Adverts

Feb 7, 2013

DC AWALIPUA POLISI, KUMBE WANAWABAMBIKIZIA KESI ILI WAPATE CHAMBI CHAMBI!


Na Danny Tweve  Mbozi
Mkuu wa wilaya Mbozi Dk MICHAEL KADEGHE

Mkuu wa wilaya ya Mbozi Dr Michael Kadeghe amesema, msongamano wa mahabusu unatokana na vitendo vya baadhi ya askari polisi kuwafungulia mashtaka yenye ugumu wa dhamana makusudi ili kuwafanya wapate rushwa kubwa wakati wa hatua za kubadilisha mashkataka hayo
Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya sheria wilayani Mbozi, Mkuu huyo wa wilaya amesema katika ziara aliyoifanya katika gereza la Mbozi amebaini asilimia 90 ya mahabusu walioko humo wana kesi ya ujambazi wa kutumia siraha na mauaji.
Alisema katika mahojiano na watuhumiwa hao mmoja wao alimweleza kuwa alikuwa ameiba simu mfukoni kwa mtu lakini akaandikiwa shtaka la ujambazi wa kutumia silaha wakati mwingine alipewa kazi ya kumuua mzungu wakati hakujawahi tokea mauaji ya mzungu katika eneo hilo.
Katika ufafanuzi huo anaeleza kuwa polisi kutokana na kupewa nafasi ya kufungua mashtaka wamekuwa wakitumia fulsa hizo kuwabambikiza kesi kubwa wananchi ili wapate rushwa kubwa  hali ambayo inaathiri utawala wa sheria .
Alisema kutokana na mfumo wa kesi za namna hizo ambazo nyingi zinakuwa hazina majalada na hivyo kukosekana  mwendelezo  wakati wa kufuatilia kwenye mahakama zenye mamlaka ya kusikiliza  zimesababisha watuhumiwa kubakia mahabusu kutokana na uwezo wa mahakama za chini kusikiliza mashtaka ya namna hiyo.
“kuna mtu nimemkuta amepewa kesi ya mauaji ya mzungu, lakini faili lake lenye kesi  ya namna hiyo halipo, lakini yupo mahabusu, mwingine nimemkuta ana kesi ya wizi wa simu lakini ameongezewa shtaka la ujambazi wa kutumia silaha  ili tu asiweze kuapata dhamana “ alifafanua Mkuu huyo wa wilaya Mbozi
Kwa upande wake hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya za Mbozi na Momba bwana Rahim Mushi amesema licha ya mafanikio makubwa ya kupunguza msongamano wa mahabusu kwa kuzitolea hukumu .
 Akifafanua kwa takwimu hakimu Mushi amesema mwaka 2010 kulikuwa na wafungwa na mahabusu 300 katika gereza la Mbozi  lakini hadi kufikia decemba  30 mwaka huu wafungwa na mahabusu walioko kwenye gereza hilo wamepungua hadi  kufikia 180.
Hata hivyo amekiri kuwepo  changamoto ya ongezeko la kesi za mauaji ambazo zimeendelea kufunguliwa na hivyo kusababisha mikono ya mahakama ya wilaya kutokakuwa na uwezo wa kushughulikia kesi hizo na kuendelea kuchangia msongamano wa mahabusu.
Alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo, mahakama inajipanga kutoa elimu kwa wananchi ili kuwawezesha kufuata utawala wa sheria na kwamba kupitia uataratibu huo matukio ya uhalifu yatapungua katika jamii.
Aidha amepongeza hatua ya idara ya mahakama kuajiri mahakimu wakazi 6 ambao watasambazwa katika mahakama za Mwanzo wilayani Mbozi, na kwamba hatua hiyo itaachangia kupunguza mlundikano wa kesi katika mahakama hizo

Naye mkuu wa wilaya ya Momba Abiud Saidea alilieza kukabiliwa na changamoto ya kesi za mauaji ya ushirikina ambayo yamesababisha vifo vya watu wengi katika kipindi cha mwishoni mwa mwaka jana na January mwaka huu.
Alisema miongoni mwa hatua walizozihchukua ni pamoja na kufanya kampeni za kuwaelimisha wananchi kuacha kutumia waganga wapiga ramli katika kushughulikia matatizo yanayowakabili na badala yake kuzingatia mfumo rasmi wa kisheria uliopo katika kuwasilisha malalamiko yao na hatimaye kuondokana na mauaji holela.
Alisema vitendo hivyo vimeleta madhara makubwa na mifarakano katika jamii akitolea tukio la vifo vya watu wawili katika kijiji cha Kalungu hivi karibuni ambapo watu walizikwa wakiwa hai na kusababisha mifarakano katika jamii kutokana na waganga wapiga ramli kuchochea hali hiyo.
mwisho