi iliyofunguliwa mahakamani na wanaharakati inafanikiwa na sio kuzunguka nchi mzima kumtaka Rais ajiuzulu.
"Najua ndugu zangu wa Chadema hawataki kusemeshwa lakini mimi kama kiongozi lazima niwaambie ukweli, kauli ya kumtaka Rais ajiuzulu hazifanani na lengo la kuishinikiza Serikali isilipe Dowans." alisema Kilango.
Naye Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema alisema kitendo cha kuiondoa madarakani Serikali bila kufuata taratibu za kikatiba kunaweza kuzalisha matatizo makubwa na kuliangamiza Taifa.
Mrema ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), alisema ufisadi na matatizo mbalimbali yanayoikumba Taifa sasa hayawezi kutatuliwa kwa maandamano na kwamba njia sahihi za kuleta ufumbuzi kwa wadau wote kuangalia njia bora isiyohatarisha uvunjifu wa amani ya nchi.
Naye Risasi Mwaulanga ambaye ni balozi wa Amani kutoka taasisi ya Unirvesal Peace Federation ametaka viongozi wa Chadema kukamatwa mara moja kwa kile alichokisema wanavunja amani ya nchi.
Akasema kuwa maandamano yanayoongozwa na Mwenyekiti wa Chadema ni ubunifu wa kutaka kukiangusha chama tawala kwa kupandikiza chuki baina ya wananchi na serikali kwa yale wanayoyaongea hadharani kuwa serikali imesababisha maisha magumu kwa wananchi.
”Hakika huu ni uhaini wa wazi ambao Chadema inaufanya, kwani unapokasirika umma na kupata hamasa mbaya matokeo yake ni kuzigomea sera na kukataa kushirikiana na serikali katika kazi za maendeleo." alisisitiza.
Source: :: IPPMEDIA