• Asaini tangazo la serikali lililochakachuliwa


RAIS Jakaya Kikwete amedanganywa tena na baadhi ya watendaji wake, akasaini tangazo lililochakachuliwa. Septemba 5 mwaka huu, Kikwete alisaini tangazo la kusudio la uanzishaji wa wilaya mpya ya Butiama, lakini katika namna ya kushangaza, sasa inaonekana eneo la wilaya mpya ni Nyamisisi.

Hali hiyo inayotia fedheha kwa Rais wa nchi, imebainika juzi wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipofika Butiama kuzuru kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Pinda alilazimika kuwatuliza wakazi wa eneo hili waliotaka kujua sababu za msingi za Rais kubadili msimamo wake na kuhamishia makao mapya yaliyotakiwa kuwa Butiama na kuyapeleka Nyamisisi.

Pinda alikiri bayana kuwa Rais alisaini tangazo hilo akijua kuwa kilichoandikwa ni makao makuu kuwa Butiama bila kujua eneo lililoandikwa ni Nyamisisi.

“Hata kama kuna mtu alitaka makao makuu yawe Nyamisisi, kwa kweli haikupaswa hiyo Nyamisisi kuchomekwa hivyo. Hata mngeniuliza mimi makao makuu yawe wapi, ningesema lazima yawe Butiama tu,” alisema Pinda na kushangiliwa.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema tangazo hilo lilikuwa na makosa kutokana na kutaja eneo la makao makuu tofauti na lile lililopendekezwa.
Pinda alisema mpango wa serikali ulikuwa ni makao makuu ya wilaya hiyo yawe katika kijiji cha Butiama ili kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Akijibu malalamiko ya wakazi wa Butiama, walioingia katika eneo la nyumba hiyo, wakimtaka atamke kuwa makao makuu yatakuwa Butiama, Pinda alisema:

“Hili la Butiama kwa kweli linaleta manenomaneno. Sisi serikalini tulidhani ukiwa na wilaya ya Butiama na makao makuu ni lazima yawe Butiama, ili tumuenzi Baba wa Taifa.

Hata hivyo, alisema pamoja na tangazo hilo kuchomekwa neno Nyamisisi, bado mtu aliyefanya hivyo hajafanikiwa, kwani tangazo hilo sio uamuzi wa mwisho wa kuhusu suala hilo.

Aliwataka wananchi wa Butiama kulichukulia tangazo hilo kuwa ni pendekezo tu ambalo wanapaswa kulitolea maoni yao kuhusu kulikubali au kulikataa na kwamba maamuzi ya mwisho kuhusu wapi yawe makao makuu ya wilaya hiyo yatatokana na maoni ya wananchi wenyewe.

Alisisitiza kuwa Butiama ikiwa wilaya sio tu huduma za msingi zitaboreshwa na kuwapa watu sababu ya kwenda wilayani hapo, bali pia itawapa sababu ya kwenda kuzuru nyumbani kwa Hayati Baba wa Taifa.

Pinda pia alimpa fursa mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, kutoa kauli yake kuhusu suala hilo, ambaye alisema yeye asingependa kuliingilia suala hilo.
“Hili suala halina tatizo, ninyi na wananchi wote mtakavyoamua ndivyo iwe hivyohivyo,” alisema Mama Maria. KUTOKA JAMII FORUMS