Adverts

May 23, 2011

WAKE WA MABAROZI WAPONGEZWA KWA MCHANGO WAO HAPA NCHINI

Na Anna Nkinda – Maelezo
  Kikundi cha wake wa mabalozi wa Afrika kimepongezwa kwa mchango wake mkubwa wa kuchangia na kusaidia huduma mbalimbali za kijamii hapa nchini.
Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na watu waliohudhuria chakula cha hisani cha kuchangia fedha kwa ajili ya kusaidia huduma za kijamii hapa nchini kilichoandaliwa na kikundi hizo katika Hoteli ya Movenpick jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa miaka kumi iliyopita kikundi hichokilianzishwa kwa malengo ya kuisaidia jamii ya watanzania jambo ambalo limewafanya wanawake na watoto kufaidika na misaada inayotolewa na wake hao wa mabalozi.
Aidha Mama Kikwete aliwahakikishia wake hao wa mabalozi kuwa fedha ambazo zitachangishwa usiku huo zitatumika kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto ambayo ni malengo mojawapo ya maendeleo ya milinia.
Akimkaribisha mgeni rasmi katika hafla hiyo Mwenyekiti wa kikundi hicho Mama Aletha Isaack ambaye ni mke wa Balozi wa Namibia alisema kuwa wao kama wanawake wamekuwa wakiguswa sana na mambo yanayowahusu wanawake na watoto hapa nchini.
Alisema kuwa wameamua kuunganisha mikono yao pamoja na Serikali na Sekta binafsi hapa nchini ili kuhakikisha kuwa malengo namba nne na tano ya milinia ya kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto yanatimizwa.
“Ili kuhakikisha maisha ya watanzania yanaimarika kwa mwaka huu hadi sasa tumeshaisaidia Taasisi ya WAMA kwa kuchangia upande wa elimu kwa watoto wa kike, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili upande wa kansa kwa watoto, kituo cha watoto yatima Nira na wahanga wa mabomu ya Gongo la Mboto”, alisema Mama Isaack.
Mwenyekiti huyo aliendelea kusema kuwa ili kupata fedha za kuwasaidia wahitaji kikundi hicho kimekuwa kikifanya shughuli mbalimbali za kupata fedha ikiwa ni pamoja na kuandaa chakula cha hisani, harambee na maonyesho ya mavazi.
Kila mwaka kikundi hicho cha wake wa mabalozi wa Afrika kimekuwa kikiandaa chakula cha hisani na kuchangisha fedha ambazo zimekuwa zikifanya shughuli mbalimbali za maendeleo huku ujumbe wa mwaka huu ukiwa ni kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto nchini Tanzania.
Mwisho.