1. Ni imani ya Ubalozi wa Tanzania Beijing kwamba Watanzania wanaoishi China na nchi za uwakilishi za Vietnam, Korea Kaskazini na Mongolia wanafuatilia maendeleo baada ya tetemeko kubwa la ardhi lililotokea Japan tarehe 11 Machi, 2011 na kufuatiwa na sunami na kusababisha uharibifu katika vinu vya kuzalisha umeme vya nyuklia vilivyopo katika mji wa Fukushima nchini humo.
2. Mamlaka za Japan zikisaidiwa na jumuiya ya kimataifa zimo katika jitihada kubwa kudhibiti uvujaji wa mionzi ya nyuklia ambao kama utatokea kwa kiwango kikubwa, utaweza kuathiri eneo kubwa ndani na nje ya Japan na kuhatarisha afya na maisha ya watu katika maeneo yataoweza kufikiwa na mionzi hiyo. Wote tunaomba juhudi hizo zifanikiwe ili kuepuka janga kubwa zaidi ya lililokwishatokea. Kama juhudi hizo zitashindikana, na kutegemea mazingira mbali mbali ya hali ya hewa, China itaweza pia kuathirika kwa kufikiwa na mionzi ya nyuklia kama itavuja kwa wingi huko Japan.
3. Ingawa China na Japan zinatenganishwa na masafa marefu ya bahari, mionzi ya nyuklia kama itavuja kwa wingi Japan itaweza kufika China ingawaje kwa viwango vya chini baada ya kuchujuka njiani, kama pepo za baharini zitavuma kuelekea Kusini Magharibi kutoka sehemu yenye vinu vilivyoathirika. Hadi sasa pepo hizo zinavuma kuelekea Kusini Mashariki ambako ni eneo la bahari ya Pacific, lakini mwelekeo huo unaweza kubadilika wakati wowote.
4. Kwa kuzingatia ukweli huo, Ubalozi unawashauri Watanzania wanaoishi China na nchi za uwakilishi wa Ubalozi huu, kuwa katika hali ya tahadhari.
Tahadhari hizo ni pamoja na:-
(a) Kufuatilia wakati wote hali ya mambo inavyoendelea kuhusiana na uvujaji wa mionzi ya nyuklia huko Japan.
(b) Kujiwekea akiba ya kutosha ya chakula na maji ili kujiweka taari na ushauri wa kujifungia majumbani kama utabidi kutolewa na mamlaka za China. Zaidi ya vyakula vya kawaida vya kupika, ni muhimu pia kujiwekea akiba ya vyakula vikavu vya aina ya biskuti, “cookies” na vingine vinavyoweza kudumu kwa muda mrefu bila kuharibika.
(c) Kujiwekea akiba ya kutosha ya dawa za msingi hasa kwa wale wenye magonjwa sugu kama vile shinikizo la damu na kisukari.
(d) Kuweka tayari nyaraka za kusafiria ili kama utatokea ushauri wa kuondoka kwa dharura, mtu awe tayari mara moja.
(e) Kwa wale ambao hawajajiandikisha Ubalozini, wafanye hivyo haraka iwezekanavyo, kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya Ubalozi ?? ?? ?? ? ? official website of Tanzania embassy-beijing NO.8 liang ma he nan lu,beijing. Wanaweza pia kujindikisha kwa kuwasilisha taarifa zao Ubalozini kwa njia a barua pepe kutumia anwani za beijing@foreign.go.tz, ekitokezi@hotmail.com, manongign@yahoo.com au nukushi (fax) namba +86 10 65324351 au +86 10 65321695. Miongoni mwa taarifa za msingi zinazohitajika ni pamoja na:
Jina
Anwani ya Unapoishi
Kazi Unayofanya
Anwani ya Unapofanya kazi
Anwani ya Barua pepe (e-mail)
Namba za simu (mkononi; kazini; nyumbani)
Paspoti: Namba
Ilipotolewa
Tarehe iliyotolewa
(f) Kuarifu Ubalozi kuhusu jamo lolote lenye umuhimu katika kujiandaa na/au kukabili hali inayohusu janga la mionzi ya nyuklia au jambo jingine lolote. Zifuatazo ni miongoni mwa namba za simu za Ubalozi na Wanaubalozi zinazoweza kutumika:-
+86 10 65321491/ 65321408/ 65322153
+8613641337072
+8613691408047
+8613522860308
Angalizo Muhimu :-
Tangazo hili halimaanishi hata kidogo kuwa hali imeanza kuwa mbaya nchini China au kuna dalili za hali hiyo. Madhumuni yake ni kuwaweka Watanzania katika hali ya tahadhari na mwamko wa kufuatilia hali inavyo endelea. Kwa hivyo, hakuna haja wala sababu ya taharuki na fadhaa. Watanzania wanatakiwa wawe watulivu na waendelee na shughuli zao za kila siku na kuzingatia ushauri uliotolewa. Ubalozi utaendelea kuwa karibu na mamlaka husika za China na kutoa taarifa kupitia tovuti yake ?? ?? ?? ? ? official website of Tanzania embassy-beijing NO.8 liang ma he nan lu,beijing na/au njia nyingine yoyote, kila haja itapotekea.
Ubalozi wa Tanzania, Beijing
18 Machi, 2011
"