Waziri wa Maji, Profesa. Mark Mwandosya |
Waziri wa Maji, Profesa.
Mark Mwandosya ameiagiza Idara ya Rasilimali za Maji ifanye upya uchunguzi wa
mwenendo wa maji chini ya ardhi wilayani Urambo na kuishauri Halmashauri ya
Wilaya hiyo ili tatizo la kuchimba visima visivyotoa maji
lisijirudie.
Prof. Mwandosya aliyasema
hayo jana( siku ya Jumatano), wakati anapewa taarifa ya utekelezaji wa miradi
iliyo chini ya mpango maalum wa kuboresha huduma ya majisafi na majitaka jijini
Dar es Salaam katika makao makuu ya Wizara hiyo.
Prof. Mwandosya ametoa
agizo hilo baada ya kukutana na kamati ndogo iliyotumwa na Halmashari ya Wilaya
ya Urambo kumweleza dai lao la kutoilipa kampuni ya PNR baada ya visima 9 kati
ya 12 vilivyochimbwa na kampuni hiyo kutotoa maji.
Kamati hiyo ilimweleza pia
Mhe.Waziri huyo nia yao ya kutaka kumshitaki pamoja na kumtaka Mhandisi Mshauri
aliyependekeza eneo la kuchimbwa visima kuirudishia Halmashauri hiyo zaidi ya
sh. Milioni 120 alizolipwa.
Prof. Mwandosya amesema
baadhi ya wananchi wanadhani kuwa fedha ambazo zingetumika kuwalipa wakandarasi
waliovurunda kazi zao kama PNR zinarudishwa wizarani kwake. Prof. Mwandosya
ameeleza kuwa dhana hiyo si sahihi kwani fedha za kugharamia miradi ya maji
iliyochini ya Halmashauri hazipitii Wizarani kwake badala yake fedha hizo
hupitia TAMISEMI.
Aidha, Prof. Mwandosya
amewatahadharisha DAWASA pamoja na watendaji wengine kuwa makini wakati wa
kufanya uchunguzi wa kufuatilia mwenendo wa maji chini ya ardhi katika maeneo
mbalimbali yaliyotengwa kwa ajili ya uchimbaji wa visima likiwemo eneo la Mpera
wilayani Mkuranga na Kimbiji wilayani Temeke ili tatizo kama lililojitokeza
Wilayani Urambo lisijirudie