Na Anna Nkinda – Maelezo, Dodoma
Wanachama wa Umoja wa Wanawake
Tanzania (UWT) nchini wametakiwa kushirikiana na vijana wasomi
katika kufanya kazi zao ili kuboresha utendaji wao wa kazi kwani nguvu kazi
zaidi itatokana na vijana hao na siyo vinginevyo.
Wito huo
umetolewa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanachama wa umoja huo
katika ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma.
Mama Kikwete
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa
hivi sasa vijana wasomi wanafanya kazi zao na kushindana kwa hoja zenye nguvu
kutokana na elimu waliyo nayo hivyo basi kama wataamua kuwatumia umoja huo
utanufaika na kuwa na mabadiliko ya kiutendaji.
“Shirikianeni
na wasomi wa vyuo vikuu, wafundisheni kazi, wapeni nafasi na siyo
kuwapinga kwa kuwaona kuwa wao wanajua zaidi kuliko ninyi kwani hivi sasa Dunia
imebadilika inaenda sambamba na teknolojia hivyo basi ni rahisi kwa vijana
kufahamu mambo mengi tofauti na wazee na mkumbuke kuwa ili muweze
kushindana ni lazima mfanye mageuzi,” alisema mama Kikwete.
Aidha Mama
Kikwete aliwasisitiza kina mama hao kuwa na tabia ya kutunza siri na kuhifadhi
yale yote ambayo yanajadiliwa ndani ya vikao vya Chama na siyo
kuyaongea nje kwa watu wasiohusika.
Mwenyekiti huyo
wa WAMA pia aliwataka wanawake hao kuongeza juhudi ya kuwahamasisha akinamama
wengi zaidi kujitokeza kuwania uongozi katika nafasi za majimbo na kata , kwani
ni dhahiri kwamba wanawake wengi wamejitokeza kwenye nafasi za viti maalum
kuliko za kata na majimbo.
Alimalizia
kwa kuwasisitiza kina mama hao kuongeza ushirikiano kupitia
vikundi vya maendeleo ya kiuchumi kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia wanawake
wengi zaidi kufaidika na fursa zilizopo chini ya mipango ya Serikali ya
kumkomboa mwanamke.
Akisoma taarifa
ya UWT ya mkoa wa Dodoma Katibu wa umoja huo Amina Kanyogoto alisema kuwa
wamekuwa wakihamasisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi kwa kufanya semina
kwa kila kata, kutoa semina kwenye mabaraza ya wilaya na mkoa, kutoa ushauri
nasaha kupitia kwa viongozi wao kujitokeza kwenda kupima kwa hiari na kutoa
semia kwa waelimisha rika.
Aliyataja
mafanikio waliyoyapa hadi sasa ni wanawake wengi kuwa na mwamko wa kugombea
nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi zote baada ya kuhamasishwa
na pia kina mama wengi wamekuwa na ari ya kufanya biashara ndogondogo za
kujitafutia kipato cha familia zao.
Kanyogoto
alisema, “matatizo yanayotukabili ni ukosefu wa fedha kwa ajili ya uendeshaji
wa shughuli za uzalishaji mali kwa wajasiriamali wanawake, mikopo
inayotolewa haitoshelezi mahitaji na bidhaa zinazotengenezwa na
kina mama bado ni tatizo kwa ajili ya ukosefu wa masoko na uuzaji wa bidhaa
hizo.”
Mama Kikwete
yupo mjini Dodoma kwa ajili ya kuhudhuria matembezi ya uchangishaji wa chakula
kwa shule za msingi yatakayofanika kesho tarehe 29/5/2011 yaliyoandaliwa na
Shirika la Chakula Duniani (WFP) kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali ya
hapa nchini.
Mwisho.