WATU 34 wa kijiji cha mtitu wilaya ya Kilolo mkoani Iringa ikiwemo familia moja ya watu sita wamenusurika kifo na kulazwa katika hospital teule ya wilaya ya Iringa (Hospital ya Ipamba) baada ya kunywa togwa katika sherehe ya kipaimara inayosadikika kuwa na sumu.
Tukio hilo lilitokea juzi jumapili katika kijiji hicho cha Mtitu wilaya ya Kilolo wakati watu hao walipofika kusherekea sherehe ya kipaimara cha mtoto Hotmary Mpogole na kupewa kinywaji hicho cha asili kilichotengenezwa kwa unga wa nafaka ya mahindi (togwa)
Akielezea juu ya tukio mhanga wa tukio hilo Geofrey Chavala alisema kuwa siku ya tukio aliitwa na rafiki yake wakati akitokea msibani kuwa waelekee katika nyumba hiyo kwa ajili ya kula wali wa sherehe na baada ya kufika walipewa chakula hicho na baada ya hapo walipewa togwa kama kisushio .
Hata hivyo alisema wakati akiendelea kunywa alibaini radha tofauti na ile ambayo amepata kuizoea kwa kinywaji kama hicho na hivyo kuonyesha kusitasita katika kuendelea kunywa japo alijitahidi kunywa hadi anamaliza lita moja peke yake.
Alisema baada ya kumaliza hali ya hewa tumboni ilibadilika na kujikuta akianza kutapika na kuhara damu hali iliyopelekea kurudi nyumbani na baada ya kufika huo alikutana na bibi yake na kuelezwa kuwa kama amekunywa togwa wenzake wanakusanywa kwa ajili ya kwenda Hospital ndipo alipoungana na wenzake hao.
Fedelika Chaula (40) ambaye ni mzazi wa watoto waliokuwa wakifanyiwa sherehe hiyo ya Kipaimara alisema kuwa aliandaa sherehe hiyo kwa ajili ya kuwapongeza watoto wake wawili na kuandaa togwa hiyo kwa ajili ya kunywaji kwa watu walioalikwa katika sherehe hiyo.
Hata hivyo alisema kuwa mahindi yaliyotumika kwa ajili ya kuandaa togwa hiyo ni mahindi ambayo wamekuwa wakiyatumia siku zote kwa ajili ya chakula na kuwa anashangazwa na kutumia nafaka hiyo kwa kutengeneza togwa na kupatwa na madhara hayo.
Alisema kuwa watoto wake wanne wamelazwa katika hospital hiyo pamoja na yeye mwenyewe kwa kunywa togwa hiyo .
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mtitu Beatus Kivamba akielezea tukio hilo alisema kuwa awali alikutana na watu wawili wakitoka katika sherehe hiyo huku wakitapika na kuraha kutona na kunywa togwa hiyo na baada ya kuwasiliana na muunguzi wa kituo cha afya Mtitu ndipo alipomthibitishia kupokea wagonjwa zaidi wa tukio hilo .
Alisema kutokana na tukio hilo alilazimika kuomba msaada kwa gari kwa Paroko wa Mtitu ambaye alitoa usafiri wa Lori na kuwachukua wagonjwa wote 34 na kuwafikisha katika Hospital hiyo ya Ipamba kwa matibabu.
Muuguzi mkuu wa Hospital hiyo ya Ipamba Sr. Julieta Mzena aliwataja waliofikishwa hospital hapo na kulazwa kuwa ni pamoja na watoto zaidi ya watano ambao ni wanafunzi na watu wazima wanaume na wanawake.
Aliwataja wahanga hao ambao wamelazwa kuwa ni pamoja na Yudita Ndongoro , Onolata Mhangara, Otineli Mpogole, Sekela Mbilingi, Jafarini Mhulila, Faines Mhulila, Agineli Luvinga, Sofia Mhulila, KIlelia CHongolo, Frolida Mgaya, Geofrey Chawala, Vero Kasuga, Meshack Chaula, Nemia Chaula, Baraka Kivale, Edison Kivale, MUstaphar Mhulila, na Gelion Mpogole.
Wengine ni Chelelina Chongolo , Raheli Mgogolo ,Kanisia Chongolo, Diana Chongolo , Chadeta Mlimakizi, Zaina Mpagama, Bile Mtono , Setty Kilave, Nesta Mwofuga,Manwela Mhagala ,Federika Chaula na mtoto Hotmery Mpogole mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi mtitu ambaye ndiye alikuwa ameandaliwa sherehe hiyo ya kipaimara.
Alisema kuwa hali za wagonjwa hao zinaendelea vizuri na kuwa tatizo lao inaonekana kula chakula chenye sumu.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Evarist Mangalla alisema kuwa yupo nje ya ofisi na kikazi na kuwa bado hajapata tarifa na kuahidi kufuatilia zaidi.