Adverts

May 8, 2011

MAMA SALMA AASA WATANZANIA KUTOJITUPA KWENYE MIJADALA YA SIASA NA KUSAHAU MAENDELEO

Na Anna Nkinda – Maelezo, Mkuranga
Wananchi wilayani Mkuranga wametakiwa kuachana na itikadi za kisiasa katika shughuli  za maendeleo kwani suala la maendeleo linamgusa kila mtu na si chama cha kisiasa.
Wito huo umetolewa jana na mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akifungua Chama Cha kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) ya Salma Kikwete iliyopo kijiji cha Hoyoyo wilayani Mkuranga katika mkoa wa Pwani.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa hivi sasa wananchi wanatakiwa kuachana na masuala ya kampeni za uchaguzi na kujishughulisha zaidi katika mambo ya maendeleo pasipo kubaguana kwani wakati wa kampeni ulishapita mwaka 2010
“Nataka mfahamu kuwa SACCOS ni chombo cha kujiletea maendeleo hata kama chimbuko lake ni ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),wewe kama utakataa kujiunga na SACCOS hii  kwa madai kuwa mbona ina jina la mama Kikwete, mbona ilifunguliwa na  Mke wa Rais shauri lako wenzako watajiunga, watapata pesa na kuzifanyia shughuli za maendeleo wewe utabaki kama ulivyo,”alisema Mama Kikwete.
Aidha Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwaasa wanachama wa SACCOS hiyo kuitumia vizuri mikopo watakayoipata katika shughuli za maendeleo kama kuongeza mitaji ya biashara, kuboresha mashamba na makazi na kuboresha maisha ya familia kwani kwa kufanya hivyo watayaona manufaa ya SACCOS.
Mama Kikwete alionya, “Mkitumia vibaya mikopo watakayoipata mtashidwa kuboresha maisha yenu na wakati mwingine kushindwa kurudisha fedha mlizozikopa ambazo wanachama wengine wanazihitaji. Na hatimaye SACCOS yenu kufilisika.”
Aliwaomba wataalamu wa biashara wawe karibu na wananchi ili kuwapa elimu ya kuendesha biashara na hatimaye biashara hizo ziweze kuzalisha faida na hivyo kuwapa wepesi wa kurudisha fedha walizokopa.
Wanachama wengi wa SACCOS hiyo wanategemea kilimo, lakini Mama Kikwete aliwashauri  wakishiriki katika biashara ndogondogo ambazo zitawasaidia kupata mahitaji muhimu ya familia  ili kuongeza kipato kinachopatikana kutokana na kilimo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mkuranga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini  Adam Malima alisisitiza kuwa jambo kubwa wanaloliangalia hivi sasa ni jinsi ya kumkomboa mwananchi kutoka katika hali ya maisha duni na kuishi maisha ambayo yatampatia kipato kila siku na hivyo kujikwamua na umaskini.
“Ninakupongeza sana kwa jitihada  zako unazozifanya za kuwakomboa wananchi hasa waishio vijijini nasi tunakuunga mkono kwa kuwahimiza wananchi waone umuhimu wa kujiunga na vikundi mbalimbali vya maendeleo kwani kwa kufanya hivyo watakopa na kupata pesa ambazo zitawasaidia kufanya mambo ya maendeleo,”alisema Malima.
Akielezea historia ya SACCOS hiyo Somoye Kilimile ambaye ni Mweka hazina alisema kuwa ilitokana na wazo  la Mama Kikwete la kutumia sehemu ya shamba lake kama kituo cha mafunzo ya kilimo na ufugaji alichokizindua tahere 23/02/2008 kama shamba darasa kwa ajili ya kujifunza uzalishaji wa zao la pilipili baridi (paprika), migomba, miembe ya kisasa na ufugaji wa kuku wa kienyeji chini ya usimamizi wa taasisi ya WAMA, viongozi wa kijiji cha Hoyoyo, wilaya ya Mkuranga na Wizara ya Kilimo.
Alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni upungufu wa mtaji kwani lengo lao ni kupata mtaji wa zaidi ya shilingi milioni 100 na mtaji walionao ni shilingi milioni tatu na laki nane, ukosefu wa fedha kwa ajili ya kuendeshea ofisi ikiwa ni pamoja na gharama za kukodi, mishahara na shajala na ukosefu wa eneo kwa ajili ya kujenga ofisi ya kudumu.
“Mipango ya baadaye tuliyonayo ni kutafuta shamba kwa ajili ya kuanzisha kilimo cha mazao ya biashara na chakula pamoja na ufugaji kutafuta eneo na kujenga jengo litakalotumia kwa shughuli za ofisi na kitega uchumi na kuanzisha miradi midogomidogo na ya kati kwa ajili ya kutoa ajira kwa wanachama”, alisema Kilimile.
SACCOS hiyo ilianzishwa tarehe 12/10/2009 ina wanachama 103 kati ya hao 65 ni wanawake na 38 ni wanaume.
Zaidi ya shilingi milioni 51 zilipatikana katika harambee iliyoendana sambamba na ufunguzi wa SACCOS hiyo ambapo Taasisi ya WAMA iliichangia shilingi  milinoni tatu  na laki nane .