Adverts

Jun 22, 2011

OFISI YA BUNGE YATOA TAARIFA JUU YA HABARI ILIYOCHAPISHWA NA GAZETI LA DIRA YA MTANZANIA…

YAH: TAARIFA POTOFU YA GAZETI LA DIRA YA MTANZANIA TOLEO LA JUMATATU, 20 – 26 JUNI, 2011 ‘ SAKATA LA POSHO ZA WABUNGE’ SPIKA MAKINDA MBUMBUMBU ‘Utafiti wabaini anasimamia asichokijua magwiji wa Bunge washangaa tamko lake’.

1.0UTANGULIZI

Pamoja na Vichwa vya habari hiyo, Katika taarifa hiyo Mwandishi wa gazeti hilo amedai kuwa;
i.Spika wa Bunge, Anne Makinda hana uelewa wa kutosha wa jinsi mbunge anavyoweza kupoteza wadhifa wake
ii.Pia Spika wa Bunge haelewi mfumo wa malipo ya Posho za Wabunge
iii.Spika hana mamlaka ya kumfukuza Mbunge yeyote anayekataa kusaini Fomu za kuchukua posho ya kikao.

2.0MAJIBU YA HOJA POTOFU ZILIZOTOLEWA
Ofisi ya Bunge ingependa kuwaarifu wananchi kwamba habari hiyo iliyoandikwa na gazeti la Dira ya Mtanzania ni ya dharau na haina ukweli wowote na imeandikwa kwa nia mbaya ya uchochezi na kuharibu sifa aliyonayo Mhe. Spika Bungeni na kwa watanzania kwa ujumla.
Ili kuondoa upotofu wa taarifa iliyotolewa na gazeti hili, Ofisi ya Bunge ingependa kutoa ufafanuzi wa hoja zilizotolewa kama ifuatavyo;

i. Sio kweli kwamba Mhe. Anne Makinda hana uelewa kuhusu uendeshaji wa shughuli za Bunge. Mhe. Makinda amekuwa mbunge kwa zaidi ya miaka 30 Bungeni na kwa kipindi hicho chote ameshika nyadhifa mbalimbali Bungeni na Serikalini. Aidha akiwa Naibu Spika ameongoza kamati ya Bunge iliyoshiriki marekebisho ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la 2007.

Kwa mantiki hiyo anazifahamu vyema Kanuni za Bunge na ana uzoefu na uendeshaji wa shughuli za Bunge kwa muda mrefu kuliko hata idadi kubwa ya wabunge wapya waliopo Bungeni. Katika utendaji wake, hafanyi kazi kwa kuvutwa na hisia bali husimamia uendeshaji wa Bunge kwa Mujibu wa Kanuni za Bunge ambazo tunashaka hata kama mwandishi wa gazeti hili anazifahamu vyema.
Ni kwa kuzingatia hilo aliwaeleza bayana Waandishi wa habari siku alipofanya nao mahojiano ambapo mwandishi wa gazeti hili pia hakuwepo, kuwa taratibu la kuchukua posho kwa Mbunge huenda sanjali na kusaini mahudhurio Bungeni (Mbunge anayehudhuria Bunge ndiye anayelipwa posho), kwa maana huwezi kumlipa posho Mbunge asiyekuwepo Bungeni. Mahudhurio ya Mbunge ni pale anaposaini fomu ya Mahudhurio. Kwa mantiki hii, kanuni zinamtaka bayana kila mbunge kuhudhuria vikao vya Bunge.

Kanuni ya 143 inatamka kuwa:
(1) kuhudhuria vikao vya Bunge na kamati ni wajibu wa kwanza wa kila mbunge.
(2) Mbunge yeyote atakaeshindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza Ubunge wake kwa mujibu wa ibara ya 71 (1) ya katiba na Spika ataiarifu Tume ya Uchaguzi.

(3) Mbunge atakapokosa kuhudhuria nusu ya vikao vya Mkutano mmoja bila ya sababu ya msingi atapewa onyo.

Hivyo basi kwa mantiki hiyo, Mbunge atakayeshindwa kusaini fomu za mahudhurio kwa mtiririko huo hapo juu atakuwa amepoteza sifa zake za kuwa Mbunge kwa mujibu wa Kanuni.
ii. Aidha ni kwa uvivu wa kufikiri au kwa makusudi kabisa, mwandishi wa gazeti hili ameandika yale aliyohisi ni sahihi na kufanya utafiti katika kiwango ambacho hajaeleza ni kwa kutumia vigezo gani bila hata kujaribu kuuliza misingi halisi aliyoizungumzia Mhe. Spika kuhusu uhalali wa mahudhurio ya Mbunge sanjali na ulipwaji wake posho awapo kazini.

Hivyo madai ya kuwa Spika hana madaraka ya kumfukuza Mbunge Bungeni hayana mantiki na wala madaraka ya Spika kuhusu kumfukuza Mbunge hayakuwa sehemu ya mahojiano na waandishi na Spika wa Bunge kama anavyodai, na Kanuni zimeeleza bayana kazi za Spika Bungeni. Kumbuka madaraka ya Spika, wajibu wa Wabunge na hata Miongozo mingine Bungeni huratibiwa kwa mujibu wa kanuni za Kudumu za Bunge.

Hatujui lengo la mwandishi ni lipi hasa kwa kuweza kutoa taarifa zenye upotoshaji mkubwa kwa umma na zenye kuleta dharau kwa kiongozi wa Bunge na Bunge kwa ujumla kwa kuzingatia kuwa kiongozi huyu amechaguliwa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.

3.0 HITIMISHO
Ofisi ya Bunge inapenda kuwaarifu wanahabari wote kuwa Idara yake ya Habari imekuwa ikitoa ushirikiano wa kutosha kuwaarifu waandishi kwa taarifa zozote wanazohitaji na inasikitishwa kwa kiasi kikubwa na uandishi unaojali hisia na wenye kulenga uchochezi badala ya kuelemisha.
Licha ya mwandishi wa habari hii kutokuwepo Dodoma na wala hakushiriki mahojiano hayo na Mhe. Spika, habari husika iliyoandikwa imelenga kutoa taarifa potofu bila kushirikisha hata upande wa pili kwa ufafanuzi. Kwa kuzingatia hilo Ofisi ya Bunge inamtaka Mhariri wa Gazeti la Dira ya Mtanzania kuomba radhi kwa uzito ule ule waliotoa habari yao ya kupotosha umma.

Deogratios Egidio
Kny: KATIBU WA BUNGE
21 Juni, 2011