Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini Ijumaa, Juni 10, 2011, kwenda Afrika Kusini ambako atakuwa na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za jumuia tatu za uchumi katika Afrika.
Aidha, akiwa Afrika Kusini, Mheshimiwa Rais Kikwete atashiriki katika mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambao watajadili hali ya kisiasa katika Zimbabwe.
Vile vile, Rais Kikwete atakuwa miongoni mwa wakuu wa nchi za Afrika na nje ya bara hilo watakaoshiriki mazishi ya mpigania uhuru mashuhuri wa Afrika Kusini Mama Albertina Sisulu, mke wa mpigania uhuru mwingine mashuhuri wa nchi hiyo, marehemu Walter Sisulu. Shughuli kubwa ya kwanza ya Mheshimiwa Rais Kikwete asubuhi ya kesho, Jumamosi, Juni 11, 2011, itakuwa ni kuhudhuria shughuli za mazishi ya Mama Sisulu ambazo zitafanyika kwenye Uwanja wa Soka wa Orlando ulioko mjini Johannesburg.
Keshokutwa, Rais Kikwete ataungana na wakuu wa nchi wanachama wa jumuia za SADC, EAC na COMESA kujadili uwezekano wa kuunganisha jumuia hizo tatu za uchumi ili kuunda kundi moja kubwa zaidi kuliko jingine la kufanya biashara huru katika Bara la Afrika.
Imetolewa na: Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, DAR ES SALAAM. 10 Juni, 2011 |