TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
CHAMA cha Waandishi wa Habari mkoa wa Mbeya(MBPC) kimepokea
kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mwanahabari mwenzetu,Danny
Mwakiteleko kilichosababishwa na ajali ya gari jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa MBPC mkoa wa Mbeya,Christopher Nyenyembe
amekielezea kifo hicho kubwa ni pigo kubwa katika tasnia nzima ya habari hasa
kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao marehemu enzi za uhai wake.
“Mwakiteleko alikuwa kamusi ya kitaaluma na kisima cha
fikra,mfumbuzi na mbunifu wa kazi mbalimbali za kihabari na aliweza kufanya
kazi zake na kuibua vipaji vya waandishi wengine,hakika wengi hawatakuja
kumsahau”Alisema Nyenyembe.
Kwa kutambua uwezo aliokuwa nao kwa niaba ya waandishi wa
habari mkoa wa Mbeya nachukua fursa hii kutoa pole za dhati kwa ndugu na
familia yote ya Mwakiteleko bila kuwaacha marafiki zake wa karibu na
wafanyakazi wa New Habari alikokuwa akifanya kazi kama Naibu Mhariri Mtendaji.
Kifo cha Mwakiteleko licha ya kuwa pigo kubwa katika tasnia
ya habari kwa namna moja au nyingine kimetuachia fumbo kubwa kwa wanaharakati
wengine waliokuwa wakitumia kazi zao kupiga vita vitendo vya hujuma,rushwa na
ufisadi wa kutisha katika Taifa letu.
Mwakiteleko alikuwa kioo hasa cha jamii katika kutekeleza
majukumu yake,alikuwa mpole,mkalimu na mcheshi wakati wote lakini alikuwa
makini zaidi katika usimamizi na utendaji wake wa kazi ambao ulimjengea heshima
na nidhamu kubwa katika uongozi wake kama
Mhariri kila alipokuwepo.
Tunatambua kuwa kifo ndiyo njia pekee ya kumtenganisha binadamu
yoyote na ndugu zake,marafiki na jamaa wa karibu waliozoeana na kwa kuwa hayo
ndio mapenzi ya MUNGU,tumuache Mungu aitwe Mungu na jina lake lihimidiwe Milele…AMEN.
IMETOLEWA NA
CHRISTOPHER NYENYEMBE
MWENYEKITI
MBEYA PRESS CLUB