Nchi za Magharibi zimewataka raia wao kuondoka haraka katika mji wa Benghazi mashariki mwa Libya, kufuatia kile nchi hizo zilichokiita ''kitisho maalum ambacho kinaweza kutekelezwa haraka''.
Uingereza ndio iliyokuwa nchi ya kwanza kuwataka raia wake waondoke mara moja mjini Benghazi, na baadaye ikafuatiwa na Ujerumani. Nchi hizo zilikuwa zimewashauri rai wao kuacha kufanya safari katika sehemu nyingi za Libya, baada ya mashambulizi ya mwezi Septemba kwenye ubalozi mdogo wa Marekani mjini Benghazi, ambayo yalimuua balozi wa nchi hiyo Christopher Stevens na maafisa wengine watatu wa ubalozi huo.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, alisema kitisho mjini Benghazi dhidi ya raia wa nchi za magharibi ni cha dhahiri.
Mzozo wa Mali wahusishwa
Alipoulizwa kama kitisho hicho kina uhusiano wowote na operesheni za kijeshi za Ufaransa nchini Mali, waziri wa nchi wa Uingereza anayehusika na masuala ya nchi za nje David Lidington, alisema kitisho hicho kilikuwepo hata kabla.
''Kitisho cha ugaidi katika mji wa Benghazi na katika maeneo mengine katika ukanda ule kilikuwepo kabla ya mzozo wa Mali na kabla ya mgogoro wa wiki iliyopita nchini Algeria. Huwa tunatoa tahadhari na ushauri wa kuondoka kama tulivyofanya sasa kuhusu Benghazi, ikiwa tu tunao ushahidi dhahiri na wa kuaminika kwamba kitisho kilichopo ni bayana.'' Alisema Lidington.
Hata hivyo, wizara ya mambo ya nchi za nje ya Uingereza imesema kuwa kuingilia kwa Ufaransa katika mzozo wa Mali kumeongeza uwezekano wa mashambulizi dhidi ya raia wa nchi za magharibi.
Marekani yajitenga
Nchi nyingine ambazo ziliwatahadharisha raia wao kuhusu kitisho cha usalama katika mji wa Benghazi ni Uholanzi na Australia, lakini Marekani imesema kuwa inaamini kuwa kitisho cha sasa katika mji huo kinawalenga raia wa nchi za Ulaya, sio wamarekani.
Shirika la ndege la Malta liliahirisha safari ya ndege yake mjini Benghazi, kwa kuzingatia onyo la wizara ya mabo ya nchi za nje ya Uingereza.
Hatua hiyo ya nchi za magharibi imeikasirisha Libya, ambayo imesema kuwa taarifa za kitisho cha usalama hazina msingi wowote. ''Wizara ya mambo ya ndani ya Libya inakanusha vikali taarifa za kuwepo kwa kitisho cha usalama wa raia wa kimagharibi na wakazi wa Benghazi, na inatoa hakikisho la usalama na utengamano katika mji huo'' limeripoti shirika la habari la Libya, LANA, likimnukuu afisa wa wizara hiyo.
Kuna raia wachache kutoka nchi za magharibi katika mji wa Benghazi, ambao umeshuhudia mashambulizi kadhaa dhidi ya wanadiplomasia wa kigeni, na pia dhidi ya vituo vya jeshi na polisi.