Adverts

Apr 4, 2011

RAIS KIKWETE AAGIZA WIZARA YA UJENZI KUKISHUGHULIKIA MARA MOJA KILE ALICHOKIITA “GENGE LA WATU WALIOJIPANGA KUIDHULUMU SERIKALI NA WANANCHI” ….

Rais Jakaya Kikwete (katikati)Balozi wa Japan nchini Hiroshi Kanagawa (kulia) wakikata utepe na Waziri wa Ujenzi John Magufuli akishuhudia kukatwa kwa utepe wakati Rais Jakaya Kikwete alipoweka jiwe la msingi la upanuzi wa Barabara ya New Bagamoyo Road, eneo la Mwenge-Tegeta, katika sherehe iliyofanyika Mwenge mjini Dar es Salaam leo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameiagiza Wizara ya Ujenzi kukishughulikia mara moja kile alichokiita “genge la watu waliojipanga kuidhulumu Serikali na wananchi” kwa kuwalipa mabilioni ya fedha makandarasi ambao ujenzi wao wa barabara ni wa kiwango hafifu na cha chini.
Aidha, Rais Kikwete ameigiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuacha mara moja kugawa maeneo ya wazi na badala yake kuyasimamia ipasavyo maeneo hayo yakiwamo yale ya watoto kuchezea kwa kuzuia kabisa ujenzi katika maeneo hayo.
Ili kutekeleza hilo, Rais Kikwete, ameagiza kuondolewa na kubomolewa mara moja kwa mabati yaliyozungushiwa katika eneo la Jangwani, Dar es Salaam, ambalo kwa jadi ni eneo la viwanja vya kuchezea watoto na hivyo kuzuia ujenzi uliopangwa kufanyika katika eneo hilo.
Rais Kikwete ametoa maagizo hayo leo,Jumatatu, Aprili 4, 2011, wakati alipoweka jiwe la msingi la upanuzi wa Barabara ya New Bagamoyo Road, eneo la Mwenge-Tegeta, katika sherehe iliyofanyika Mwenge mjini Dar es Salaam. Rais Kikwete ameshirikiana na Balozi wa Japan katika Tanzania, Mheshimiwa Hiroshi Nakagawa katika uwekaji huo wa jiwe la msingi.
Ujenzi wa kipande hicho cha kilomita 12.9 kutoka Mwenge hadi Tegeta unagharimiwa kwa kiasi cha shilingi bilioni 88 na serikali ya Japan na barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami kwa njia nne na vituo 22 vya mabasi.
Akizungumza kwenye sherehe za uwekaji wa jiwe hilo la msingi ya upanuzi wa barabara hiyo, Rais Kikwete pia alitangaza kuwa Serikali baada ya kuwa imeendesha kwa mafanikio Mfuko wa Barabara (Road Fund) sasa inaanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Barabara (Road Development Fund) akifafanua kuwa Road Fund kazi yake ni kufanya matengenezo ya barabara na mfuko mpya utakuwa na jukumu la kujenga barabara.
Rais Kikwete pia amekejeli baadhi ya madai ambayo yamekuwa yanatolewa na baadhi ya wananchi kuwa maendeleo ya Tanzania yanakwenda kwa kasi ndogo kulinganisha baadhi ya nchi nyingine za Afrika zikiwamo baadhi ya nchi za jirani.
“Tanzania ni nchi kubwa. Ukubwa una uzuri wake na una gharama zake. Umeme uliovutwa kutoka Kidatu hadi Tarime, kwa mfano, kama ungewekwa katika baadhi ya nchi nyingine, umeme huu ungefungwa hata kwenye matendegu ya vitanda. Na hata ujenzi wa barabara za lami wa barabara tunazozijenga katika miradi yetu 105 katika nchi nyingine barabara hizi zingeingia hata majumbani mwa watu. Jamani, Tanzania ni nchi kubwa na maendeleo yetu ni makubwa, tuache kuilinganisha na nchi nyingine hizi ndogo ndogo.”
Kuhusu ujenzi wa barabara kwa kiwango kisichoridhisha, Rais Kikwete amesema: “Barabara zina gharama kubwa sana na nyingine zinajengwa kwa kiwango hafifu kwa sababu mbili., Moja ni kwamba mhandisi mshauri wetu ni mzembe ama Wizara na Wakala wa Barabara (Tanroads) nao wanazembea na kuwalipa makandarasi ambao barabara zao ni za kiwango duni.”
“Tunawalipa kwa nini? Nimelisemea hili na sitaki kulisemea tena. Lipo genge zima la watu waliojipanga kudhulumu – Waziri hili lazima liishe. Sitaki kulisemea tena,” Rais amemsisitizia Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli ambaye kabla ya hapo alikuwa ametoa hotuba ya kusisimua kuhusu mafanikio makubwa ya Serikali ya Kikwete katika ujenzi wa barabara nchini.
Kabla ya hapo, Rais Kikwete amezungumzia ugawaji holela wa viwanja katika maeneo ya wazi wazi na yale ya watoto kuchezea michezo: “Na nyie watu wa Ardhi, juzi nimepita Jangwani nikienda Morogoro na kuona mtu amezungushia mabati kwenye kiwanja cha kuchezea watoto. Kabomoeni wenyewe mabati yale. Nimelisemea mara nyingi hili la kulinda maeneo ya wazi na maeneo ya watoto wetu kuchezea. Sitaki kulisemea tena. Nendeeni mkaondoe yale mabati yote na eneo libakie la watoto kuchezea.
Rais Kikwete pia ameishukuru Serikali ya Japan na watu wake kwa kuendelea kutoa misaada muhimu katika maendeleo ya Tanzania.
Rais Kikwete pia amewaomba walioshiriki katika sherehe hiyo kusimama kwa dakika moja kuwakumbuka maelfu kwa maelfu ya wananchi wa Japan ambao majuzi wamepoteza maisha yao katika mafuriko na uharibifu uliosababishwa na tetemeko kubwa la ardhi lililofuatiwa na kimbunga cha tsunami.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
04 Aprili, 2011
"