Mar 4, 2011
Pinda Ataka Ripoti Ya CAG Kuhusu Matumizi Ya Halamashauri
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akisalimia na wa Askofu Kilaini baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Bukobakwa ziara ya sikun nane mkoani Kagera.
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema anataka apatiwe taarifa za Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Fedha za Serikali kuhusu matumizi na mapato ya kila Halmashauri ili apate picha kamili ya matumizi ya fedha za Serikali.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Machi 4, 2011), mara baada kuwasili mjini Bukoba na kusomewa taarifa ya mkoa wa Kagera na Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Mohammed Babu. Waziri Mkuu yuko mkoani hapa kwa ziara ya siku nane ambako atakagua shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kutembelea wilaya zote za mkoa huu.
Akizungumza na viongozi mbalimbali wa mkoa huo, Waziri Mkuu alisema kuna haja ya kumpatia taarifa hiyo juu ya ukaguzi uliofanywa na ofisi ya CAG. “Uzuri wa taarifa wa hiyo unaonyesha nani kapata nini na katumia vipi, pia utaona ni Halmashauri zipi zimepewa ripoti safi na zipi zimepewa ripoti chafu,” alisema.
Alisema Serikali inatuma fedha nyingi mikoani na katika Halmashauri kupitia miradi mbalimbali lakini matokeo halisi ya fedha hizo hayaonekani katika maisha ya Mtanzania wa kawaida.
Akitoa mfano, alisema fedha nyingi inatolewa katika Miradi ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya (DADPS) lakini impact yake kwa jamii haionekani. “Mkuu wa Mkoa inabidi ufuatilie kwa karibu matumizi ya fedha hizi kwa sababu kuna watu wametulia tu wanafanya watakavyo wakijua RC hawezi kufuatilia hadi miradi ya wilayani,” alionya.
“Mkoa wa Kagera umepata sh. bilioni 10 kwa ajili ya miradi ya DADPS na ninyi mna wilaya saba, maana yake ni kwamba kila wilaya ina zaidi ya sh.bilioni moja na ushee lakini kama fedha hii haionekani imefanya nini, hali inatisha.
Akizungumzia kuhusu kero za wananchi, alishauri Mkuu wa Mkoa na kila Mkuu wa Wilaya watenge siku maalum za kusikiliza wananchi na kuwapatia suluhisho kwa matatizo hayo na kwa yale yaliyoshindikana, wapeleke taarifa ngazi za juu.
Kuhusu elimu, alisema mkoa unakabiliwa na tatizo la mimba hali ambayo alisema hairidhishi kutokana na idadi kubwa ya wasichana waliopata ujauzito. “Katika mwaka 2009/2010 jumla ya watoto 339 waliacha shule kutokana na ujauzito na kati yao 70 ni wa shule ya msingi… hii inatisha. Ongeeni na wazazi na walimu, lakini zaidi watafuteni wakosaji, wakiwekwa ndani hata watu 10, basi watajua kuwa hili ni baya,” alisisitiza.
Akizungumzia matatizo ya mkoa kwa ujumla, Waziri Mkuu alisema ataendelea kufuatilia tatizo la takwimu kwani anataka kubaini ni kwa nini mkoa wa Kagera kwa miaka mitano mfululizo umekuwa miongoni mwa mikoa mitano ya mwisho kwenye Kiashiria cha Kipato cha Wastani wa Mwananchi (Per-Capita Income) wakati una rasilmali za kutosha na fursa nyingi za uzalishaji.
Aliitaja mikoa mitano ya mwisho ambayo iko chini ya wastani wa Kitaifa wa pato la mtu ambalo limefikia sh. 693,470 kwa mwaka; ni Kigoma ulioko nafasi ya 17 ukiwa na wastani wa pato la mwananchi la sh. 483,158; Shinyanga wa 18 (sh. 455,000); Kagera wa 19 (sh. 453,235); Dodoma wa 20 (sh. 414,597) na Singida ambao ni wa mwisho ukiwa na wastani wa sh. 373,694.
Mchana huu, Waziri Mkuu anatarajiwa kuzindua barabara ya Zamzam na kuzungumza na wakazi wa Manispaa ya Bukoba katika uwanja wa Mayunga (Uhuru Platform).
Kesho (Jumamosi, Machi 5, 2011), Waziri Mkuu atakwenda wilaya ya Muleba ambako atakagua shamba la mkulima bora wa kahawa katika kijiji cha Ilogero kabla ya kwenda Buganguzi ambako atakagua mashamba ya migomba ambayo yameshambuliwa na magonjwa ambayo mpaka sasa hayajajulikana kisayansi. Pia ataweka jiwe la msingi katika mradi wa umwagiliaji wa kijiji cha Buyaga na kuhutubia wananchi katika viwanja vya Shule ya Msingi ya Kasharunga.
Kesho kutwa (Jumapili, Machi 6, 2011), Waziri Mkuu atakuwa wilayani Chato ambako anatarajiwa kuweka jiwe la msingi katika jengo la Halmashauri ya Wilaya hiyo na kufungua SACCOS ya Mshikamano kabla ya kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye shule ya msingi ya Chato.
"