Adverts

Jan 8, 2012

Nyoni: Hakuna daktari aliyefukuzwa MNH

SERIKALI imesema haijawafukuza madaktari walio katika mafunzo ya vitendo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) waliogoma hivi karibuni na wala haina mpango wa kama huo.

Hayo yamesema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni.

Katibu huyo amelazimika kutoa ufafanuzi huo kutokana na vyombo kadhaa vya habari kuripoti kuwa, madaktari 229 walio katika mafunzo ya vitendo katika hospitali ya Muhimbili wamefukuzwa kutokana na kufanya mgomo wa nchi nzima kwa lengo la kushinikiza serikali kuwalipa malimbikizo ya posho zao yanayofikia Sh milioni 176.

Aliongeza kusema kuwa, ingawa madaktari hao walikiuka maadili ya weledi kwa kufanya mgomo, hakuna daktari aliyerudishwa nyumbani wala kufutiwa mkataba kutokana na ukweli kuwa siku zote serikali inatumia busara na njia sahihi kutatua matatizo bila kumuumiza mtu.

“Hakuna daktari aliyefukuzwa, bali serikali inafanya utaratibu wa kuwaita makao makuu ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupokea maelekezo ya mkataba mpya ili waweze kufanyakazi kwa kuzingatia kanuni na maadili na kurudisha nidhamu katika fani ya udaktari.

Wakati huo huo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda amesema Taifa linakabiliwa na uhaba mkubwa wa madaktari na watenda kazi katika sekta ya afya hivyo serikali haikusudii kupunguza idadi yao.

Akizungumza na HABARILEO Jumapili kwa njia ya simu, Dk Mponda alisema baada ya mgomo huo kutokea serikali ilichukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha kuwa wagonjwa wanaendelea kupata huduma ili kuzuia madhara ambayo yangeweza kusababishwa na mgomo huo.

Alisema hatua mojawapo iliyochukuliwa na serikali ni kuchukua madaktari 50 waliokuwa katika orodha ya madaktari waliokuwa wakisubiri kupata nafasi ya kufanya mafunzo kwa vitendo na kuwajumuisha na madaktari wengine 25 ambao hawakujihusisha na mgomo huo.

“Kwa kuwa tulikuwa na akiba ya madaktari ambao walikuwa wanasubiri fursa ya kufanya mafunzo kwa vitendo tuliwaita na kuwapa fursa iliyoachwa na wenzao waliogoma. Tulifanya hivyo kuzuia athari za mgomo hivyo serikali haina mpango wa kufukuza wala kupunguza wafanyakazi wa seta ya afya.

Anafafanua kuwa lengo la kuwaita wizarani madaktari waliopo kwenye mafunzo kwa vitendo ni kuwapangia vituo vipya vya kazi na kuwapatia mkataba ambao utasaidia kuboresha nidhamu katika sekta ya afya.

Baadhi ya magazeti ya kila siku nchini (siyo HABARILEO), katika matoleo ya jana yalipamba kurasa zao za mbele kwa habari za kufukuzwa kwa madaktari 229 kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa madai ya kujihusisha na mgomo uliodumu kwa siku mbili wakishinikiza kulipwa malimbikizo ya posho.

Source: Habarileo