Mwanamke mmoja mkazi wa kitongoji cha Seif katika
kijiji cha Chiwezi-Mpemba TABU MWASHITETE
anashikiriwa na polisi wilayani Momba kwa tuhuma za kuumuuza mtoto wake
wa kumzaa mwenye umri wa miaka mitano kwa shilingi 100,000/=
Tukio hilo limetokea
jana majira ya saa 12 jioni baada ya majadiliano ya biashara hiyo yaliyodumu
kwa saa 7 baina ya muuzaji na mnunuzi.
Akizungumzia mchezo
ulivyokuwa mpaka kumkamata mtuhumiwa, Bwana John Sinyinza ambaye alishakuwa
mtumishi wa umma na kustaafu anaeleza kuwa alifuatwa na Bi Tabu majira ya saa
tano asubuhi nyumbani kwake.
Anaeleza kuwa katika
mazungumzo na mama huyo alishitushwa
alipoambiwa kuwa anamuuza mtoto ambaye amemtoa Malawi na kwamba lengo la
kumuuza anataka kupata fedha kwaajili ya kugharimia kumtoa baba yake mzazi wa
mtoto huyo ambaye amefungwa nchini Malawi.
Hata hivyo katika
majadiliano ya biashara hiyo, mwanamke huyo alitaka kulipwa kiasi cha shilingi
1,000,000/=(Milioni Moja) ambapo walikubaliana kuwa wangeuziana majira ya saa
12 jioni baada ya kupatikana kwa fedha hizo.
Ndipo bwana Sinyinza
kutokana na tukio hilo kutokuwa la kawaida aliwasiliana na vyombo vya usalama
na kupewa askari wa kike wa upelelezi ili waongozane eneo la tukio ambapo
katika mtego wa kufanyika biashara hiyo, mwanamke huyo alifika akiwa na mwanaye
ambaye alikuwa uchi ili wakabidhiane.
Bwana Sinyenga katika
kuhakikisha kuwa mwanamke huyo hashtukii mchezo alimtambulisha askari huyo kama
binti yake na kwamba walikubaliana kulipata fedha hizo kwa awamu ambapo
angemlipa shilingi 100,000/= kwanza na kesho yake angemaliziwa kiasi cha
shilingi 900,000/= zilizobakia.
Kufuatia makubaliano
hayo mwanamke huyo alimkabidhi mtoto wake kwa mnunuzi na baadaye kuagana kwa makubaliano kuwa angepewa kiasi
kilichobakia na binti huyo wa upelelezi kesho yake.
Baada ya mteja kutoweka na “bidhaa ya mtoto” ndipo askari wa upelelezi huyo alipomweka chini ya
ulinzi bi mkubwa huyo na baadaye kufikishwa
kituo ch polisi cha Tunduma ambako
katika mahojiano imebainika kuwa mtoto huyo ni mwanaye ambaye baba yake alishafariki.
Alisema kuwa kutokana
na ugumu wa maisha aliamua kumuuza mtoto wake huyo ili apate fedha kwaajili ya
shughuli za kiuchumi kama mtaji na kwamba anatambua kuwa wanunuzi wangeweza
kumuua mtoto huyo ama kwa matumizi mengine!
Kulingana na fununu za
jeshi la polisi mwanamke huyo atafikishwa mahakamani kesho jumatano katika
mahakama ya wilaya ya Mbozi